Rafiki yangu mpendwa,

Moja ya vitu vinavyowafanya wengi wakose usingizi ni fedha.

Sehemu kubwa sana ya watu wanaishi kwa mfumo wa mkono kwenda kinywani. Yaani wanafanya kazi au biashara, wanalipwa kiasi kidogo cha fedha, wanaitumia kwenye chakula halafu wanabaki hawana fedha nyingine. Inawabidi wakafanye tena kazi au biashara ndiyo wapate tena fedha ya kula.

Wakati mwingine kile kiasi cha fedha wanachopata hakiwatoshi kulingana na mahitaji yao, hivyo wanaingia kwenye madeni, wanakopa ili waweze kukidhi mahitaji muhimu ya maisha yao.

Maisha ya aina hiyo huwa yanaenda kwa mazoea, mpaka pale linapotokea jambo ambalo linamfanya mtu asiweze kufanya kazi au biashara yake kama alivyozoea. Labda anakuwa amefukuzwa kazi, au ameumwa na hivyo hawezi kwenda kwenye biashara yake. Hapo ndipo mambo yanakuwa magumu na mtu anakuwa hana namna ya kuendesha tena maisha yake.

Rafiki yangu, kama upo kwenye kundi la aina hii, au upo kwenye kundi la watu ambao wanafanya kazi sana, lakini kipato wanachopata bado ni kidogo, basi vipo vitu viwili vinavyokuzuia kupata kile kiasi cha fedha unachotaka kupata.

KWA NINI SIYO TAJIRI

Simaanishi kwamba uko hapo ulipo kwa sababu ya vitu hivi viwili ninavyokwenda kukushirikisha hapa, kuna mengi yanachangia, lakini hivi viwili ndivyo msingi mkuu wa wengi kushindwa kupata kiasi cha fedha wanachotaka kupata kwenye kazi au biashara zao.

Kitu cha kwanza; kuna kitu hujui kuhusu fedha.

Kama kuna kitu huna kwenye maisha yako, basi tatizo linaanzia na ujuzi wako juu ya kitu hicho. Mara nyingi kuna kitu utakuwa hujui kuhusu kile ambacho huna. Na kwenye fedha ndivyo ilivyo, sehemu kubwa sana ya watu hawajui kuhusu fedha.

Na siyo kosa lako, maana hakuna popote ambapo umewahi kufundishwa kuhusu fedha. Maisha yako yote umejifunza kuhusu fedha kwa mazoea, kutoka kwa watu ambao nao hawajawahi kufundishwa kuhusu fedha.

Umekuwa unawaangalia wazazi na walezi wako, wakiteseka na fedha miaka yote, na wewe umeondoka na somo hilo. Umekuwa ukiwaangalia wakikopa na kufanya vitu visivyo vya msingi na wewe umeondoka na darasa hilo.

Hatua ya kwanza na muhimu unayopaswa kuchukua kuhusu fedha ni kupata ELIMU YA MSINGI YA FEDHA. Kwanza unahitaji kujua kuhusu fedha, msingi mkuu wa fedha. Unahitaji kujua kuhusu njia sahihi za kuongeza kipato chako, unapaswa kujua jinsi ya kukitumia na jinsi ya kuwekeza kipato chako ili kikuzalishie zaidi.

Unapaswa kujua wakati gani wa kukopa na wakati upi siyo wa kukopa, unapaswa kujua kuhusu aina mbalimbali za uwekezaji ambazo zitaifanya fedha yako ikufanyie wewe kazi hata kama umelala.

Kuendelea kuishi kwa mkono kwenda kinywani, hata kama unalipwa fedha nyingi kiasi gani, ni kujiweka kwenye hatari kubwa ya maisha yako. Kama usipofanya kazi moja kwa moja au usipokuwepo kwenye biashara yako moja kwa moja utakosa fedha ya kula, basi upo kwenye kundi la mkono kwenda kinywani, upo kwenye kundi hatari sana kifedha.

SOMA; Hatua Ya Kwanza Muhimu Sana Ya Kuelekea Kwenye Utajiri, Ambayo Wengi Wanaipuuza Na Inawagharimu Sana.

Kitu cha pili; huchukui hatua kubwa na sahihi kuhusu fedha.

Kitu cha pili kinachokuzuia usipate kiasi cha fedha unachotaka kupata, ni kiwango cha hatua unazochukua. Hatua unazochukua kwenye eneo la fedha, zinachangia sana kiasi cha fedha unachopata.

Kama unachukua hatua ndogo, au hatua za kawaia, utapata fedha kidogo na za kawaida. Kama unachukua hatua kubwa, na zisizo za kawaida, utapata fedha nyingi.

Na kuchukua hatua kubwa haimaanishi tu kufanya kazi muda mrefu, kama unafanya kazi muda mrefu, lakini kwa mazoea, hakuna kiasi kikubwa cha fedha unaweza kupata. Kama unafanya biashara yako kuanzia asubuhi mpaka usiku, lakini unaifanya kwa mazoea, huwezi kupata fedha nyingi.

Kitu cha kwanza unahitaji kufanya ni kuangalia wengine wanafanya nini, halafu usifanye kama wao. Fanya kinyume kabisa na wao kama wanafanya kwa mazoea na fanya mara kumi ya wanavyofanya wao.

Kama umeajiriwa weka kaza ya tofauti kabisa, ambayo hakuna mwingine anaweza au yupo tayari kufanya, kwa njia hiyo utaongeza thamani yako na kipato chako kitaongezeka pia.

Kama unafanya biashara, weka thamani kubwa kwenye bidhaa na huduma zako kiasi kwamba mteja aone kama anakuibia hivi, mteja aone akilinganisha hela aliyolipa na thamani aliyopata, basi ni sawa na amepata bure. Ni kiwango hichi cha uchukuaji wa hatua ambacho kitakutofautisha na wengine kabisa na kitafanya fedha nyingi sana ziweze kuja kwako.

Hivi ndivyo vitu viwili vinavyokuzuia wewe kupata kiasi cha fedha unachotaka kufanya. Tafakari kwenye maisha yako na angalia kipi unajua na kipi hujui kuhusu fedha, pia angalia kiwango cha hatua unazochukua kama kweli kinaendana na kiasi cha fedha unachotaka kupata.

HATUA ZA KUCHUKUA.

Leo hii rafiki, hakikisha unapata ELIMU YA MSINGI YA FEDHA, haya ni mafunzo ambayo yapo ndani ya KISIMA CHA MAARIFA. Kama tayari ni mwanachama unaweza kuyarejea mafunzo haya kwa kufungua hapa; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/seminafedha/ Kama bado hujawa mwanachama, utashindwa kuyafungua hayo masomo. Karibu ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA leo kwa kulipa ada ya mwaka na utaweza kuyapata masomo hayo na mengine mengi mazuri kuhusu mafanikio yako. Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA, niandikie ujumbe kwa njia ya wasap namba 0717396253 wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Rafiki, kama ungependa kujifunza zaidi kupitia mafunzo ninayotoa, karibu ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA. Hii ni blog maalumu inayoenda na kundi maalumu la wasap ambapo kila siku unajifunza na kuhamasika, kila wiki kuna madarasa ya mafanikio na kila mwaka kuna semina tatu nzuri sana kwa mafanikio yako.

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA tuma ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa wasap kwenda namba 0717396253 au fungua hapa;  www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Usomaji