Karibu rafiki kwenye makala ya ushauri wa changamoto ambapo tunapata nafasi ya kujifunza kupitia changamoto ambayo msomaji mwenzetu anakuwa ameishirikisha.

Kila mmoja wetu kuna changamoto mbalimbali anazopitia, na uzuri ni kwamba hakuna changamoto mpya. Changamoto nyingi ni zile zile ila zinajitokeza kwa namna tofauti.

Kupitia changamoto za wengine, unaweza kujifunza namna bora ya kutatua changamoto zako mwenyewe. Hivyo karibu sana tujifunze.

Kwenye makala hii tunakwenda kupata ushauri wa mfumo bora wa kuajiri utakaokuwezesha kupata wafanyakazi bora na waaminifu. Kabla hatujaingia ndani na kujua hatua za kuchukua, tupate maoni ya msomaji mwenzetu aliyeomba ushauri kwenye hili.

Mimi ni mfanyabiashara, biashara yangu naisimamia mwenyewe napenda sana niwe na msaidizi kwa maana ya kuajiri, changamoto inakuja kwenye uaminifu maana napenda niwe nasafiri maeneo mbalimbali, ili nifungue fursa zingine, ni mfumo gani niutumie wa kuajiri nisaidie Dr. – John M.I.

Kama alivyotueleza msomaji mwenzetu hapo juu, kuna changamoto kubwa kwenye kupata wafanyakazi bora na waaminifu kwenye biashara.

Wakati mtu unaanza biashara, huwa unaamini unaweza kufanya kila kitu peke yako. Na kweli mwanzoni unafanya kila kitu.

Lakini kadiri biashara yako inavyoendelea kukua, unagundua kwamba wewe ndiyo kikwazo kwenye ukuaji wa biashara yako. Unagundua kwamba huwezi kufanya kila kitu mwenyewe, hivyo unahitaji usaidizi katika kuendesha biashara yako ili ikue.

Wengi wanapofika kwenye hatua hii hukimbilia kuajiri kabla hawajaweka mfumo mzuri. Kinachotokea ni wanaajiri watu ambao siyo sahihi na kinachotokea ni biashara kufa badala ya kukua zaidi. Na hapa ndipo wengi hukata tamaa na kuona bora wapambane wenyewe kuliko kuajiri.

Lakini hilo siyo sahihi, ni kweli kupata wafanyakazi bora na waaminifu ni kazi ngumu, lakini inawezekana. Na ukifuata hatua sahihi, basi kazi hii inakuwa rahisi kwako.

Hapa tunakwenda kujifunza hatua sahihi kwako kufuata ili uweze kupata wafanyakazi bora, waaminifu na watakaoiwezesha biashara yako kukua zaidi.

hiring.jpg

Moja; anza kwa kuweka mfumo mzuri kwenye biashara yako.

Unapokuwa unaendesha biashara yako mwenyewe, kila kitu kinakuwa kwenye akili yako, hivyo unaweza kuisimamia vizuri. Sasa ukiajiri kwa mtindo huo, unatafuta matatizo. Hakuna mtu mwingine anayeweza kuielewa biashara yako kama unavyoielewa wewe, au kuwa mwaminifu kama ulivyo wewe.

Hivyo jukumu lako la kwanza kabla hata hujaajiri ni kutengeneza mfumo wa biashara yako. Igawe biashara yako kwenye vitengo mbalimbali ambavyo ni rahisi kufuatilia na kusimamia.

Kwa biashara ndogo, unaweza kuanza na vitengo vichache kama uzalishaji, masoko na mauzo na fedha na mipango. Ukiwa mwenyewe vitu hivyo unaweza kuwa unavifanya kwa pamoja, lakini unapoajiri, lazima ujue mtu unamweka kwenye kitengo gani na unamfuatiliaje.

Kwenye mfumo, hakikisha una njia ya uhakika ya kufuatilia mzunguko wa fedha kwenye biashara yako na hakuna mwanya wowote wa mtu kufanya udanganyifu.

Kitu kimoja unachopaswa kujua ni kwamba, kutokuwepo kwa mfumo au kuwepo kwa mfumo mbovu, kunaweza kuwaharibu wafanyakazi, mwanzo wanakuwa wazuri na waaminifu, ila baadaye wanabadilika, kwa sababu kuna mwanya wa kufanya udanganyifu.

Mfumo unaoweka kwenye biashara yako unapaswa kuondoa kila nafasi ya kufanyika kwa udanganyifu.

MUHIMU; Kutengeneza mfumo ni somo pana na linapatikana kwenye KISIMA CHA MAARIFA, kama ni mwanachama rejea somo hilo hapa;  na  kama siyo mwanachama jiunge ili uweze kupata somo hilo na kuchukua hatua. Kujiunga tuma ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa wasap kwenda namba 0717396253

SOMA; Faida Kumi (10) Za Kujua Kusoma Namba Za Biashara Na Taarifa Tatu Za Kifedha Unazopaswa Kujua Kuzisoma Ili Kufanikiwa.

Mbili; anza na majukumu ya kazi na siyo mfanyakazi.

Kosa jingine ambalo watu wamekuwa wanafanya wakati wa kuajiri ni kuanza kumwajiri mtu kisha kuangalia ni kazi gani anaweza kukusaidia. Hapa ni sawa na kuweka mkokoteni mbele ya farasi na kutegemea auvute.

Unapaswa kuanza na majukumu ya kazi ambayo unahitaji kupata usaidizi. Hapa unaweza kukaa chini na kufanya tathmini, ni majukumu yapi ambayo unataka kuacha kuyafanya, ili uweke muda na nguvu kwenye majukumu yaliyo muhimu zaidi.

Ukishaorodhesha majukumu hayo, hapo sasa ndiyo unaweza kutafuta mtu anayeweza kukusaidia.

Ukianza na majukumu ni rahisi kufanya maamuzi umwajiri mtu gani. Lakini ukianza na mtu, utajikuta unajaribu kumpa kila aina ya majukumu na hawezi.

Tatu; unapoajiri, kuwa na njia ya kumpima mtu.

Upo usemi kwamba kisichopimika huwa hakifanyiki. Hivyo kama huna njia ya kumpima mtu unayemwajiri, hawezi kuwa na msaada kwako na pia hatakuwa mwaminifu.

Kwenye majukumu ya kazi unayompa mtu unayemwajiri, kuwa na njia ya kupima uzalishaji wake na ufanisi wake. Kama umeajiri mtu wa masoko, mpe namba ya wateja anaopasa kuwafikia kila siku, kila wiki na kila mwezi, kisha mpime kwa matokeo anayozalisha. Kadhalika kama umeajiri mtu wa mauzo, mpe kiwango cha mauzo anachopaswa kufanya.

Unapowapa watu namba ya kufanyia kazi, wao wenyewe wanajisukuma kuifikia. Lakini kama hakuna namba, watakachofanya ni kuigiza kazi, utawaona wako bize kweli, lakini hakuna wanachozalisha.

Mwandishi na mkufunzi wa mauzo Grant Cardone anasema aliwahi kumwajiri mtu wa masoko, ila hakuwa amempa namba. Siku moja akamkuta kwa muda mrefu amekaa ofisini, akamuuliza unafanya nini, akamjibu naandaa orodha ya wateja wa kuwapigia simu. Grant akamwambia sijakuajiri kuandaa orodha, bali kupiga simu na kuongea na wateja. Na kuanzia hapo alimpa idadi ya wateja anaopaswa kuwapigia simu kwa siku na mfanyakazi huyo alifanya hivyo.

Nne; anza na tabia kabla ya sifa nyingine.

Bilionea mwekezaji Warren Buffett anasema katika kuajiri huwa anaangalia vitu vitatu; akili, nguvu na uadilifu. Anaendelea kusema kama kigezo cha tatu hakipo, basi huwa haajiri, maana hivyo viwili vya kwanza vitakumaliza. Kuna pointi kubwa sana ya kujifunza hapo kwa Buffett, kama mtu ana nguvu ya kujituma sana kwenye kazi na ana akili na uwezo mkubwa wa kufanya kazi zake, lakini siyo mwadilifu, atakumaliza.

Hivyo tabia ya mtu ni kigezo cha kwanza kuangalia kabla hujaangalia elimu au mengine. Unaweza kumfundisha mtu jinsi ya kufanya kazi unayompa kwenye biashara yako, lakini huwezi kumfundisha mtu tabia, wala kubadili tabia yake.

Hivyo ukishagundua mtu hana tabia ya uaminifu na uadilifu, achana naye mara moja. Usijidanganye kwamba utambadili au kumdhibiti, na wala usiamini pale mtu anapokuambia atabadilika, siyo rahisi kihivyo.

Anza na tabia, kama tabia siyo sahihi, sifa nyingine alizonazo mtu zitakuumiza zaidi.

SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kutengeneza Timu Bora Itakayokuwezesha Kufanikiwa Kwenye Biashara.

Tano; usiamini watu haraka, hasa kwa maneno.

Wakati mtu anakuomba umwajiri, atakuambia maneno ya kila aina. Kama ni wasifu amekutumia basi utakuwa umerembwa kwa maelezo mazuri. Wasifu wa kila mtu unaeleza ni mchapa kazi, mwaminifu na anayeweza kufanya kazi zake bila ya usimamizi wa karibu.

Ni mpaka utakapofanya kazi na mtu ndiyo utajua kwamba alichoeleza ni kweli au siyo kweli.

Hivyo unapotoa nafasi ya kuajiri watu, mwanzoni wape muda wa kuwaangalia. Usikimbilie kuamini yale wanayokuambia, badala yake waangalie kile wanachofanya. Kwenye kuongea kila mtu huwa sahihi, lakini kwenye kufanya, ndiyo utajua kama ni sahihi kweli au siyo.

Kabla hujaingia kwenye makubaliano ya kumwajiri mtu kwa muda mrefu, mpe kipindi cha kumwangalia kwanza kwenye ufanisi wake. Na katika kipindi hicho, usiangalie sana kazi, bali angalia tabia zake. Anajitumaje, ni mwaminifu, anashirikiana na wengine, anatekeleza aliyoahidi, anaweza kuwahi eneo la kazi mwenyewe bila kusukumwa, vipi mahusiano yake binafsi? Vitu hivyo vitakupa mwanga wa kumjua mtu vizuri kabla hujamwajiri kabisa.

Sita; fukuza wale ambao hawafai.

Kosa kubwa ambalo watu wengi wanafanya kwenye kuajiri ni kuajiri haraka na kufukuza taratibu. Yaani mtu anapotafuta mfanyakazi, huwa ni rahisi kuajiri yeyote anayemshawishi, hachukui muda kumjua kwa undani. Pale mfanyakazi huyo anapokuwa mzigo, mtu anakuwa mzito kumfukuza, anaona ampe muda labda atajirekebisha.

Iko hivi rafiki, kwenye biashara unapaswa kuwa taratibu kwenye kuajiri na haraka kwenye kufukuza. Chukua muda kabla hujamwajiri mtu kama tulivyojifunza hapo juu.

Na pale mtu anapokosa zile sifa za msingi ambazo unazisimamia, mwondoe mara moja, usijipe moyo kwamba atabadilika, tabia za watu huwa hazibadiliki kwa haraka.

Mfanyakazi anapokosa uaminifu na kuiba kwenye biashara au kutafuta njia nyingine ya kujinufaisha yeye binafsi na kuiumiza biashara, hapaswi kubaki kwenye biashara, unapaswa umwondoe mara moja. Ukimwacha, siyo tu ataendelea kufanya hayo, bali pia atawaharibu wafanyakazi wengine wazuri ulionao.

Mweleze wazi kila mfanyakazi ni makosa gani akifanya yanampelekea kufukuzwa mara moja bila ya kupewa nafasi ya pili, ili afanye kazi akiwa anaelewa hilo na inapotokea asishangazwe.

Na wewe simamia hilo kama ulivyoeleza, unahitaji kujenga utamaduni mzuri sana kwenye biashara yako, hivyo usivumilie yale ambayo yataharibu utamaduni huo.

SOMA; Tano Za Juma Kutoka Kitabu TRACTION; Get A Grip On Your Business (Maeneo Sita Ya Kuzingatia Ili Kufanikiwa Kwenye Biashara).

Saba; watu wa kuepuka kuajiri kwenye biashara yako.

Mwisho kabisa kuna watu ambao unapaswa kuepuka kuwaajiri kwenye biashara yako, hata kama wana sifa nyingine unazoziangalia. Najua wengi mtaenda kinyume na hili na kujiambia lakini huyu hana shida, ni mpaka pale watakapokuumiza ndiyo utajua kwa nini hukupaswa kuwaajiri.

Epuka kuajiri watu hawa;

  1. Watu ambao mna mahusiano ya kindugu au kirafiki, mtu yeyote ambaye tayari mna mahusiano nje ya biashara yako, usimwajiri.
  2. Mtu ambaye anakuambia hana kazi ya kufanya hivyo msaidie kwa kumpa kazi.
  3. Mtu ambaye anakuambia yuko tayari kufanya kazi yoyote ili tu apate fedha ya kuendesha maisha yake.
  4. Mtu ambaye anakuambia yuko tayari umlipe chochote, ili tu aweze kuendesha maisha yake.
  5. Mtu ambaye amewahi kufanya kazi maeneo mengi, na kila eneo analalamika jinsi ambavyo hakutendewa haki.
  6. Mtu ambaye hawezi kuwahi eneo analopaswa kufika kwa wakati. Mfano umempa muda wa kumfanyia usaili na hakufika kwa wakati, ni tiketi ya kutokumwajiri.
  7. Mtu ambaye siyo mwaminifu kwenye mahusiano yake nje ya biashara. Usidanganyike kwamba hayo ni maisha yake binafsi na hayahusiani na biashara. Kama mtu siyo mwaminifu ni siyo mwaminifu tu, na tabia hiyo itagusa kila eneo la maisha yake.
  8. Mtu ambaye anaamini anajua kila kitu na hayupo tayari kujifunza. Kama mtu siyo msomaji wa vitabu au kutumia njia nyingine za kujifunza kuwa makini naye.
  9. Mtu ambaye ana vipaumbele vingine anavyovipa uzito kuliko kazi unayompa. Mfano anakuambia hawezi kukosa mechi ya timu fulani inapocheza.
  10. Kama biashara yako ni changa, epuka kuajiri mtu ambaye ana uzoefu kutoka kwenye biashara kubwa. Hawa huja na utamaduni mbovu na kuamini wanajua kuliko wewe, hivyo watakusumbua. Kama unaanzia chini, anza na wafanyakazi ambao hawana uzoefu na kisha wafundishe mfumo wako na jenga utamaduni wako.

Fanyia kazi haya na utaweza kuajiri wafanyakazi bora na waaminifu na watakaoiwezesha biashara yako kukua zaidi.

Kama upo kwenye biashara, kuna kitu muhimu sana unapaswa kukijua ambacho ni jinsi ya kutengeneza MFUMO WA KUENDESHA BIASHARA KWA MAFANIKIO. Kwenye KISIMA CHA MAARIFA kuna mafunzo kamili ya mfumo, ambayo yanakupitisha kila hatua na pia yamefundisha kwa kina eneo la uajiri. Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, jiunge sasa ili upate mafunzo hayo na pia utakapohitaji ushauri na usimamizi wa karibu kutoka kwa kocha, utaupata ukiwa kwenye KISIMA CHA MAARIFA. Tuma ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa wasap kwenda namba 0717396253 kisha utapewa maelekezo. Karibu sana.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania