“Iron rusts from disuse; stagnant water loses its purity and in cold weather becomes frozen; even so does inaction sap the vigor of the mind.” — Leonardo da Vinci
Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee ketu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Ni kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari UKITULIA UMEKWISHA…
Watu wengi hufikiri maisha ni kupambana mwanzoni, kufanikiwa kisha kutulia. Kwamba ukishafanikiwa basi hupaswi kuhangaika tena, unapaswa kutulia na kufurahia matunda ya juhudi zako.
Rafiki, ukweli ni kwamba, kutulia ni kinyume na msingi na sheria za asili.
Kwa asili, chochote kinachotulia kinaharibika.
Chuma kikitulia mahali, bila ya kutumika kinashika kutu, kutu inakula chuma hicho na kinakuwa hakifai tena kwa matumizi.
Maji yakitulia sehemu moja kwa muda mrefu yanakuwa hayafai tena kutumia, yanabeba magonjwa na baridi ikija yanaganda kabisa.
Kutulia ni kinyume na sheria za asili, kwa asili mwendo ndiyo maisha, vitu vilivyopo kwenye mwendo ndiyo vinazidi kuwa bora na kuwa imara zaidi.
Hivyo kama bado upo hai, jua kwamba lengo la maisha siyo kupambana kisha kutulia. Bali kujua kile ambacho ni muhimu zaidi kwako, ambacho utakifanyia kazi kwa maisha yako yote.
Hata pale utakapofikia uhuru wa kifedha, kiasi kwamba hata usipofanya kazi kabisa maisha yanaenda, unahitaji kuwa na kitu cha kukushughulisha.
Wengi wamekuwa wanakufa muda mfupi baada ya kustaafu, kwa sababu wanatulia, wanaona wameshafanya sana na sasa ni muda wa mapumziko.
Maisha nimmchezo usio na muda wa mapumziko, muda unaolala ni mapumziko tosha.
Kitu pekee kitakachoendelea kukuweka hai, ni juhudi unazoweka, mapambano unayoendelea nayo.
Kamwe usikimbilie kutulia, hakikisha kila wakati upo kwenye mwendo, maana mwendo ndiyo dalili ya maisha, mwendo ndiyo sheria ya asili.
Kaza mwendo leo na uwe na siku bora sana.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha