Kuna watu hata mambo yawe magumu kiasi gani, kwa upande wao fursa ni nyingi kuliko wanavyoweza kuzifanyia kazi.
Hata pale ambapo kila mtu analalamika, wao wanakuwa wapo bize kuchukua hatua kama vile hakuna kinachoendelea zaidi.
Kwa nje ni rahisi kuona watu hao wana bahati au wanapendelewa, lakini unapochunguza kwa ndani, unagundua picha ni tofauti kabisa.
Ukiwaangalia watu hao, inaonekana kuna namna ambavyo wanazikaribisha fursa zaidi kwenda kwao, hata kama mambo ni magumu kiasi gani.

Kama na wewe unapenda kuwa mtu wa kuzivutia fursa zaidi zije kwako, kama unataka hata mambo yakiwa magumu kiasi gani uwe kwenye upande mzuri, yapo mambo ambayo ukiyafanya yatakufanya uwe wa tofauti kabisa.
Popote unapopata nafasi ya kufanya kitu, kifanye kwa ubora wa hali ya juu sana. unapopata nafasi ya kufanya kazi, fanya kazi ambayo ni bora kabisa, kazi ya kipekee ambayo watu hawajawahi kuiona.
SOMA; UKURASA WA 1001; Utakutana Na Bahati…
Unapoahidi kitu, kitekeleze kama ulivyoahidi. Hata kama unasukumwa kiasi gani kutoa sababu za kutokutekeleza usifanye hivyo, badala yake tekeleza. Wala usitake watu wajue umepata shida kwenye kutekeleza, wewe tekeleza na watu wataamini neno lako.
Unapokuwa kwenye mawasiliano na mazungumzo na mtu yeyote, jifunze kusikiliza kwa umakini, sikiliza vizuri, sikia kinachoongelewa na pia ona kinachofanyika. Kusikiliza kwa makini kutakuwezesha kusikia kile ambacho wengi hawasikii.
Unapopata nafasi ya kutoa, toa kadiri uwezavyo na toa kwa moyo mmoja. Toa kwa sababu unatoa na siyo kwa sababu unategemea kupata. Toa hata kama huna uhakika wa utapataje kile ambacho umetoa.
Popote unapokuwa, kuwa mtu wa hamasa, kuwa mtu wa kuwafanya wengine waone tumaini, kuwa mtu wa kuwapa wengine sababu ya kupiga hatua.
Fanya mambo hayo kila wakati, kila siku na mara kwa mara kila unapopata nafasi ya kufanya. Na kwa hakika, kila wakati utakuwa na fursa nyingi kuliko unavyoweza kuzitumia.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog