Kama ukisikia neno utajiri unajisikia vibaya, unapata mawazo ya watu wabaya, watu wanaowanyonya na kuwanyanyasa wengine, basi nina habari mbaya kwako, umejizawadia maisha ya umasikini mpaka kifo chako.

Akili yako ni janja sana, haiwezi kamwe kukupa kitu ambacho imani yako inapingana nacho, hivyo kama imani yako inaona matajiri ni watu wabaya, matajiri ni watu wasiofaa, basi akili yako itahakikisha inakuepusha na utajiri.

FEDHA KWA BLOG

Nimefungua makala ya leo kwa maelezo hayo muhimu kabisa, ili kuwaondoa wale ambao wanapenda unafiki linapokuja swala la fedha na utajiri. Utakuta wengi wanausema utajiri vibaya, lakini wakilala na kuamka wanachowaza ni fedha.

Fedha ni muhimu kwa mambo yanayohusu fedha, na kwa mara ya mwisho naangalia, kitu pekee nimekuwa nakipata bure bila ya kulipia fedha ni hewa ninayopumua. Vingine vyote vina gharama yake, ambapo ukiwa na fedha, mambo yanakwenda vizuri.

Sasa pamoja na kwamba watu wengi wanapenda kuwa matajiri, huwa ni wachache sana ambao wanafikia utajiri wa kweli. Katika watu 100 wanaotaka kuwa matajiri, ni watano pekee ambao wanafikia utajiri, na mmoja kati ya hao 100 ndiyo atakuwa na utajiri wa viwango vya juu sana.

Je nini kinatokea kwa wale 95, ambao walipenda sana wawe matajiri lakini hawawi? Je ina maana wale 5 wanaofikia utajiri ni wajanja sana kuliko wengine wote 95? Je ina maana wale 5 wana bahati zaidi?

Kitu kikubwa ambacho nimekuwa nakiona linapokuja swala la mafanikio, kama kuna wachache wamepiga hatua fulani lakini wengi wameshindwa, basi tatizo siyo ujanja wala bahati, bali tatizo lipo kwenye maarifa na ujuzi.

Kwamba wale 5 wanaofikia utajiri, kuna maarifa na ujuzi wanao, ambao wale 95 hawana. Na iwapo wale 95 watapata maarifa na ujuzi huo, na kuchukua hatua, basi hakuna kinachoweza kuwazuia kufikia utajiri.

SOMA; USHAURI; Jinsi Ya Kuituliza Fedha Unayoipata Ili Uweze Kutimiza Malengo Ya Maisha Yako.

Leo nakwenda kukushirikisha hatua ya kwanza kabisa ya kuelekea kwenye utajiri, ambayo wengi wamekuwa wanaipuuzia na inawagharimu. Hii ni hatua muhimu, ambayo imekuwa mtego kwa wengi, bila hata ya wao wenyewe kujua. Mtu anaona anaingiza kipato, lakini bado umasikini unakuwa umemganda.

Hatua ya kwanza na muhimu kabisa ya kuelekea kwenye utajiri ni KUONDOA UKOMO KWENYE KIPATO CHAKO.

Hii ndiyo hatua muhimu mno, ambayo kama hutaivuka, haijalishi una kipato kikubwa kiasi gani, hutaweza kufikia utajiri wa kweli.

Unapokuwa na ukomo kwenye kipato chako, unajizuia kufikia utajiri, kwa sababu kikomo kinakuzuia kufika juu zaidi.

Unapokuwa umeajiriwa, na kipato chako pekee ni mshahara, una ukomo kwenye kipato chako. Hata ulipwe mshahara mkubwa kiasi gani, ile tu kuwepo na ukomo kwenye kipato chako ni changamoto kwako.

BIASHARA NDANI YA AJIRA SOFT

Kama una biashara ambayo mteja ni mmoja au wachache, na wao ndiyo wanaamua biashara iwepo au la, unakuwa umejiwekea ukomo kwenye kipato chako. Hata ukazane kiasi gani, unajikuta unaendelea kuwa pale pale.

Hatua ya kwanza kabisa ya kuelekea kwenye utajiri, ambayo unapaswa kuizingatia, na kila unapoamka asubuhi ujikumbushe  ni kuondoa ukomo kwenye kipato chako.

Ondoa kabisa kila aina ya ukomo wa kipato. Kama una ajira pekee, unahitaji kuwa na njia nyingine za kukuingizia kipato. Kama una biashara, hakikisha una wateja wengi kiasi kwamba wateja wachache hawawezi kukutikisa kibiashara.

Kila unapoamka, jiulize ni ukomo gani unao kwenye kipato chako. Maana wengi wamekuwa wanafikiria ukomo ni kwa walioajiriwa tu. Lakini hakuna watu wenye ukomo mkubwa kwenye kipato kama waliojiajiri.

SOMA; Tabia Hii Moja Itakufanya Uendelee Kuwa Masikini Maisha Yako Yote. Jifunze Hapa Namna Ya Kuiepuka

Kama umejiajiri kuwashauri watu, na unalipwa kwa masaa unayoshauri watu, unaweza kufanya kazi masaa mangapi kwa siku? Huoni kuna ukomo wa muda hapo?

Kama umeanzisha biashara, lakini kama wewe haupo biashara hiyo haiwezi kwenda, huoni kwamba bishara yako ndiyo ukomo wa kipato chako? Kwa sababu biashara unayotaka uwepo wako muda wote, inakunyima uhuru zaidi wa kukuza biashara hiyo na nyingine.

Ondoa kila aina ya ukomo kwenye kipato chako, hakikisha unakuwa huru sana linapokuja swala la kipato, na kazana sana kujenga mifumo ambayo itaweza kufanya kazi bila ya uwepo wako wa moja kwa moja.

Kosa kubwa wengi wanalofanya wanapojiajiri au kuanzisha biashara, ni wao ndiyo wanakuwa biashara zenyewe, hivyo wasipokuwepo, hakuna biashara. Hivyo kabla hujawacheka walioajiriwa, ambao wana ukomo kwenye mshahara, jiulize je kwenye biashara yako una uhuru wa kipato?

Mwisho kabisa, ningependa nikukumbushe kwamba, hatua ya kuondoa ukomo kwenye kipato chako siyo ngumu. Kwa sababu watu bado wana shida, watu bado wana matatizo na watu bado wana mahitaji ambayo wapo tayari kulipia ili kuyapata.

Hivyo ukiweza kuona matatizo au uhitaji wa watu, kisha kuja na suluhisho, ambalo linaendeshwa kwa mfumo ambao siyo lazima uwepo moja kwa moja, itakuwa hatua nzuri sana kwako.

Ondoa ukomo kwenye kipato chako, hakikisha muda, nguvu na hata rasilimali haziwi kikwazo kwako kupiga hatua na kufikia utajiri, hali ambayo wengi wanaipenda, lakini wachache pekee ndiyo wanaifikia.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Rafiki, kama ungependa kujifunza zaidi kupitia mafunzo ninayotoa, karibu ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA. Hii ni blog maalumu inayoenda na kundi maalumu la wasap ambapo kila siku unajifunza na kuhamasika, kila wiki kuna madarasa ya mafanikio na kila mwaka kuna semina tatu nzuri sana kwa mafanikio yako.

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA tuma ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa wasap kwenda namba 0717396253 au fungua hapa;  www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Usomaji