Alpheus Bingham ni mkemia mbobezi ambaye mwaka 2001 alikuwa akifanya kazi na taasisi ya utafiti na madawa inayoitwa Eli Lilly. Akiwa kwenye taasisi hiyo, aligundua kwamba wanasayansi na wakemia wa taasisi hiyo walikuwa na maswali magumu ya kisayansi na kikemia ambayo yalikuwa yamewashinda wao licha ya ubobezi wake.

Kupitia uzoefu wake binafsi, Bingham alikuwa anajua kwamba ni rahisi kupata ufumbuzi wa changamoto kwa mtu wa nje kuliko mtu aliyebobea. Hivyo alikusanya maswali magumu 21 ambayo yalikuwa yameshindikana na kuuaweka kwenye tovuti ili kila mtu aweze kuyaona na kujaribu kuyatatua.

Wanasayansi na wakemia wa taasisi hiyo ya Eli Lilly hawakufurahishwa na hilo, waliona ni kutoa siri za ugunduzi wao. Lakini pia walihoji kama wao wabobezi wameshindwa, nani mwingine atakayeweza? Bingham aliomba mpango wake huo upewe majaribio kwa muda na kama hautakuwa na matokeo mazuri basi unaweza kuondolewa.

specialists vs generalist.jpg

Haikuchukua muda mrefu, theluthi moja ya maswali hayo magumu ilikuwa imepata majawabu rahisi na yanayofanya kazi. Lakini cha kushangaza zaidi ni kwamba, majibu rahisi na yanayofanya kazi yalikuwa yanatoka kwa watu ambao hawakuwa hata wanasayansi au wakemia. Yalitoka kwa wetu wenye taaluma mbalimbali, kama sheria, uchumi na kadhalika.

Kupitia mafanikio ya jaribio hilo, Bingham alianzisha taasisi INNOCENTIVE ambayo inatoa nafasi ya watu kuweka wazi changamoto na maswali magumu yaliyoshindikana na kupata mawazo kwa watu wengine. Na taasisi hiyo imekuwa na mafanikio makubwa sana, kwani matatizo mengi yamepaya suluhisho, na mara zote suluhisho limekuwa linatoka kwa watu ambao hawajabobea kwenye kitu hicho.

Tafiti nyingi zimekuwa zinaonesha kwamba, kadiri watu wanavyobobea kwenye kitu, ndivyo inavyokuwa vigumu kwao kuona suluhisho rahisi kwa changamoto ngumu. Hata kwenye utabiri wa matokeo ya baadaye, wale waliobobea sana kwenye kile wanachotabiri, huwa wanapata matokeo mabovu kuliko ambao hawajabobea.

SOMA; Hatua Sita (06) Za Kutengeneza Ubobezi Kwenye Kile Unachopenda, Kutoa Thamani Zaidi Na Kuongeza Kipato Chako.

MAKUNDI MAWILI YA WATU KATIKA UTATUZI WA MATATIZO.

Inapokuja kwenye utatuzi wa matatizo, watu wanaweza kugawanywa kwenye makundi mawili makubwa.

Kundi la kwanza ni NDEGE.

Hawa ni wale watu ambao wanaona vitu vingi lakini wanaviona kwa umbali. Kama ambavyo ndege anapaa angani, anaweza kuona eneo kubwa sana anapokuwa angani, lakini hawezi kuona vitu vidogo vidogo vilivyopo chini. Anaweza kuuona msitu akiwa juu, lakini hawezi kuona mti mmoja mmoja.

Ndege hawa ni wale watu ambao wana uelewa mdogo kwenye vitu vingi. Hawa wanakuwa wanajua vitu vingi, lakini hawavijui kwa undani sana.

Watu hawa ni wazuri sana kwenye utatuzi wa changamoto mbalimbali kwa sababu wanaweza kuhamisha uzoefu wa eneo moja na kupeleka kwenye eneo jingine.

Watu hawa wanafanya vizuri pale wanapokuwa wanafanya kitu kisichokuwa na uhakika, yaani kile ambacho matokeo yake hayajulikani. Kwa ujuzi wao kwenye mambo mengi, inakuwa rahisi kwao kutumia maeneo hayo kuja na majibu.

Ndege ni sifa nzuri ya viongozi, kwa sababu hawa wanawaongoza watu kufanya vitu ambavyo ni vikubwa na hawajazoea, wanapaswa kuwa na uelewa mkubwa wa maeneo mengi ili kuweza kutoa mwongozo sahihi.

Kundi la pili ni VYURA.

Hawa ni wale watu ambao wana uelewa mkubwa sana kwenye kitu kimoja, lakini vitu vingine hawavijui. Hawa ni wale ambao wamebobea kwenye eneo moja kiasi kwamba wanalijua vizuri na hakuna kinachowashinda.

Kama ilivyo kwa mnyama chura, huwa anayaona mazingira yake vizuri, na kuyaelewa kwa undani ukilinganisha na ndege anayeruka juu. Chura hawezi kuuona msitu mzima, ila anaweza kuuona mti kwa ukaribu na kuelewa sifa zake zote.

Watu wenye sifa ya vyura ni wazuri sana kwenye kazi ambazo zina uhakika wa matokeo na hivyo uelewa wao mkubwa unawapa manufaa ya kufanya vizuri. Hii ni sifa nzuri sana kwa wale ambao ni mameneja, ambao tayari wanajua matokeo wanayoyataka hivyo kazi ni kuyafikia. Kadiri wanavyolielewa eneo lao, ndivyo wanavyozalisha matokeo bora zaidi.

SOMA; Hivi Ndivyo Kifafa Cha Ujasiriamali Kinavyowatesa Wale Wanaotoka Kwenye Ajira Na Kwenda Kujiajiri.

Makundi yote mawili ni muhimu na yanahitaji kushirikiana ili kupiga hatua. Hakuna kundi moja ambalo ni bora zaidi ya mwenzake, tunahitaji ndege ambao wataongoza mwendo na tunahitaji vyura ambao watahakikisha yale muhimu yanazingatiwa.

Tunaishi kwenye dunia ambayo inaonekana ubobezi kwenye kitu kimoja ndiyo njia bora ya kufanikiwa kwenye kile ambacho mtu anafanya. Japo kuna wachache waliofanikiwa kwa njia hiyo, lakini tafiti nyingi zinaonesha kwamba wanaofanikiwa zaidi ni wale ambao hawabobei kwenye kitu kimoja, bali wanakuwa na uelewa kwenye mambo mengi.

Mwandishi David Epstein kwenye kitabu chake kinachoitwa Range : why generalists triumph in a specialized world, ametushirikisha kwa kina jinsi ambavyo kutokubobea kwenye jambo moja kuna manufaa makubwa. Kupitia mifano na tafiti mbalimbali, kuanzia kwenye michezo, sayansi na hata biashara, iko wazi kwamba wale wanaofanikiwa zaidi ni wale wenye uelewa mpana wa mambo mengi na siyo uelewa wa kina wa jambo moja.

JINSI YA KUTUMIA UELEWA MPANA KUFANIKIWA KWENYE BIASHARA.

Kosa moja ambalo watu wengi wamekuwa wanafanya wanapoingia kwenye biashara ni kwenda kufanya kile ambacho wamebobea. Labda mtu ni mwalimu mzuri basi anakwenda kuanzisha shule yale, na yeye ndiye anayefundisha. Au mtu ni daktari bingwa, anakwenda kuanzisha hospitali yake na yeye ndiye anayetibu.

Kwa njia hii wengi wamekuwa wanakwama kukuza biashara zao, kwa sababu hawaoni mbali. Wanachoona ni kile wanachofanya kila siku, ambacho kinawachosha sana. Hilo haliwapi nafasi ya kuziona fursa za kukuza zaidi biashara zao.

Njia bora ya kufanikiwa kwenye biashara ni wewe kuchagua kuwa NDEGE, lakini kuajiri VYURA.

Hapa wewe mmiliki wa biashara hubobei kwenye jambo moja, bali unakuwa na uelewa mpana wa maeneo mengi. Lakini wale unaowaajiri kufanya kazi kwenye biashara yako, unachokua waliobobea.

Mfano wewe mmiliki wa biashara unapaswa kuwa na uelewa mpana wa uzalishaji, masoko, mauzo, huduma kwa wateja, rasilimali watu, mzunguko wa fedha na mengine muhimu ya biashara. Lakini unapoajiri mtu wa masoko, unachagua yule ambaye amebobea kwenye eneo la masoko ili aweze kuleta matokeo bora kwenye biashara yako.

Kwa njia hii, wewe utaweza kuweka nguvu kwenye kuikuza zaidi biashara yako na wale wabobezi unaowaajiri wanazalisha matokeo bora sana.

Hendry Ford ni mmoja wa watu walioleta mapinduzi makubwa duniani, kwa kuzalisha magari kwa bei rahisi ambayo kila mtu aliweza kumudu. Lakini hakuwa na elimu kubwa, hakumaliza hata shule ya msingi. Katika kupishana kauli, ripota mmoja wa chombo cha habari alisema Ford  ni mjinga na asiye na uelewa. Jambo hilo lilifika mahakamani na katika kujitetea ripota yule alimuuliza Ford maswali mbalimbali kuhusu historia na mengine ambayo Ford hakuweza kuyajibu. Mwisho akamwambia hakimu unaona mwenyewe, hawezi kujibu maswali hayo. Ford akasema, nina haja gani ya kukariri majibu ya mambo yote hayo wakati ninaweza kuajiri mtu atakayenipa majibu ya kitu chochote ninachotaka kujua kwa muda wowote?

Hicho ndiyo kitu ambacho unapaswa kukifiria mara zote unapokuza biashara yako, kwamba huhitaji kujua vile vitu vya ndani kabisa, hivyo ajiri watu wafanyie kazi. Wewe jua yale ya juu na muhimu kwa uendeshaji na ukuaji wa biashara yako na hilo litakupa nafasi ya kuziona fursa nyingi za ukuaji zaidi.

SOMA; Tano Za Juma Kutoka Kitabu; THE E-MYTH REVISITED, (Kwa Nini Biashara Nyingi Zinashindwa Na Hatua Za Kuchukua Ili Biashara Yako Isishindwe).

VIPI KAMA WEWE TAYARI NI CHURA?

Najua kuna watu ambao tayari wameshaingia kwenye biashara zinazohusu kile walichobobea, walimu walioanzisha biashara, madaktari walioanzisha hospitali, wahasibu walioanzisha biashara za ukaguzi wa mahesabu au wanasheria ambao wameanzisha biashara inayotoa huduma za kisheria.

Kama upo kwenye kundi hili hujapotea, bali unapaswa kubadili mpango na namna unavyoichukulia biashara hiyo.

Acha kuwa mtendaji mkuu wa kile kinachofanyika kwenye biashara na kuwa mtendaji mkuu wa biashara nzima. Acha kufanyia kazi lile eneo ulilobobea na bobea kwenye biashara nzima. Unapotaka kupata ubobezi wa ndani zaidi, ajiri wale wenye ubobezi huo. Lakini kataa kabisa wewe kuwa ndiyo mbobezi tegemezi kwenye shughuli kuu inayofanyika kwenye biashara.

Unaweza kufanya shughuli hiyo kama ni kitu unachopenda, lakini kumbuka upo kwenye biashara, na jukumu kubwa la kwanza kwako kama mfanya biashara ni kukuza biashara yako. Na hutaweza kuikuza kama muda wote upo ‘bize’ kutekeleza majukumu ya kila siku ya biashara husika.

Chagua kuwa ndege na kazana kutafuta vyura ambao utawaajiri kwenye biashara yako ili iweze kukua zaidi.

Kwenye makala ya TANO ZA JUMA hili la 36 tutakwenda kujifunza kwa kina njia bora ya kufanikiwa bila ya kupitia ubobezi wa eneo moja kutoka kitabu kinachoitwa Range : why generalists triumph in a specialized world kilichoandikwa na David Epstein. Usikose makala hiyo kwa sababu inakwenda kufungua ulimwengu mpya kwako, ambao utakuwezesha kufanya makubwa bila ya kuzama kwenye eneo moja kwa kina.

Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha