Kuna vitu ambavyo kila mtu anapaswa kufanya, lakini wengi hawajui kama wanapaswa kufanya, na wanaweza kujiambia kwamba hawafanyi.

Wasichojua ni kwamba, chochote ambacho unapaswa kufanya halafu hufanyi, siyo kwamba hufanyi kweli, bali unafanya vibaya.

Kwa mfano kila mtu anauza, na kila kitu kwenye maisha kinahusisha kuuza. Wale wanaojitambua kama wauzaji na wakachukua hatua sahihi wanafanikiwa kwenye chochote wanachofanya. Ila wale ambao hawajui kama wanauza, au wanajiambia kabisa kwamba hawapendi kuuza, siyo kwamba hawauzi, bali wanauza vibaya. Kwa kujifanya kwao kwamba hawauzi, basi wanatumiwa vibaya na wale wanaonunua kile ambacho wangepaswa kuuza.

Kila mtu ni mtangazaji wa kile anachofanya, na yule anayesema kwamba siyo mtangazaji basi anatangaza vibaya.

Kila mtu anapaswa kuwa na falsafa ya maisha ambayo anaiishi kwenye maisha yake. Yule ambaye hajui ni falsafa gani anaishi, siyo kwamba hana falsafa, bali anaishi falsafa ambayo ni mbaya kwake.

SOMA; UKURASA WA 763; Hakikisha Watu Wanafanya Kile Wanachopaswa Kufanya….

Kila mtu ana jukumu kubwa la kuhakikisha maisha yake yanakwenda vizuri kwa mafanikio. Wale ambao wanajifanya hawajui, au wanakwepa majukumu yao, siyo kwamba majukumu hayo yanawakwepa, bali wanakuwa wanayafanya vibaya.

Unapaswa kujua kila kilicho muhimu kwenye maisha yako, na kuhakikisha unakifanya hasa, unakifanya kwa usahihi. Usijifanye hujui au hufanyi, unachokuwa umefanya ni kuchagua kufanya vibaya.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog