Rafiki yangu mpendwa,
Kila mtu anapenda sana kujulikana kwa ubobezi kwenye kile anachopenda kufanya. Lakini ni wachache sana ambao wameweza kufikia ubobezi wa hali ya juu. Wengi wamekuwa wanabaki kuwa wa kawaida kwenye chochote wanachofanya, na hicho kinakuwa kikwazo kwao kupiga hatua zaidi kwenye maisha yao.
Ukiangalia kwenye eneo lolote lile, wale wanaolipwa vizuri ni wale ambao wamebobea sana kwenye kile wanachofanya. Wale ambao wana ujuzi mkubwa na wana uzoefu katika kufanya kitu hicho kwa ubora wa hali ya juu sana ukilinganisha na wengine wanavyofanya.
Kadiri siku zinavyokwenda, ndivyo wabobezi kwenye eneo lolote lile wanakuwa wachache zaidi. Hii inatokana na zama tunazoishi kuwa zama za kelele, ambapo kelele zimekuwa nyingi kiasi kwamba watu wanashindwa kuweka umakini kwenye eneo moja au maeneo machache, wanaishia kutawanya nguvu zao kwenye maeneo mengi na hivyo wasiweze kubobea kwenye chochote.
Sisi binadamu tuna ukomo kwenye vitu vikubwa viwili, muda na nguvu. Kila mmoja wetu ana masaa 24 peke yake kwenye siku yake, na hakuna anayeweza kuongeza muda huo. Lakini pia tuna ukomo kwenye nguvu zetu, unapokuwa unaianza siku yako unakuwa na nguvu nyingi, lakini kadiri siku inavyokwenda, nguvu hizo zinapungua na mpaka siku inaisha unakuwa umechoka kabisa. Hivyo ni muhimu sana kuchagua vizuri wapi tunawekeza muda na nguvu zetu.
Lakini pia hizi ni zama bora kabisa kuwa hai kwa sababu mtu yeyote anaweza kutengeneza ubobezi kwenye eneo lolote bila ya kuzuiwa na chochote. Miaka iliyopita, ili uweze kuwa na ubobezi ilikupasa ujiuge na chuo kikuu, ufundishwe, uhitimu na hapo uweze kutunukiwa ubobezi kwenye kile ulichosomea. Lakini kwa sasa maarifa yametapakaa kila kona, huhitaji tena kujiunga na chuo ndiyo upate ubobezi.
Hivyo kila mtu anaweza kujijengea ubobezi kwenye eneo lolote analochagua kama atakuwa tayari kuweka nguvu na muda wake kwenye eneo hilo.
Mwandishi Dorie Clark kwenye kitabu chake kinachoitwa Stand out : how to find your breakthrough idea and build a following around it, ametushirikisha njia mbalimbali za kujijengea ubobezi na kuweza kujitofautisha na wengine, kitu ambacho kinatupa mafanikio makubwa sana.
Kwenye makala hii tunakwenda kujifunza hatua sita za kujijengea ubobezi kwenye eneo lolote unalochagua, kitu ambacho kitakuwezesha kutoa thamani zaidi na hatimaye kipato chako kiongezeke zaidi. Hatua hizi sita tunajifunza kutoka kwenye kitabu STAND OUT.
Zifuatazo ni hatua sita za kutengeneza ubobezi.
HATUA YA KWANZA; TAFUTA ENEO LA KUBOBEA.
Hatua ya kwanza kwenye kujijengea ubobezi ni kutafuta eneo gani unalotaka kubobea. Na hapa ndipo wengi wanapokwama kwa sababu huwa hawachukui muda wa kujihoji na kutafakari kwa kina ili kuweza kupata eneo wanaloweza kubobea.
Ili kujua eneo gani unaweza kubobea, anza kuangalia vile vitu ambavyo umekuwa unapenda kufanya au kufuatilia tangu ukiwa mtoto. Pia angalia taaluma, ujuzi au uzoefu ambao umeshaupata mpaka sasa kwenye maisha yako. Maeneo hayo yatakuwezesha kujua eneo gani linakufaa zaidi wewe kwa ubobezi.
Lakini bado inaweza kuwa vigumu kujua eneo gani la kubobea, hasa pale unaposhindwa kujua kwa hakika nini unataka. Hapa cha kufanya ni kuchagua kitu chochote unachokipenda, kisha kukifuata hicho na kuona kitakufikisha wapi.
HATUA YA PILI; CHAGUA ENEO MOJA UTAKALOBOBEA.
Katika kutafuta eneo la kubobea unaweza kuwa umejaribu mambo mengi ambayo umekuwa unayapenda. Na huenda maeneo yote unayapenda, lakini huwezi kuanza safari ya ubobezi kwa kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja. Unahitaji kuchagua eneo moja utakalobobea, eneo moja utakaloweka nguvu zako zote kwa muda mpaka uone matokeo bora.
Hapa ndipo wengi hushindwa, kwa sababu huona kuchagua eneo moja na kuachana na mengine ni kujiwekea ukomo kwenye fursa. Lakini huwezi kupata ubobezi kama huweki umakini wako kwenye kitu kimoja au vichache.
Kama inakuwa vigumu kwako kuchagua eneo lipi ubobee katika mengi unayofanyia kazi, basi acha soko lichague. Tengeneza kitu au toa huduma kwenye soko kisha angalia watu wapo tayari zaidi kwa kipi katika vile vingi ambavyo unavifanya.
Hii ni hatua muhimu sana katika zote, kwa sababu ili uweze kubobea, lazima uwe tayari kusema hapana kwa vitu vizuri, ili uweze kusema ndiyo kwa vitu bora.
HATUA YA TATU; TENGENEZA UBOBEZI WAKO.
Baada ya kuchagua eneo moja ambalo unataka kubobea, sasa kazi ya ubobezi inaanza. Na hapa kitu kimoja kikubwa cha kufanya ni kukazana kuongeza thamani zaidi kwa wengine kupitia kile unachofanya. Kitu pekee ambacho watu wanajali ni thamani wanayoipata kutoka kwa wengine.
Hivyo kama utakazana kutoa thamani kubwa zaidi kupitia unachofanya, na kila wakati ukawa mtu wa kujifunza na kuboresha zaidi, utaweza kuwa na ubobezi mkubwa kwenye kile unachofanya.
Watu wengi huwa wanakata tamaa kwenye kutengeneza ubobezi kwa sababu huwa wanafikiria ili wabobee basi wanahitaji kuwa bora kuliko watu wengine wote duniani. Hili siyo sahihi, huhitaji kuwa bora kuliko wote duniani, badala yake unahitaji kufanya kwa ubora kadiri ya unavyoweza. Unapaswa kutoa thamani kubwa sana kwa wengine kupitia kile unachofanya, na kadiri watu hao wanavyonufaika ndivyo watakavyokuwa tayari kukutangaza wewe kwa wengine pia.
HATUA YA NNE; KUJITOFAUTISHA NA WENGINE.
Ili kutengeneza ubobezi wako, unahitaji kujitofautisha na wengine ambao wanafanya kile unachofanya wewe. Lazima kuwe na kitu ambacho watu wanakipata kwako na hawawezi kukipata kwa mtu mwingine yeyote.
Na hili ni rahisi kujua na kutumia kama utajitafakari wewe binafsi na kuangalia maeneo yote ya maisha yako. Angalia uzoefu wako wa nyuma, angalia vipaji ulivyonavyo kisha ona unawezaje kuvitumia kwenye lile eneo unalojenga ubobezi na kuweza kujitofautisha na wengine wanaofanya kile unachofanya.
Hakuna ubobezi kama hakuna kinachokutofautisha na wengine. Lazima kuwe na sababu kubwa ya watu kuja kwako. Lazima watu wajue kuna kitu wanapata kwako ambacho hawawezi kupata kwa wengine.
Na ni rahisi sana kujitofautisha na wengine kama utachagua kuwa wewe. Kama utaacha kuiga na kujilinganisha na wengine na kuchagua kuwa wewe, kwa kuweka utu wako kwenye kile unachofanya, basi utakuwa tofauti kabisa na wengine. Kwa sababu kumbuka hakuna mtu anayefana na wewe kwa kila kitu hapa duniani. Hivyo ukichagua kuwa wewe, utajitofautisha na wengine wote.
HATUA YA TANO; KUJIENDELEZA KWENYE ENEO LAKO LA UBOBEZI.
Kuna watu ambao huwa wanaanza safari ya ubobezi, wanaweka juhudi mwanzoni na wanapata matokeo mazuri. Lakini baada ya muda wanadumaa, hawakui tena na hapo ubobezi wao unapotea.
Ili kuondokana na hali hii unapaswa kuwa mtu wa kujiendeleza kwenye eneo lako la ubobezi. Jiendeleze kila mara kwa kupata na kushiriki mafunzo mbalimbali yanayokufanya kuwa bora zaidi kwenye eneo hilo.
Unaweza kuongeza elimu kwa kujiunga na mfumo rasmi wa elimu, mfano kupata shahada au shahada ya uzamili au uzamivu kwenye kile unachofanya. Unapojiunga na elimu ili kupata shahada ya kwanza au za juu, unapata nafasi ya kujifunza kwa kina.
Lakini pia unaweza kujifunza kupitia wale waliofanikiwa zaidi kwenye eneo unalotengeneza ubobezi wako. Hapa unaweza kuchagua kuwa na menta wa kukuongoza au ukachagua kufanya kazi chini ya wale waliobobea zaidi na wakakuwezesha wewe kupiga hatua pia. Kwa kufanya kazi chini ya wale waliobobea, unajifunza kwa vitendo zaidi.
Njia nyingine ya kujiendeleza kwenye eneo lako la ubobezi ni kutumia maarifa mengi yanayopatikana bure au kwa gharama ndogo. Hapa unahitaji kusoma vitabu vilivyoandikwa kuhusiana na eneo unalojenga ubobezi. Kuhudhuria semina na makongamano mbalimbali yanayohusiana na kile unachofanya na hii itakupa fursa ya kujifunza na kukua zaidi.
Katika safari yako ya ubobezi, hakuna wakati ambapo unaweza kusema umeshajua kila kitu hivyo huwezi kujifunza tena. Kila siku ni kujifunza.
SOMA; Hii Ndiyo Nguvu Kubwa Iliyopo Ndani Yako Na Jinsi Unavyoweza Kuitumia Kufanya Miujiza.
HATUA YA SITA; KUKUZA UBOBEZI WAKO KWENYE MAENEO MENGINE.
Baada ya kubobea eneo moja, watu wataanza kuhitaji msaada wako kwenye maeneo mengine. Watu huwa wanafikiri kwa sababu unajua sana kuhusu eneo fulani, basi utakuwa unajua na maeneo mengine pia.
Na hapa ndipo unapopaswa kuwa makini, kwa sababu wengi kwa kupenda sifa, huwa wanakubali kwamba wanajua kila eneo, na hatimaye kutoa matokeo mabovu na kuharibu ubobezi wao.
Ukishakuwa umebobea sana kwenye eneo moja, sasa angalia maeneo yanayoendana na eneo hilo ulilobobea, ambayo unaweza kubobea pia, lakini hayatakutumia nguvu kubwa kama anayeanza.
Hapa ndipo unapokuza ubobezi wako zaidi na hivyo kufungua fursa nyingi na bora zaidi kwako.
Ni muhimu sana ubobee kwanza kwenye eneo moja kisha utafute maeneo mengine yanayoendana na eneo hilo na kuyabobea pia. Hili linakupa faida ya kutokutumia nguvu kubwa wakati unakuza ubobezi wako. Kwa sababu utatumia rasilimali ulizonazo kwenye ubobezi wako wa kwanza kubobea eneo jingine tena.
Angalia ni maeneo gani yanayohusiana na kile ulichobobea na ona ni thamani ipi kubwa unaweza kutoa kwa wengine kisha toa thamani hiyo. Na kwa kuwa kila mara utakuwa unajiendeleza zaidi, utaweza kukuza zaidi ubobezi wako.
Rafiki, hizo ndiyo hatua sita za kutengeneza ubobezi mkubwa, unaokuwezesha kutoa thamani kubwa kwa wengine na kukuza kipato chako pia.
Kwenye TANO ZA JUMA hili la 28 tutakwenda kujifunza kutoka uchambuzi wa kina wa kitabu hiki, kuona njia sahihi za kutengeneza ubobezi wako na hata jinsi ya kulipwa zaidi kutokana na ubobezi ambao umejitengenezea. Usikose kabisa TANO ZA JUMA hili, kwa sababu zitakwenda kukupa maarifa sahihi ya kusimama na kuonekana ndani ya kundi kubwa la watu wanaopiga kelele.
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha
Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge