When I think over what I have said, I envy dumb people – Lucius Annaeus Seneca
Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari UKITAFAKARI KILA UNACHOSEMA…
Kuongea ni rahisi, na kila mtu anapenda kuongea.
Iwe ni kujieleza, kujitetea au hata kuwashauri wengine, tunapenda sana kuongea.
Lakini kama utapata muda wa kutafakari kila unachoongea, utawaonea wivu watu ambao ni mabubu.
Kwa sababu utagundua sehemu kubwa ya yale uliyoongea siyo muhimu.
Wakati mwingine siyo kweli halisi,
Na wakati mwingine watu wanakuwa wamekuelewa vibaya na ulivyomaanisha.
Ukifanya zoezi hili la kutafakari kila baada ya kuongea, utaona jinsi ambavyo mengi unayoongea wala hayahitajiki.
Na dunia ingeweza kwenda vizuri tu bila hata ya wewe kuweka neno lolote.
Sasa baada ya kutafakari kila baada ya kuongea na kuona mengi unayosema hayahitajiki, hamishia zoezi hilo kwenda kabla ya kuongea.
Jipe muda wa kutafakari kila neno kabla hunalitoa, na uone kama kweli ni muhimu na linahitajika.
Hii itakuepusha na matatizo mengi ambayo yanayokana na yale unayosema.
Na kama huna muda wa kutafakari kabla hujaongea, basi ni bora usiongee kabisa.
Siyo kwamba dunia itasimama kwa sababu wewe hujaongea, au hujatoa maoni yako.
Na hakuna mtu amewahi kugombana na mtu kwa sababu hajaongea, au kufungwa kwa sababu hajaongea. Ila kila mara kuna ugomvi baina ya watu kwa sababu ya maneno ambayo mtu alisema.
Tafakati kila neno kabla hujalitoa kwenye kinywa chako, maana likishakuponyoka, huna tena mamlaka juu ya neno hilo. Watu watalichukua kama wanavyotaka kulichukua, na hawatajisumbua kwamba ulikuwa unamaanisha nini. Litamaanisha kile wanachotaka kuamini wao.
Ukawe na siku bora leo, siku ya kutafakari kabla ya kutoa neno lolote kwenye kinywa chako.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha