Rafiki yangu mpendwa,

Kwa zama tunazoishi sasa, kila mtu anapaswa kuwa kwenye biashara.

Kila mtu anapaswa kuwa na bidhaa au huduma ambayo anaiuza kwa watu wengine moja kwa moja na kutengeneza faida.

Haijalishi unafanya nini, haijalishi una cheo gani, ni muhimu sana uwe na biashara.

Hii ni kwa sababu kama ambavyo kila mmoja wetu anaona, ajira zimekuwa ngumu.

Ajira zimekuwa ngumu kupata na hata ukishaipata kipato chake kimekuwa hakitoshelezi.

Hivyo kadiri siku zinavyokwenda, inakuwa vigumu sana kupata uhuru wa kifedha, muda na hata maisha kwa ujumla kupitia ajira.

Biashara ndiyo njia pekee inayoweza kukupatia uhuru unaotaka kwenye maisha yako.

Kwenye biashara hakuna anayeweza kukuwekea ukomo wa kipato bali wewe mwenyewe. Ukiamua kuwauzia watu kumi ni sawa na ukiamua kuwauzia watu mia ni sawa.

business team.jpg

Pamoja na umuhimu huu wa kila mtu kuwa kwenye biashara, kuna ukweli mchungu ambao umekuwa unawatisha wengi na kuwakatisha tamaa wasiingie kwenye biashara.

Ukweli huo ni huu, asilimia 80 ya biashara zinazoanzishwa hufa ndani ya miaka mitano tangu zianzishwe. Yaani kama kuna biashara 10 zimeanzishwa mwaka huu 2019, mpaka kufika mwaka 2024, biashara 8 kati ya hizo 10 zitakuwa zimekufa kabisa.

Biashara ni ngumu, biashara zina changamoto nyingi, na hili ndiyo limekuwa linawafanya wengi wasite kuingia.

Biashara hazina uhakika wa kipato kama ilivyo kwenye ajira, kuna kipindi unaweza kuingiza kipato kizuri, na kipindi kingine ukawa huna kipato kabisa.

Pamoja na changamoto hizi za kibiashara, wapo wengi ambao wameweza kufanikiwa. Na hawa walioweza kufanikiwa ni kwa sababu kuna vitu wamekuwa wanafanya tofauti na wale wanaoshindwa.

Mwandishi Bill Murphy kwenye kitabu chake kinachoitwa The Intelligent Entrepreneur ametushirikisha sheria kumi ambazo wajasiriamali wenye mafanikio makubwa wamekuwa wanazifuata na kuweza kufanikiwa sana.

Kwenye kitabu hiki, ameshirikisha hadithi ya wahitimu wa tatu wa shule maarufu ya biashara duniani, Havard Business School, maisha yao tangu wanajiunga na chuo hicho, wanahitimu na kwenda kuanza biashara. Watu hao watatu walipitia magumu mengi, lakini mwishoni waliibuka washindi.

Bill amekusanya masomo kumi kutoka kwa wajasiriamali hawa na kutushirikisha kwa njia rahisi kwa kila mmoja wetu kuelewa na kuweza kuchukua hatua.

Kwenye makala hii ya leo nakwenda kukushirikisha moja ya sheria hizi, halafu kwenye makala ya TANO ZA JUMA hili la 43 nitakwenda kukushirikisha sheria zote 10 za kufanikiwa kwenye ujasiriamali.

Sheria ya 4 katika sheria 10 za mafanikio kwenye ujasiriamali, Bill anaiita; You can’t do it alone, akimaanisha HUWEZI KUFANYA PEKE YAKO.

Rafiki, kama kweli unataka kufanikiwa kwenye biashara na ujasiriamali, basi unapaswa kujua kitu hiki muhimu sana, huwezi kufanya kila kitu peke yako. Unaweza kuanza mwenyewe mwanzoni, lakini kadiri biashara inavyokua, unahitaji kuwa na watu wa kukusaidia majukumu mbalimbali.

Wajasiriamali wengi huwa wanaanza vizuri mwanzoni, pale biashara inapokuwa ndogo na wanafanya kila kitu wenyewe. Biashara inapokuwa kubwa na kuhitaji watu wa ziada wa kumsaidia, hapo ndipo matatizo mengi huanza kuibuka na kupelekea biashara kushindwa.

Kumbuka, hakuna kitu kigumu kama kuwaongoza watu, na kwenye biashara siyo tu inabidi uwaongoze, bali pia inabidi uwahamasishe kila mara ili waweze kutekeleza majukumu yao na hasa pale mambo yanapokuwa magumu.

Ili kufanikiwa kwenye ujasiriamali, unapaswa kujenga timu bora ambayo itakuwa na ushirikiano mzuri, itajituma sana na kuweza kuzalisha matokeo makubwa.

SOMA; Hatua Sita (06) Za Kutengeneza Ubobezi Kwenye Kile Unachopenda, Kutoa Thamani Zaidi Na Kuongeza Kipato Chako.

Kwenye kitabu hiki cha The Intelligent Entrepreneur Bill Murphy ametushirikisha hatua tano za kuchukua katika kutengeneza timu bora itakayokuwezesha kufanikiwa kwenye biashara.

Hatua hizo tano ni kama ifuatavyo;

Moja; penda sana ile biashara unayoifanya.

Hatua ya kwanza kwako ni kupenda sana ile biashara ambayo unaifanya. Unapopenda unachofanya, watu wengine wanaona na kuvutiwa kufanya kazi na wewe pia.  Unapopenda unachofanya, wale unaowaajiri wakusaidia nao watajikuta wanakipenda pia. Hivyo watakuwa na msukumo wa kujituma zaidi.

Lakini kama hupendi kile unachofanya, unafanya kwa mazoea tu, hivyo ndivyo wengine watakavyofanya pia na muda siyo mrefu utakuwa na watu ambao hawana hamasa ya kufanya kazi zao na hivyo hakuna kikubwa kinachofanyika.

Penda sana kile unachofanya na utaweza kuwavutia wengine kwa hamasa uliyonayo na wao kuwa na hamasa ya kukifanya pia.

Mbili; tumia mtandao ulionao sasa.

Mpaka hapo ulipofika sasa, una mtandao mkubwa sana, sema tu hujaanza kuutumia. Anza kufikiria watu wote ambao umewahi kukutana nao kwenye maisha yako. Kuanzia shule ya msingi, sekondari mpaka chuo. Fikiria watu wote ambao umewahi kukutana nao kwenye jumuia za kijamii kama dini, au watu mnaotokea eneo moja. Fikiria ndugu, jamaa na marafiki ambao umekuwa nao katika kipindi chote cha maisha yako. Pia fikiria mikutano au makongamano mbalimbali ambayo umewahi kuhudhuria na kukutana na watu mbalimbali.

Ukifikiria kwa namba hiyo, utaona jinsi ambavyo una mtandao mkubwa. Na katika watu wote hao ambao umewahi kukutana nao, kuna ambao utakuwa umependa vitu fulani kutoa kwao. Utaona wanaweza kuwa na mchango fulani kwenye biashara yako, na hapo unaweza kuwashawishi wajiunge na wewe.

Na kama wale unaowajua hawawezi, basi unaweza kuwaomba wakupatie aina ya watu unaowatafuta kutoka kwenye mtandao wao.

Katika kutumia mtandao wako kupata watu sahihi, unapaswa kuwa mvumilivu na king’ang’anizi, watu wazuri huwa hawapatikani kwa urahisi, lakini unapojua ni watu wa aina gani unawataka na kujipa muda wa kuwatafuta, lazima utawapata.

Tatu; fanya kazi kwenye lile eneo unalotaka kuwa na biashara yako.

Ipo njia bora sana kwako kuielewa biashara na kupata watu wazuri wa kushirikiana nao kabla hata hujaingia kwenye biashara hiyo. Njia hiyo ni kufanya kazi kwenye lile eneo ambalo unataka kuwa na biashara yako.

Hii ina maanisha kwamba, kabla hujaingia kwenye biashara, angalia biashara nyingine kama hiyo na kisha omba kuajiriwa kwenye biashara ya aina hiyo. Kama unataka kuanzisha mgahawa, omba kwanza kazi kwenye mgahawa mkubwa. Kama unataka kuanzisha shule, ajiriwa kwanza kwenye shule.

Kupata taarifa za ndani kuhusu biashara unayokwenda kufanya ni ngumu kama haupo ndani. Unapoajiriwa kwenye aina ya biashara unayotaka kuanzisha, unajifunza vitu vingi vya ndani kwa ukaribu sana.

Lakini pia inakupa nafasi ya kukutana na watu wazuri unaoweza kushirikiana nao kwenye biashara utakayokwenda kuanzisha. Mfano katika wafanyakazi wenzako utakaokuwa nao, kuna ambao utaona wana vitu vya tofauti na hivyo utakapokwenda kuanzisha biashara yako, unaweza kuwashawishi wakaungana na wewe.

Pia unapata nafasi ya kukutana na watu mbalimbali ambao wanaweza kuja kukusaidia pale utakapoanzisha biashara yako.

Kama huwezi kuajiriwa kwenye aina ya biashara unayotaka kuanzisha, kazana upate nafasi ya kuwa karibu kabisa na aina hiyo ya biashara. Unaweza hata kumwomba mtu mwenye aina hiyo ya biashara awe menta wako na ujifunze kutoka kwake. Hili litakufanya uielewe biashara kwa karibu.

SOMA; Ishi Kwa Tabia Hizi Kumi (10) Kila Siku Ya Maisha Yako Na Utaweza Kupata Mafanikio Makubwa Sana Kwenye Maisha Yako.

Nne; tumia teknolojia.

Tunaishi kwenye zama bora sana, kwa sababu teknolojia imerahisisha sana mawasiliano. Siku za nyuma ulihitaji sana ‘koneksheni’ ya watu ili kuweza kuwafikia watu sahihi. Lakini ujio wa mitandao ya kijamii umerahisisha sana kuweza kuwasiliana na mtu yeyote yule kwenye nafasi yoyote ile.

Lakini pia mtandao wa intaneti na mitandao ya kijamii inatupa nafasi nzuri ya kuweza kuwatafuta watu na kuwachunguza kabla hata hatujakutana nao. Watu wameweka taarifa zao zote kwenye mitandao yao ya kijamii, kuanzia walikosoma, wanakoishi na hata kazi ambazo wamewahi kufanya au wanafanya. Lakini pia maisha yao ya kijamii wanayaweka wazi kupitia mitandao hiyo.

Hivyo unaweza kutumia mtandao wa intaneti kutafuta watu wenye sifa unazozitaka, halafu ukaingia kwenye mitandao yao ya kijamii na kuangalia aina ya vitu wanavyoweka na hapo utajua kama ni watu sahihi kwako au la.

Pia kuna mitandao ya kijamii maalumu kwa kupata watu wa kushirikiana nao au kuwaajiri kwenye kazi au biashara. Mfano wa mitandao hiyo ni LinkedIn ambao unawapa watu nafasi ya kueleza ujuzi wao, uzoefu wao na nafasi ambazo wanzitafuta.

Ukitumia vizuri teknolojia, utaweza kuwapata watu sahihi na hata kuwafuatilia kabla hawajajua kama unawafuatilia.

Tano; usipoteze muda kutengeneza mtandao usio na umuhimu.

Ujio wa mitandao ya kijamii na urahisi wa kutengeneza mtandao umewafanya watu kuhangaika kujiunga na kila mtandao. Watu wanaposikia kuna kundi la aina fulani wanataka wajiunge nalo. Kinachotokea ni mtu kuwa amejiunga kwenye makundi mengi na hakuna cha maana anachokipata kwenye makundi hayo.

Kumbuka lengo lako wewe ni kupata watu sahihi ambao utaweza kushirikiana nao kwenye biashara yako, iwe ni kwa kuwaajiri, kwa kuwa wabia au hata kuwa wateja wa biashara hiyo.

Hivyo chagua sana aina ya mitandao utakayojiunga nayo, aina ya makundi utakayoingia, yawe yale ambayo una nafasi kubwa ya kuwapata watu sahihi. Chagua makundi machache yenye watu wenye sifa unazozitaka na kujiunga na hayo.

Watu wengi huwa wanafikiria ukishakuwa na wafuasi wengi mtandaoni basi umefanikiwa. Mafanikio kwenye mtandao hayatokani na ukubwa wa wafuasi, bali ubora wake. Unaweza kuwa na wafuasi elfu moja, lakini wote hawana manufaa kwako. Lakini ukawa na wafuasi mia moja ambao wanakujua kwa ukaribu, wanajali kile unachofanya na wapo tayari kushirikiana na wewe zaidi.

Unapokazana kutengeneza mtandao wako, usiangalie namba au ukubwa, bali angalia ubora wa wale waliopo kwenye mtandao huo.

Kwa kufanyia kazi mambo haya matano, utajiweka kwenye nafasi nzuri ya kuwavutia watu bora kwako ambao watakuwezesha kuanzisha na kukuza biashara yako. Fanyia kazi mambo haya matano, iwe tayari upo kwenye biashara au ndiyo unapanga kuingia kwenye biashara na kwa hakika utaweza kufanikiwa sana kwenye biashara hiyo.

Usikose makala ya TANO ZA JUMA hili la 43 ambapo nitakushirikisha sheria 10 za kufanikiwa kwenye ujasiriamali. Makala za TANO ZA JUMA kwa sasa zinapatikana kwenye channel ya TELEGRAM inayoitwa TANO ZA MAJUMA YA MWAKA. Ili kupata makala hizi za uchambuzi wa vitabu pamoja na vitabu vyenyewe, karibu ujiunge na channel hii. Maelezo ya kujiunga yako hapo chini, yasome na uchukue hatua.

MUHIMU; Toleo la pili la kitabu cha BIASHARA NDANI YA AJIRA tayari limetoka, kama hujapata nakala yako unajichelewesha na utaikosa zawadi niliyotoa. Hiki ni kitabu ambacho kitakupa mwongozo sahihi wa kuanzisha na kukuza biashara yako ukiwa kwenye ajira. Kupata nakala yako tumia mawasiliano 0678 977 007, zawadi ya punguzo la bei inaelekea ukingoni, chukua hatua leo.

#PATA KITABU NA UCHAMBUZI ZAIDI.

Rafiki yangu mpenda, kama ungependa kupata kitabu tulichochambua kwenye makala hii ya tano za juma, pamoja na kupata uchambuzi wa mafunzo zaidi kutoka kwenye kitabu hiki, karibu ujiunge na channel ya TANO ZA MAJUMA 52 YA MWAKA.

Hii ni channel ambayo ipo kwenye mtandao wa TELEGRAM MESSENGER, ambapo kila juma nakutumia kitabu cha juma, uchambuzi huu na mafunzo ya ziada yote kwa mfumo wa pdf ambapo utaweza kusoma na hata kuhifadhi vizuri kwa matumizi ya baadaye. Pia kwa kujiunga na channel hii, utaweza kupata mafunzo yote ya nyuma na hata ukipoteza mafunzo hayo utaweza kuyapakua tena muda wowote unapoyataka.

Ada ya kujiunga na channel hii ni ndogo mno, ni shilingi elfu moja tu kwa wiki. Au unaweza kuchagua kulipa kwa mwezi (elfu 3) au kwa mwaka (elfu 30). Lakini wiki ya kwanza ni bure na hulipi chochote. Karibu ujiunge leo bure kwa kutuma ujumbe kwa njia ya telegram kwenda namba 0717396253. Ujumbe uwe na maneno TANO ZA MAJUMA YA MWAKA.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu