Ni vigumu sana kuzijua tabia za binadamu, kwa sababu kinachotutofautisha sisi binadamu na viumbe wengine, ni uwezo wetu wa kuhadaa wengine. Tunaweza kuwatega wanyama wakali kama simba na chui kwa sababu wanatabirika. Lakini kumtega binadamu ni kugumu kwa sababu hatabiriki, na anaweza kuhadaa.

Hivyo unapojifanya unatafuta kujua tabia ya mtu, labda mtu unayemuajiri au unayetaka kushirikiana naye kwenye jambo fulani, kumwangalia kwa yale mambo unayotaka kushirikiana naye atakuhadaa. Mtu anaweza kukuambia yeye ni mchapa kazi na akakueleza sifa nyingi za namna amekuwa akichapa kazi.
Mtu anaweza kujiita chochote anachotaka na hata kukupa watu ambao ni mashahidi wa uongo wakimsifia kwamba ni mzuri kwenye mambo hayo.
Lakini yote hayo hayatakupa uhalisia wa jinsi ambavyo mtu alivyo. Na kwa kuwa ni vigumu mtu kukuonesha, unaweza kujiona upo njia panda.
Lakini ipo njia rahisi ya kuzijua tabia za mtu kwenye ufanyaji, na njia hiyo ni kumwangalia akiwa anafanya mambo tofauti kabisa, ambayo hayahusiani na kile unachotaka kumpima.
SOMA; UKURASA WA 1008; Maisha Ni Mlolongo Wa Miradi…
Kwa mfano kama mtu anakuambia ni mwaminifu kwenye biashara, halafu ukamkuta anamwibia mtu mwingine, hicho ni kiashiria kwamba siyo mwaminifu na ipo siku atakuumiza kwa tabia yake hiyo. Kama mtu anakuambia anaijali kazi, halafu siku mnapanga mkutane mahali anachelewa, ni kiashiria kwamba hayupo makini au hajali kile anachosema anajali.
Jinsi mtu anavyofanya kitu kimoja, ndivyo anavyofanya kila kitu. Unaweza kutumia hilo kupima chochote kwa mtu. Kwa kuangalia jinsi anavyowafanyia wale ambao wako chini yake, namna anavyowachukulia wale ambao wamemkosea au wanaotofautiana naye.
Kila tabia unayoiona kwa mtu, hata kama haihusiani na kile mnachofanya kwa pamoja, jua hiyo ndiyo tabia yake, na ipo siku tabia hiyo italeta matatizo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog