Rafiki yangu mpendwa,

Maamuzi muhimu sana unayoweza kufanya kwenye maisha yako, ni kuifanya kazi yako. Na kuwaacha wengine wafanye kile walichochagua kufanya.

Pale unapokutana na hali ya kukata tamaa, ifanye kazi yako, kila unapofanya kitu, unabadili hali uliyonayo.

Kila unapotamani kulalamika na kulaumu wengine kwa mambo yaliyotokea, ifanye kazi yako, ukiwa umetingwa na kazi, hutapata muda wa kulalamika na kulaumu wengine.

Kila wengine wanapokusema vibaya, kukukatisha tamaa au kukupa hofu, ifanye kazi yako. Kwa kutingwa na kazi yako hutaweza kumsikiliza mtu mwingine yeyote.

Kila unapokutana na ugumu kwenye maisha yako, ifanye kazi yako, ugumu wowote utakukimbia pale utakapogundua kwamba umetingwa na kazi yako.

Rafiki, kama maisha yako ni magumu kwa namna yoyote ile, anzia kwenye kazi yako, ifanye kazi yako, weka kazi yako kuwa kipaumbele cha kwanza kwako.

Amka asubuhi ukiwa na hamasa kubwa ya kuifanya kazi yako, na lala ukiwa umeshapanga nini unafanya utakapoamka.

652d5-tangazo2bmasikini

Ifanye kazi yako rafiki, na ifanye kazi yako kwa misingi hii mitatu;

MOJA; Ifanye kazi yako kwa juhudi kubwa sana, asiwepo mwingine anayeweka juhudi zaidi yako, hili lipo ndani ya uwezo wako, lifanye.

MBILI; Ifanye kazi kwa uaminifu wa hali ya juu sana, timiza unachoahidi, simamia unachosema na kuamini, hili lipo ndani ya uwezo wako, lifanye.

TATU; Ifanye kazi yako kwa kuwasaidia wengine kwa kadiri uwezavyo, jinsi unavyowasaidia wengi zaidi, ndivyo unavyopata kile unachotaka. Hili pia lipo ndani ya uwezo wako, ni wewe kuchukua tu hatua.

Ifanye kazi yao rafiki, ifanye asubuhi, ifanye mchana na ifanye usiku.

Kama unaanzia chini kabisa, kama huna chochote, basi ni vyema ukaifanya kazi yako muda wako wote. Kwa sababu kama huna chochote, una ukomo kwenye nini unaweza kufanya, lakini huna ukomo kwenye kuifanya kazi yako. Hivyo ifanye kazi yako.

Na ninaposema ifanye kazi yako simaanishi kazi ya kuajiriwa, bali chochote ulichochagua kufanya. Iwe umechagua kufanya biashara ndogo, kuajiriwa na mtu au kutoa muda wako kwa wengine. Ifanye kazi yako kwa misingi mitatu niliyokushirikisha hapa.

SOMA; Sababu Hizi Saba Ndiyo Zinakuzuia Kupata Mafanikio Makubwa Licha Ya Wewe Kuwa Na Juhudi Kubwa Kwenye Kazi Zako.

Ifanye kazi yako, kwa sababu ndiyo kitu pekee ambacho hakitakutupa hata kama mambo yatakuwa magumu kiasi gani. Kazi yako itasimama na wewe kama wewe utasimama nayo.

Ifanye kazi yako, kwa sababu hakuna aliyewahi kushindwa kwa kuwa alifanya kazi sana, na tunajua wengi waliofanikiwa wamefanya kazi sana.

Waache wengine wafanya yale waliyochagua kufanya, usiwahukumu wala kuwasema vibaya, peleka muda huo kwenye kuifanya kazi yako.

Ifanye kazi yako, kwa sababu ndiyo kitu pekee ambacho hakitakuangusha kwenye maisha yako.

Ifanye kazi yako, kwa sababu ndiyo kitu pekee kitakachokutoa chini kabisa na kukufikisha kwenye mafanikio makubwa.

Ipende kazi yako, ifanye kazi yako, ifikirie kazi yako, iishi kazi yako.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; http://eepurl.com/dDZHvL