Hongera sana rafiki yangu kwa kulimaliza juma namba 17 la mwaka huu 2018 na kulianza juma namba 18.

Juma moja, yaani siku saba, masaa 168 ndiyo kipimo kizuri sana cha muda unachoweza kutumia. Hii ni kwa sababu ni rahisi kupangilia na kufuatilia siku saba na pia kuchukua hatua haraka pale mambo yanapokwenda tofauti.

Nimekuwa nakushauri sana na kukusisitiza kwamba kila mwisho wa wiki kaa chini na itafakari wiki yako, kisha pangilia wiki inayofuata. Wiki ikiisha tena angalia umefanyiaje kazi mipango yako, wapi umefanikiwa na wapi hukufanikiwa, kisha wiki inayofuata weka mipango bora zaidi ili kuweza kupiga hatua.

095a5b996f7db11bfe3b1d93a17b444b.0

Karibu kwenye #TANO ZA JUMA, mkusanyiko wa mambo matano muhimu niliyojifunza na kukutana nayo ambayo yanaweza kukusaidia wewe kuwa bora zaidi na kuweza kufanya maamuzi sahihi.

#1 KITABU NILICHOSOMA; KAMA HASARA HAIKUGUSI, HUPASWI KUNUFAIKA NA FAIDA.

Wale wanaosema dunia haipo sawa, hasa pale wanapoweka juhudi fulani na kupata matokeo ambayo siyo waliyotegemea, hawakosei, ila tu hawajui kwa undani ile hali ya kutokuwa na usawa kwenye dunia.

Kuna watu, kwa makusudi kabisa, wanatengeneza hali isiyo ya usawa hapa duniani. Watu hao, ikipatikana faida basi wananufaika, lakini ikipatikana hasara basi wao haiwagusi.

Yaani ni sawa na wewe ufanye biashara na mtu, biashara ya kushirikiana ambapo mmeweka mtaji sawa, na wote mnaweka juhudi kwenye biashara hiyo. sasa ikipatikana faida, mnagawana nusu kwa nusu, lakini ikipatikana hasara, unaibeba wewe tu, mwenzako haimgusi.

Mwandishi Nassim Nicholas Taleb, anatufunulia aina hii ya kukosekana kwa usawa kwenye maisha ya kila siku kwenye kitabu chake cha SKIN IN THE GAME. Taleb anaonesha kwenye kila eneo la maisha yetu, kuanzia siasa, kazi, biashara na hata dini, jinsi ambavyo wapo watu wanaonufaika kwa faida lakini hasara haiwagusi.

Kwa mfano, nchi moja inapopigana vita na nchi nyingine, wanaoanzisha vita huwa ni viongozi wa nchi, lakini hata siku moja viongozi hao hawaumii, bali wanaoumia ni wananchi, ambao hata hawajui maana halisi ya vita hiyo ni nini. Taleb anasema ingependeza sana kama nchi zinapoamua kuingia kwenye vita, basi viongozi wanaoamua pamoja na familia zao wawe mstari wa mbele kwenye kupigana vita.

Lakini hilo halitokei, na viongozi hao watajisifia kama watashinda vita na hata wakishindwa, hasara haiwaumizi.

Taleb anasema wale waliowekeza kitu kwenye kile wanachofanya, kiasi kwamba hasara ikitokea basi wanaumia, hao wana SKIN IN THE GAME. Lakini wale ambao hawajawekeza chochote, wananufaika tu na faida, lakini hasara haiwagusi, hawana SKIN IN THE GAME.

Kama unataka kufanikiwa kwenye maisha, kwenye chochote unachofanya, wekeza kwa kiasi kwamba hasara ikitokea inakugusa na unaumia hasa. Uwekezaji wa aina hiyo utakufanya uchukue hatua na hata wengine wakuamini.

Taleb anasema usichukue ushauri kwa mtu ambaye matokeo ya ushauri huo hayatamgusa.

Na mwisho kabisa, Taleb anasema vijana wengi wamekuwa wanamwomba ushauri wafanye nini, kwamba wanataka kuiokoa dunia, na Taleb anasema njia pekee ya kuiokoa dunia ni kuwa mjasiriamali na kuanzisha biashara. Unapoingia kwenye biashara unakuwa kweli umeweka SKIN IN THE GAME, na juhudi zako ndiyo zitakupa mafanikio na kuwasaidia wengine pia.

Chochote unachofanya kwenye maisha yako, kazi, biashara, mahusiano, imani na mengineyo, unahitaji kuwekeza kila ulichonacho kiasi kwamba ukifanya makosa unapoteza kila kitu. Na kama upo kwenye mahusiano au ushirikiano ambapo mwingine ananufaika na faida ila hasara haimgusi, ondoka haraka.

#2 MAKALA YA WIKI; SHERIA TATU ZA MAFANIKIO KWENYE UJASIRIAMALI.

Mafanikio kwenye jambo lolote ni kitu kinachotengenezwa. Siyo bahati au ajali, bali ni matokeo yanayotengenezwa kwa juhudi fulani ambazo mtu anakuwa ameweka.

Watu wengi huwa hawapendi sheria, huwa wanapenda kujiendea kama wanavyotaka wao wenyewe, lakini mafanikio yoyote ni matokeo ya kufuata sheria na taratibu fulani.

Kwenye makala ya wiki tunajifunza sheria tatu muhimu za kuzingatia ili kufanikiwa kwenye ujasiriamali. Kama hukupata nafasi ya kusoma makala hiyo, unaweza kuisoma hapa; Sheria Tatu Za Kimafanikio Ambazo Kila Mjasiriamali Anatakiwa Kuzijua. (https://amkamtanzania.com/2018/04/24/sheria-tatu-za-kimafanikio-ambazo-kila-mjasiriamali-anatakiwa-kuzijua/)

#3 NILICHOJIFUNZA; WHATEVER IT TAKES (HUJAWA TAYARI KUFANYA KINACHOHITAJIKA KUFANYWA).

Kupanga ni rahisi, kila mtu anaweza kupanga na wengi huwa wanapanga. Tatizo linakuja pale mtu anapochukua hatua kutekeleza yale aliyopanga, hatua ya kwanza kabisa ni kukutana na vikwazo ambavyo vinapima kama mtu amejitoa kweli, kama kweli mtu ana SKIN IN THE GAME.

Wengi huishia hapo kwenye vikwazo vya mwanzo, na huwa ndiyo mwisho wa safari yao ya mafanikio. Na watakuambia nimejaribu sana lakini nimeshindwa.

Nimekuwa nawasikiliza watu ambao wanasema biashara ni changamoto kwao. Mtu anakuambia nimefanya biashara nyingi lakini nimeshindwa. Ukimuuliza biashara ngapi anakuambia tano, ukimuuliza kila biashara ulifanya kwa muda gani utakuta ni chache ambazo zilivuka mwaka mmoja. Hapo ndipo unagundua kwamba watu hawajui nini hasa kinahitajika kupata kile unachotaka.

Wenzetu wana msemo WHATEVER IT TAKES, ukimaanisha chochote utakachohitajika kufanya, yaani kwenye safari ya mafanikio, siyo tu utahitaji kufanya yale uliyopanga, bali utahitaji kufanya chochote unachohitajika kufanya ili kufika pale unapotaka kufika.

Utasikia watu wanasema unahitaji kufanya kile unachopenda, lakini hilo halimaanishi kila wakati utakuwa unapenda unachofanya, kuna wakati utahitajika kufanya vitu ambavyo hupendi kabisa, ili tu uweze kufika kwenye kile unachopenda kufanya.

Hivyo rafiki, unapoweka mipango yoyote, malizia kwa kujiambia kwamba NITAFANYA KILA NINACHOHITAJIKA KUFANYA MPAKA NIPATE HICHI NINACHOTAKA. Ila tu chochote unachopaswa kufanya, kiwe sahihi.

#4 HUDUMA NINAZOTOA; NAFASI ZA COACHING KWA MWEZI WA TANO.

Zipo nafasi chache za COACHING kwa mwezi may 2018. Kama una kitu ambacho kimekuwa kinakusumbua kufanya wewe mwenyewe, umekuwa unakosa nidhamu ya kujisimamia kufanya, au umekuwa unapanga kufanya lakini unaahirisha, basi nina huduma nzuri sana kwako.

Kila mwezi huwa nafanya kazi moja kwa moja na watu wachache, kuwasaidia kupiga hatua kwenye yale ambayo wanataka kufanya ila wanakwama.

Kwa mwezi huu wa tano tunaokwenda kuanza, nakukaribisha kwenye huduma hii.

Karibu tufanye kazi pamoja, uweze kutengeneza SKIN IN THE GAME na kufanya WHATEVER IT TAKES ili uweze kupata kile unachotaka au kufika pale unapotaka kufika.

Ni program ya mwezi mmoja ambayo ina ada ya kulipa ili kushiriki. Kupata huduma hii tuma neno COACHING PROGRAM kwa wasap namba 0717396253 kisha nitakupa maelekezo zaidi, baada ya kujua kama una kitu kinachoweza kunufaika na program hii.

Karibu sana, tuma ujumbe sasa, kwa wasap 0717396253.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; KITU PEKEE CHA THAMANI UNACHOMILIKI.

Our mind is the most valuable possession that we have. The quality of our lives is, and will be, a reflection of how well we develop, train, and utilize this precious gift. – Brian Tracy

Huwa tunakimbizana na fedha na mali, tukiamini tukishapata hivyo basi maisha yetu yatakuwa tulivu. Lakini kama hatujaweka sawa kitu pekee cha thamani ambacho tunacho, chochote tutakachopata hakitakuwa na manufaa kwetu. Ndiyo maana wengi wanapata mali na zinapotea zote.

Kama Brian Tracy anavyotuambia, kitu pekee cha thamani unachomiliki ni akili yako. Ubora wa maisha yako ni matokeo ya jinsi unavyoendeleza akili yako, na kuitumia vizuri.

Hivyo rafiki yangu, jukumu lako la kwanza ni kunoa akili yako, uwekezaji muhimu kufanya ni kuwekeza ndani yako, kujifunza na kuwa bora zaidi. Akili ikiwa vizuri, utaweza kupata chochote kile unachotaka kupata.

Hakikisha unatumia vizuri rasilimali hii ya kipekee iliyopo ndani yako.

Uwe na juma bora sana rafiki, tumia kila dakika yako kwa ukamilifu, ukijua ni nini hasa unachotaka na nini unapaswa kufanya, huku ukiwa tayari kufanya chochote unachohitajika kufanya.

Maneno ya kwenda nayo na kujikumbusha wiki hii; #SkinInTheGame na #WhateverItTakes

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Rafiki, kama ungependa kujifunza zaidi kupitia mafunzo ninayotoa, karibu ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA. Hii ni blog maalumu inayoenda na kundi maalumu la wasap ambapo kila siku unajifunza na kuhamasika, kila wiki kuna madarasa ya mafanikio na kila mwaka kuna semina tatu nzuri sana kwa mafanikio yako.

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA tuma ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa wasap kwenda namba 0717396253 au fungua hapa;  www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Usomaji