“Whenever you are angry, be assured that it is not only a present evil, but that you have increased a habit” – Epictetus
Habari za asubuhi mwanamafanikio?
Hongera kwa nafasi hii nyingine nzuri sana ya leo, nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuishi kwa msingi wa mafanikio ambao ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wetu wa mwaka huu 2018 ambao ni TATUA, AMUA NA ONGOZA.
Msingi na mwongozo tunaoishi utatuwezesha kufanya makubwa sana leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari KINACHOKUKASIRISHA SIYO KILICHOTOKEA…
Kuna mambo huwa yanatokea kwenye maisha yako, ambayo yanakufanya upate hasira, kwa nini yametokea au kwa nini mtu amekufanyia hivyo.
Ni rahisi kuona kwamba mambo hayo yanakukasirisha, lakini ukweli ni kwamba, kinachokukasirisha siyo kilichotokea.
Kwa sehemu kubwa, kinachokukasirisha ni wewe mwenyewe, kwa kujijaza mambo ambayo hayapo kabisa kwenye kile kilichotokea.
Unaongeza chumvi, unazidisha uhalisia wa mambo, unajikumbusha mambo ambayo yalishapita huko nyuma, halafu unajaa hasira.
Kwa mfano kama mtu amekujibu vibaya, ukapata hasira, kilichokukasirisha siyo mtu kukujibu vibaya. Bali utakiwa umeongeza chumvi na kujikumbusha ya nyuma. Utakuwa umejiambia kwa nini anijibu hivyo mimi, ana dharau, alishafanya tena hivi, na kadhalika, mambo ambayo ndiyo yanakujaza hasira, na siyo kilichotokea.
Kupata hasira hakuna tofauti na kujaza puto upepo, kadiri upepo zaidi unavyoingia ndivyo linavyozidi kubwa kubwa.
Kadhalika kadiri unavyojikumbusha mambo ya nyuma, kadiri unavyoongeza chumvi kwenye kile kilichotokea, ndivyo unavyozidi kupata hasira.
Dawa ya kujiepusha na hasira ni kuangalia kilichotokea kwa uhalisia wake, acha kuongeza chumvi, acha kujikumbusha ya nyuma. Usijijaze upepo kwa namna yoyote ile, na utajiepusha na hasira zisizo za msingi.
Ukawe na siku bora kabisa ya leo, siku isiyo ya kujijaza upepo wa hasira.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha