Rafiki yangu mpendwa,

Kama ambavyo wahenga walivyosema, kila chenye mwanzo huwa kina mwisho wake. Tulilianza juma namba 28 la mwaka huu 2018, na sasa tunakwenda kumaliza juma hili.

Lakini imani yangu ni kwamba, yale makubwa na mazuri uliyojifunza kwenye juma hili, zile hatua ambazo ulichukua, zitaendelea kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi na zaidi.

Na kama mtu mmoja alivyowahi kusema, miaka 10 ijayo utajitia zaidi yale ambayo hukufanya kuliko ambayo ulifanya na kushindwa. Utajiambia ningejua ningefanya hivi au vile, lakini utakuwa umechelewa sana na chochote ulichotaka kufanya kwa muda huo hakifai tena.

Hii inatukumbusha kitu kimoja muhimu sana kwetu rafiki, kwamba chochote ambacho ni muhimu kwetu kufanya, basi tunapaswa kukifanya sasa, siyo kesho, siyo tukiwa tayari, bali sasa.

Karibu kwenye tano za juma, ambapo nakukusanyia mambo matano muhimu ya kujifunza na kuchukua hatua ili maisha yako yazidi kuwa bora zaidi. Kumbuka nimekuwa nakuambia, uko hapo ulipo sasa kutokana na unachojua na ulichofanya, ili kuondoka hapo na kwenda mbele zaidi, lazima ujue zaidi na ufanye zaidi.

KURASA ZA MAISHA YA MAFANIKIO

Karibu kwenye tano za juma, ujue zaidi, halafu ukikamilisha kwa kuchukua hatua, utaweza kufika mbali zaidi.

#1 KITABU NILICHOSOMA; HEKIMA YA MAISHA YA FURAHA.

Moja ya vitabu nilivyosoma juma hili ni kitabu THE WISDOM OF LIFE kilichoandikwa na mwanafalsafa Arthur Schopenhauer.

Arthur alikuwa mwanafalsafa wa Ujerumani, ambaye alikuwa na falsafa ngumu sana kuhusu maisha yetu sisi wanadamu. Wengi sana walikuwa hawazielewi falsafa zake kwa sababu hakuwa anapindisha maneno, alikuwa anaeleza kama yalivyo. Kwamba kwa sehemu kubwa maisha ni mateso na watu wengi wataishi maisha ya mateso hapa duniani, kama hawatajua kile kweli kinacholeta maisha ya furaha na mafanikio.

Kwenye kitabu hichi cha THE WISDOM OF LIFE Arthur ameyagawa maisha ya mwanadamu kwenye makundi makuu matatu.

Kundi la kwanza ni mtu kama mtu, haiba ya mtu na kile ambacho kipo ndani ya mtu.

Kundi la pili ni mali ambazo mtu anazo, kile ambacho mtu anamiliki.

Kundi la tatu ni nafasi ambayo mtu anayo kwenye jamii, jinsi anavyochukuliwa na wengine.

Arthur ametushirikisha njia bora ya kuyaendesha maisha yetu kwenye maeneo haya matatu ya maisha yetu ili tuweze kuwa na maisha yenye furaha na mafanikio.

Hapa nakwenda kukushirikisha mambo kumi niliyojifunza kwenye kitabu hichi, ambayo unaweza kuyafanyia kazi na maisha yako yakaa bora zaidi.

  1. Msaada wa nje hauwezi kumsaidia mtu yeyote ambaye ameshajiwekea ukomo ndani yake. Arthur anasema mtu hawezi kujikimbia yeye mwenyewe, kama ambavyo mtu hawezi kuondoka ndani ya ngozi yake. Hivyo mabadiliko ya kweli kwenye maisha ya mtu, lazima yaanzie kwenye utu wake, lazima awe tayari kubadilika yeye mwenyewe. Ukomo wa mtu kwenye maisha, ni ule ambao amejiwekea wewe mwenyewe. Hebu jiangalie ni vitu hani umewahi kukosa kwenye maisha yako na ona kama hakuna ukomo umekuwa unajiwekea wewe mwenyewe.
  2. Njia pekee ya kufanikiwa kwenye maisha, ni mtu kutumia kile ambacho kipo ndani yake, kukifanyia kazi na kuweza kutoa matokeo mazuri. Kila mtu ana kitu ambacho kipo ndani yake, kitu ambacho ni tofauti kabisa na watu wengine. Lakini wengi wamekuwa hawafanyii kazi kilichopo ndani, ila wanakimbizana na vitu vya nje.
  3. Furaha ni kile ambacho kipo ndani ya mtu, na siyo kitu cha nje. Hakuna furaha ambayo imewahi kupatikana kwa kutafuta vitu vya nje. Vitu vya nje vinayafanya maisha yetu yaweze kwenda, lakini furaha ni tunda la ndani. Wanafalsafa wengine wanasema furaha ndiyo hali kuu ya binadamu, ila wengi wamekuwa anaipoteza kwa kutafuta vitu wasivyohitaji, huku wakifikiri ndiyo wanatafuta furaha.
  4. Maisha ni mwendo, kama hakuna mwendo hakuna maisha. Arthur anasema kwa afya nzuri, lazima mwili uwe na mwendo. Kama ambavyo moyo unakuwa na mwendo kila siku, ukisimama hakuna maisha. Lakini watu wamekuwa wanapunguza mwendo kwenye maisha yao, kitu kinachowaathiri sana. Mfano kazi za watu wengi kwa sasa ni za kukaa, hivyo mwili unakosa mwendo, vyakula wanavyokula havitumiki na vinageuka kuwa sumu. Hakikisha kila siku unaupa mwili wako mwendo wa kutosha, kwa mfumo wa mazoezi. Na hata kwenye mengine unayofanya kwenye maisha, hakikisha una mwendo, hakikisha kila siku unapiga hatua na usikubali kabisa kusimama.
  5. Asilimia 90 ya furaha yetu ni zao la afya bora. Afya ikiwa vizuri vitu vingine vyote vinaweza kwenda vizuri. Lakini afya ikiwa hovyo, kila kitu kitakwenda hivyo. Hivyo basi, kipaumbele cha kwanza kabisa kwenye maisha yetu, kinapaswa kuwa afya zetu. Kuhakikisha tunalinda na kuimarisha afya zetu maana ndiyo mtaji namba moja tulionao kwenye maisha yetu.
  6. Kuna maadui wakubwa wawili wa furaha kwa mwanadamu. Wa kwanza ni maumivu(pain) na wa pili ni uchoshi(boredom), na maadui hawa wanakwenda kwa pamoja. Arthur anasema kwamba huwezi kukwepa maadui hao wawili, ukiondoka kwa adui mmoja, unakwenda kwa adui mwingine. Kwa mfano kama huna kitu, unapata maumivu ya kukosa kitu hicho, ukiwa na hicho kitu unakizoea na unapata uchoshi. Njia pekee ya kushinda maadui hawa ni kuwa na utajiri wa akili, kwa sababu kadiri unavyokuwa na maarifa bora, ndivyo unavyokosa nafasi ya kusikia maumivu au kuona uchoshi. Wale wasio na maarifa, wakiwa na kitu shida, wasipokuwa nacho pia shida. Waangalie wengi kwenye fedha, wakiwa hawana shida, wakiwa nazo pia shida.
  7. Ili usiwe tegemezi kwa wengine, lazima uwe na mengi ndani yako, lazima ujue kilichopo ndani yako na uweze kukitumia. Watu wengi wamekuwa tegemezi kwa wengine, wamekuwa watumwa kwa wengine kwa sababu wamejitelekeza wao wenyewe. Wameacha kuangalia kile kilichopo ndani yao na kukitumia na kuhangaika na vile vilivyo kwa wengine. Jijue wewe mwenyewe vizuri, jua kilichopo ndani yako na hutakuwa mtumwa wa mtu yeyote yule.
  8. Maisha ya mpumbavu ni mabaya kuliko kifo. Duh, unaweza kuamini hilo? Yaani kuliko uwe mpumbavu ni afadhali hata ufe kabisa. Maana utateseka kwa kuwa mpumbavu kuliko utakavyoteseka kwa kuwa umekufa. Na hili wala halina upinzani, wewe waangalie wapumbavu wanavyoteseka hata pale ambapo hapahitaji kuwepo na mateso. Kwa maneno mafupi, usiwe mpumbavu, utakuwa mzigo kwako na kwa wengine pia.
  9. Watu wa kawaida huwa wanafikiria jinsi gani watatumia muda wao, watu wenye akili huwa wanafikiria jinsi gani watawekeza muda wao. Na hili pia halina ubishi, mpe mtu wa kawaida muda ambao hana chochote cha kufanya, na atachoka kweli, atazunguka kwenye mitandao, atasema hakuna kipya, atatafuta hata watu wa kuwasumbua nao ataona hawana jipya. Atajikuta amechoka zaidi na hakuna hata kikubwa alichofanya. Lakini mpe mtu mwenye akili muda wa ziada na ataona hata haumtoshi, atatumia muda huo kujifunza, kujenga misingi zaidi kwenye kile anachofanya. Kuwa na akili, wekeza muda wako na siyo tu kukazana kuutumia, isije ikatokea kwa dakika yoyote ya maisha yako ukasema sijui hata nifanye nini kwa muda huu, utapoteza muda unaojiuliza kwa aina hiyo.
  10. Tatizo la kuweka furaha kwenye vitu vya nje au watu wengine ni kwamba, pale vitu hivyo vinapoondoka, na karibu kila kitu huwa kinaondoka, furaha iliyojengwa pale inabomoka kabisa. Ni sawa na kujenga nyumba halafu msingi ukaondoka, hakuna nyumba hapo. Kama unajiambia una furaha kwa sababu una kazi fulani au una gari au nyuma au hata mke/mume au watoto, jua vitu hivyo vyote unaweza kuvipoteza, na hapo ndipo utaona maisha yako hayana maana. Furaha ya kweli ni zao la ndani, zao la kujua maana kubwa ya maisha yako.

Haya ni machache muhimu niliyokushirikisha kwenye kitabu hichi cha HEKIMA YA MAISHA, ni kitabu kizuri, kinachoeleza namna maisha ya msingi, maisha ya falsafa yanavyoweza kuwa maisha ya furaha na mafanikio makubwa. Ndani ya kitabu hichi, Arthur ametushirikisha kuhusu umaarufu na hata sifa, na jinsi ya kuhakikisha vitu hivyo havivurugi maisha yetu.

Fanyia kazi haya niliyokushirikisha na pata muda ujisomee kitabu hichi, utajifunza mengi sana kuhusu maisha ya furaha na mafanikio makubwa.

#2 MAKALA YA WIKI; SIFA SABA ZA KUVUTIA MAFANIKIO KWAKO.

Watu wengi wamekuwa wanataka mafanikio, kabla hawajawa watu ambao wanaweza kuyavutia na kuyatunza mafanikio. Kama umewahi kuona watu fulani ambao walipata mafanikio makubwa kwa haraka bila maandalizi, labda ni kushinda bahati nasibu, au kupata urithi, mafao na hata kupata nafasi ambayo ni  ya bahati fulani, wengi huwa mafanikio hayo hayadumu.

Hakuna lolote la maajabu kwenye mafanikio yanayokuja haraka na kuondoka haraka. Bali kinachotokea ni kwamba watu wanakuwa hawajajijengea sifa zinazovutia na kutunza mafanikio.

Kabla hujaendelea kuyatafuta mafanikio, hakikisha unazo sifa hizi saba zinazovutia na kutunza mafanikio yako. Nimeeleza sifa hizo kwenye makala ya wiki ambayo unaweza kuisoma hapa; Mafanikio Makubwa Huwa Yanaenda Kwa Watu Wenye Sifa Hizi Saba, Zijue Na Ujijengee Ili Uweze Kufanikiwa Zaidi. (https://amkamtanzania.com/2018/07/14/mafanikio-makubwa-huwa-yanaenda-kwa-watu-wenye-sifa-hizi-saba-zijue-na-ujijengee-ili-uweze-kufanikiwa-zaidi/)

#3 TUONGEE PESA; FEDHA NA FURAHA

Kuna watu ambao huwa wanatumia kigezo cha furaha kama sababu ya kutokuwa na fedha. Utawasikia wakijiambia kabisa kwamba sina fedha lakini nina furaha, wale wenye fedha nyingi hawana furaha kama niliyonayo mimi.

Rafiki yangu, kama umewahi kujiambia hivyo kwanza kabisa naomba nikuambie jiombe msamaha, maana umejikosea sana. Pili usirudie tena kufanya hivyo. Kama uliwahi kumsikia mtu akisema hivyo, au kama kuna watu wanaokuzunguka wanasema hivyo, anza kukaa nao mbali mara moja, maana watapelekea utengeneze matatizo mengi kwenye maisha yako.

Huhitaji fedha kwa ajili ya furaha, hiyo tu dhana ya kuifikiria fedha na furaha kwa wakati mmoja ni kosa kubwa. Ni kweli fedha haileti furaha, lakini hiyo siyo sababu ya wewe kuacha kutafuta fedha. Ni mpumbavu pekee anayeweza kusema hahangaiki na fedha kwa sababu ana furaha bila kuwa na fedha.

Tunapozungumzia fedha siyo kwa sababu ya furaha, bali ni kwa sababu ya umuhimu wake. Tunaishi kwenye zama ambazo kitu pekee unachoweza kupata bila ya fedha ni pumzi, na hapo ni iwe hujaumwa. Lakini vitu vingine vyote, vinahitaji fedha.

Pia fedha ni nzuri kwenye ulimwengu tunaoishi kwa sababu ndiyo njia pekee ya kupima thamani. Hivyo kama unapata fedha, ni kiashiria kwamba unatoa thamani kwa wengine, kwamba unayafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi.

Na kama hupati fedha, tunaweza kusema bila ya shaka kwamba kuna uzembe na uvivu ambao unaufanya mahali. Kuna namna ambavyo hutoi thamani kubwa kwa wengine.

Sasa kwa kuwa wengi hawapendi kukubali wana uzembe na uvivu ndani yao, basi hutafuta sababu za kijinga pale ambapo wanakuwa hawana fedha. Sababu kama hizo kwamba fedha haileti furaha. Nakuomba rafiki yangu, usitumie tena sababu hiyo, jiambie ukweli pale unapokuwa hutengenezi fedha na chukua hatua sahihi kutengeneza fedha.

#4 HUDUMA ZA KOCHA; SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018.

Rafiki yangu katika mafanikio, kila mwaka huwa nakuandalia semina tatu, mbili kwa njia ya mtandao na moja ya kukutana ana kwa ana, yaani live au kama wanavyosema mubashara. Juma hili nimetoa taarifa za semina hii ya kukutana ana kwa ana ya mwaka huu 2018. Pia nimeeleza mpango bora wa malipo kwako ili usikose nafasi hii bora sana kwako.

Kupata taarifa kamili za semina hii, na hatua za wewe kuchukua ili usiikose, fungua hapa; https://amkamtanzania.com/2018/07/13/karibu-kwenye-semina-ya-kisima-cha-maarifa-2018-mafanikio-biashara-na-uhuru-wa-kifedha/

Rafiki yangu, kama utakosa semina hii, utakuwa tu umetaka kukosa, na siyo sababu nyingine yoyote. Chukua hatua sasa ili usikose semina hii, maana haitakuacha kama ulivyo sasa.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; CHA KUFANYA ASUBUHI, MCHANA, JIONI NA USIKU.

“Think in the morning. Act in the noon. Eat in the evening. Sleep in the night. – William Blake”

Kitu ambacho nimekuwa nakiona kwa wengi wanaolalamika kwamba hawana muda wa kutosha kufanya yale muhimu, ni kwamba hawana utaratibu wowote na muda wao. Wengi wanaanza siku kama ajali, wanarukia kila kinachokuja mbele yao kama nyani anavyorukia tawi la mti analoona. Siku inaisha na hawaoni kikubwa ambao wanakifanya.

Unapoianza siku yako unakuwa na nguvu kubwa, na unapoimaliza nguvu zinakuwa zimeisha kabisa. Mfano mzuri wa kuichukulia siku yako na nguvu zako ni kutumia simu. Ukichaji simu usiku na asubuhi ikawa na chaji asilimia 100, kila unavyoendelea kuitumia chaji inapungua. Mpaka inapofika usiku tena, unakuta chaji ipo chini ya asilimia 10 na inakuletea taarifa kwamba simu itazima muda siyo mrefu.

Kauli hii ya mwandishi William Blake niliyoshirikisha hapo juu, inaweza kutupa picha nzuri sana ya jinsi ya kuiendea siku yetu.

Fikiri asubuhi; huu ndiyo muda mzuri wa kufikiri na kufanya zile kazi ambazo zinahitaji umakini wetu. Kwa sababu asubuhi unakuwa na nguvu za kutosha.

Chukua hatua mchana; mchana ndiyo muda mzuri kwako kufanya kazi zinazokuhitaji kutumia nguvu. Hapo akili yako unakuwa umeshaitumia kufikiri na kupanga yale muhimu, na mchana wako unakuwa mzuri kwa kazi za nguvu.

Kula jioni; ni muhimu sana upangilie ulaji wako, maana mara nyingi ukila kabla hujafanya kazi, unachoka sana na kushindwa kufanya kazi yako vizuri. Kula jioni baada ya kuwa umemaliza kazi zako muhimu.

Lala usiku; usiku ndiyo wakati mzuri kwako kulala, wakati wa kupumzisha mwili wako ili kesho uamke ukiwa na nguvu mpya.

Je kuna njia rahisi ya kutumia muda wako na kuisimamia siku yako kama hii? Inaweza kuwepo, lakini hii naiona ni bora zaidi na yeyote anaweza kuitumia.

Rafiki yangu, nikutakie kila la kheri kwenye juma namba 29 tunalokwenda kuanza, nenda kaishi kwa hekima kubwa kama alivyotushirikisha Arthur, nenda kajijengee sifa zinazovutia mafanikio, tengeneza fedha za kutosha na usichanganye fedha na furaha, jiandae na semina ya KISIMA CHA MAARIFA 2018 na FIKIRI ASUBUHI, CHUKUA HATUA MCHANA, KULA JIONI NA LALA USIKU.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Usomaji