“He is a wise man who does not grieve for the things which he has not, but rejoices for those which he has” – Epictetus
Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari USISIKITIKE KWA ULIVYOKOSA, FURAHIA ULIVYONAVYO…
Huwa tunafikiri kwamba, tukishakuwa na kila tunachotaka, basi ndiyo tutakuwa na furaha.
Na hivyo tunapofikiria yale tuliyokosa, tunasikitika na kuona kama maisha yetu hayajakamilika.
Ukweli ni kwamba, hakuna yeyote anayeweza kupata kila anachotaka.
Hata upate kila unachotafuta, kuna vitu ambavyo utavikosa,
Hivyo ndivyo maisha yalivyo.
Hivyo, badala ya kufikiria sana na kusikitika kwa vile ulivyokosa, ni bora kufikiria zaidi na kufurahia vile ambavyo tayari unavyo.
Kwa kufikiria vile ulivyonavyo, unakuwa kwenye upande mzuri wa kuyaona maisha ni bora.
Lakini pale unapofikiria kila ulichokosa, ndipo unaona maisha hayafai na siyo mazuri.
Kumbuka kila mtu kuna kitu anakosa kwenye maisha, na lengo la maisha siyo kuweka pata kwamba umepata kila kitu, kama vile unafanya mtihani.
Bali lengo la maisha ni kuyaishi, kwa kila wakati unaoupata.
Hivyo hapo ulipo sasa, fikiria zaidi na furahia kila ulichonacho, maana kesho unaweza usiwe na hivyo ulivyonavyo leo.
Na kwa vile uliyokosa, visiwe ndiyo sababu ya kuona maisha yako hayafai, bali endelea kufanyia kazi kupata vile muhimu, na visivyo muhimu visikusumbue.
Uwe na siku bora sana leo, siku ya kufurahia kila ulichonacho leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha