Rafiki yangu mpendwa,
Mimi binafsi huwa naamini sana kwenye kazi, naamini mno kwenye kuweka juhudi binafsi ili kuweza kupata matokeo bora sana kwenye kila tunachofanya kwenye maisha yetu.
Na hata ukiangalia, wale ambao wamefanikiwa sana, ni wale wanaoweka juhudi kubwa kwenye kile wanachofanya. Wanaotoa thamani kubwa na hata kwenda hatua ya ziada.
Lakini wapo watu ambao wanaweka juhudi kubwa, wanafanya kazi sana miaka na miaka ila hakuna hatua kubwa ambazo wamepiga. Wanajituma sana, wanaonekana kuwa wametingwa muda wote, lakini wako pale pale ambapo wamekuwepo miaka yote.
Kama wewe ni mmoja wa watu hao ambao umekuwa unaweka juhudi kubwa ila hufanikiwi, zipo sababu kubwa saba zinazokuzuia usifanikiwe licha ya juhudi unazoweka. Kwenye makala hii nakwenda kukushirikisha sababu hizo na hatua za kuchukua ili juhudi unazoweka ziweze kuzaa matunda.
- Hujui kwa hakika nini hasa unataka.
Hitaji la kwanza kabisa la kufanikiwa kwenye maisha ni kujua kwa hakika nini unataka. Lazima ujue kwa uhakika kabisa na uweze kumweleza mtu yeyote kwa lugha rahisi ni nini unataka na unapataje kile unachotaka. Lazima kile unachotaka kiwe wazi, kinahesabika na kina muda wa kufikia.
Kwa mfano kusema kwamba unataka fedha nyingi, hapo hujui unachotaka. Kwa sababu fedha nyingi ni kiasi gani? Kama una elfu moja, elfu kumi ni fedha nyingi. Je hicho ndiyo unataka? Kama unachotaka ni fedha nyingi, basi weka kabisa kiasi hicho cha fedha unachotaka. Labda ni milioni kadhaa, au bilioni kadhaa, taja namba kabisa na weka muda wa kupata kile unachotaka.
Watu wengi huwa hawapendi kujifunga kwenye kiasi wala kwenye muda kwa sababu wanaogopa kushindwa. Wanaona wakisema watapata kiasi fulani cha fedha ndani ya muda fulani, wakishindwa kutimiza hilo watu watawaona hawafai. Hivyo wanabaki na malengo ambayo yapo wazi, ambayo hawawezi kuonekana wameshindwa.
Jua kwa hakika ni nini unataka, kiwe kinapimika na ujiwekee muda wa kukipata. Kwa namna hii, juhudi utakazoweka zitakuelekeza kwenye kile unachotaka na muda utakuwa hamasa kwako kuchukua hatua kubwa na sahihi.
- Bado hujawa tayari kulipa gharama kubwa.
Kupata mafanikio makubwa kunahitaji kulipa gharama kubwa. Siyo watu wote wapo tayari kulipa gharama kubwa ya mafanikio. Hivyo unaweza kuwaona watu wanakazana sana kwenye kile wanachofanya, kumbe wanafanya hivyo kuepuka kulipa gharama wanayopaswa kulipa ili wafanikiwe.
Ili kufanikiwa, huhitaji tu kufanya kazi kwa sababu ipo, bali unapaswa kujua ni gharama gani hasa unapaswa kulipa ili kupata kile unachotaka, kisha kuwa tayari kulipa gharama hiyo.
Kama umeshajua nini hasa unataka, na gharama unayopaswa kulipa ili kukipata, kitu kingine chochote utakachofanya ambacho siyo cha kulipa gharama hiyo ni kujipoteza tu wewe mwenyewe. Chochote utakachofanya ambacho hakichangii kwenye gharama, kinakuzuia wewe kufanikiwa.
Jua gharama unayopaswa kulipa na usipoteze hata dakika yako moja kufanya mambo ambayo hayakupeleki wewe kwenye kulipa gharama.
- Huweki juhudi eneo moja kwa muda mrefu.
Hata baada ya kujua kile hasa unachotaka, na kuwa tayari kulipa gharama kukipata, bado haitakuwa rahisi kwako kupata kile ambacho unataka. Kwanza utahitaji kuweka muda wa kutosha ili kupata kile unachotaka. Kuna wakati utaweka juhudi na zitaonekana kama hazisaidii chochote. Hapo ndipo wengi hukata tamaa na kuona wanachofanya hakiendelei, hivyo kubadili na kufanya mengine.
Unahitaji kuweka juhudi zako eneo moja kwa muda mrefu, kama ambavyo unachemsha maji, lakini hayachemki mpaka yanapofikia nyuzi joto fulani, haimaanishi moto ulioweka mwanzo haukuwa na msaada, ila ulikuwa haujatosha kupandisha nyuzi joto mpaka kufikia kuchemka.
Unapoweka juhudi, kuwa mvumilivu, jua itakuchukua muda kupata unachotaka. Usiwe mtu wa kukata tamaa haraka na kujaribu mambo mengine, endelea kuweka juhudi mpaka upate kile unachotaka.
- Umetawanya sana nguvu zako.
Juhudi unazoweka kwenye kazi zako, lazima ziwe zimelenga kwenye yale maeneo muhimu yatakayokufikisha kwenye kile hasa unachotaka. Lazima uwe na vipaumbele kwa sababu yapo mambo mengi ya kufanya na huna muda wala nguvu za kufanya kila kitu.
Usiwe mtu wa kukazana kufanya kila kitu, bali kuwa mtu wa kuweka vipaumbele, kuelekeza nguvu zako kwenye yale maeneo muhimu ambayo yatakufikisha kule unakotaka kufika. Kukazana kufanya kila kitu kwa sababu tu unaweza kufanya au kimejitokeza mbele yako, ni kupoteza muda wako na nguvu zako pia.
- Unatafuta njia ya mkato, ambayo haipo.
Kama umewahi kukimbizana na fursa zaidi ya tatu, na zote hazijawahi kukupa kile unachotaka, uwezekano wako wa kupata mafanikio makubwa ni mdogo sana. Kwa sababu inaonekana unatafuta njia ya mkato, ambayo haijawahi kuwepo na hivyo utapoteza muda wako na nguvu zako na hutafanikiwa. Licha ya kuonekana unajituma sana kwenye kila fursa, juhudi zako hazitasaidia kwa sababu akili yako haijatulia sehemu moja na nguvu zako umezitawanya.
Ninachosema hapa ni ile hali ya wewe kukimbizana na kila fursa mpya. Mfano umesikia kilimo cha tikiti ni fursa kubwa, ukaanza kulima, kabla hata hujafika mbali, ukasikia ufugaji wa kware ni fursa kubwa mno, ukaacha kulima tikiti ukaenda kufuga kware, hujafika mbali unasikia ufugaji wa sungura ndiyo habari ya mjini, unaachana na kware na kuanza kukimbizana na sungura. Utaendelea kukimbizana na kila fursa hivyo na mwishi wa siku unakuja kustuka miaka 20 imepita na hakuna hatua kubwa umepiga. Licha ya kuwa mtu wa kujituma sana kwenye fursa.
Hiyo ni kwa sababu unakuwa hujajua nini hasa unataka, na hujaweka juhudi za kutosha kwenye chochote unachofanya.
- Unafanya ili kuonekana na siyo kuwa.
Kuna watu huwa wanafanya vitu, siyo kwa sababu wanataka kufanya, siyo kwa sababu ni muhimu kwao, ila kwa sababu wanataka kuonekana nao wanafanya. Sasa kama kuna kitu chochote unachofanya kwenye maisha yako, ambacho unafanya ili tu uonekane na wewe unafanya, kuwa na uhakika na hili, hutaweza kufanikiwa kwenye kufanya kitu hicho.
Na matatizo yanarudi pale pale, kwamba unakuwa hujajua nini hasa unataka, hivyo juhudi zozote unazoweka ni za juu juu tu kwa sababu unataka kuonekana na wengine, siyo kuwa au kufikia pale unapotaka.
Tatizo la kutaka kuonekana au kuwaridhisha wengine ni kwamba, watu hawana msimamo, wanabadilika sana. Hivyo hutaweza kuwaridhisha watu kwa chochote, licha ya kubadilika badilika kama wanavyobadilika wao.
Chochote unachofanya, fanya kwa sababu ni muhimu kwako kufanya, fanya kwa sababu kina maana kwako kufanya na kamwe usifanye kwa sababu unataka kuonekana ukifanya.
SOMA; ONGEA NA COACH; Aina Kuu Mbili Za Kipato Na Jinsi Ya Kuzitumia Kufika Kwenye Utajiri.
- Unaridhika haraka na mafanikio madogo.
Kuna watu wanajua kabisa nini wanataka kwenye maisha yao, na wanajitoa kuweka juhudi kubwa ili kukipata. Wanaweka juhudi kubwa kweli na shida inakuja pale wanapoanza kupata mafanikio madogo, yanawazuia kabisa wasiendelee kupata mafanikio makubwa.
Kama unaridhika na mafanikio madogo unayopata, hutaweza kupata mafanikio makubwa. Kama ukipiga hatua kidogo unaanza kupata hofu kwamba ukipiga hatua zaidi utapoteza kile ambacho tayari umeshapata, hutaweza kuiga hatua kubwa.
Hivyo unaweza kukuta mtu anakazana sana kwenye maisha, lakini hapati mafanikio makubwa, kwa sababu anakuwa anaweka juhudi kwenye kulinda mafanikio madogo aliyopata, badala ya kutafuta makubwa zaidi. Yaani ni sawa na timu ya mpira ifunge goli moja, halafu isiendelee kushambulia, badala yake ilinde goli lake ili isifungwe.
Kwenye maisha kama hushambulii huwezi kufanikiwa. Acha kuridhika na mafanikio madogo, acha kuhofia kupoteza kidogo ulichopata na kuwa mshambuliaji, kila siku kuwa kama ndiyo unaanza na juhudi zako zitazaa matunda sana.
Rafiki yangu, epuka sababu hizi saba zisiwe kikwazo kwako kufikia mafanikio makubwa. Na kama ambavyo nimekuwa nakuambia mara kwa mara, upo hapo ulipo sasa kwa sababu yako mwenyewe. Ni wewe mwenyewe ambaye umejizuia usifanikiwe zaidi. Hebu jiachie sasa na utaweza kupiga hatua kubwa sana kwenye maisha yako.
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha