Kwa kuwa kwenye mazingira ya aina moja, kuna watu waliofanikiwa na walioshindwa, kinachowatofautisha watu hao hakiwezi kuwa mazingira, bali kile ambacho kipo ndani ya watu hao.

Na katika vitu ambavyo vipo ndani ya watu, kimoja muhimu ni kile ambacho wanajua.

Kuna vitu ambavyo waliofanikiwa wanajua lakini wale ambao hawajafanikiwa hawavijui. Na wale wanaojua hawajui kama ni vitu vya tofauti, au ndiyo vinawafanya wafanikiwe, wanaona ni sehemu ya maisha yao.

Vipo vingi ambavyo waliofanikiwa wanajua wakati wasiofanikiwa hawajui, lakini leo napenda tujikumbushe vitu hivi vitatu ambavyo kila mmoja wetu anapaswa kuvijua kuhusu mafanikio.

Moja; unapaswa kujua ya kwamba hujui kila kitu, huu ni msingi wa kwanza na wa muhimu sana katika kujifunza na kufanikiwa. Ukiwaangalia wale waliofanikiwa, kila wakati kuna kitu wanajifunza, na kwenye kila hali, huwa wanatafuta cha kujifunza. Lakini upande wa pili kwa wasiofanikiwa kuna shida kubwa, waambie wajifunze na watakuambia wanajua kila kitu. Waambie wasome vitabu na watakuambia vitabu havina maana. Na wataendelea na maisha yao magumu huku wakiamini kujua kila kitu.

SOMA; UKURASA WA 596; Njia Bora Kabisa Ya Kujifunza Kitu…

Mbili; jua hata kama mambo yanaonekana mazuri kiasi gani, kunaweza kuwa na mtego au anguko mbele yako. Hivyo hii inakufanya uwe makini kwa kila hatua unayochukua, unahitaji kuweka nafasi za kuanguka na kushindwa na hivyo kuwa na mpango mbadala ni muhimu. Wanaoshindwa huwa wanataka kila kitu kiende kama wanavyotaka wao, na kinapokwenda tofauti, wanakuwa hawajajiandaa na hivyo kupoteza.

Tatu; jua kwamba huhitaji kufanya kila kitu peke yako, jua wakati wa kuhitaji msaada wa wengine. Wanaofanikiwa wanajua kuwatumia wengine vizuri na hawapati shida kwenye kuomba msaada. Ila wanaoshindwa, wanataka kufanya kila kitu wao wenyewe, na kuomba msaada wanaona kama ni kujidhalilisha.

Hivi ni vitu vitatu, ambavyo ni muhimu sana tukajikumbusha kwa sababu vinasahaulika haraka na kwa mazoea vimekuwa vinafanyika kwa upande wa kushindwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog