Ukitaka kueleweka vizuri, ukitaka kushawishi watu wachukue hatua, ukitaka ujumbe wako ufike vizuri, picha ni muhimu zaidi kuliko maneno.
Unaweza kutoa maelezo yenye kuonesha data na kile ambacho ni kweli, lakini watu hawapendi kusikia tu maelezo na kusikia ukweli.
Watu wanataka kitu kitakachowahamasisha, kitakachowafanya wajione ni sehemu ya kile wanachosikiliza.

Na njia bora ya kufanya hivyo ni kutumia picha.
Unaweza kutumia picha halisi, ambayo mtu akiangalia anaona kile ambacho anataka yeye kuona, na maelezo yatamfanya ajione kuwa ndani ya kitu kile. Kwa mfano unaweza kuwaeleza watu kuhusu hatari ya magonjwa kwa watoto, ukawapa na data za watoto wanaokufa kutokana na magonjwa hayo, lakini kama unataka watu waelewe vizuri, washirikishe picha ya mtoto ambaye anaugua magonjwa unayozungumzia.
SOMA; UKURASA WA 1005; Usishushe Viwango Vyako…
Njia nyingine ya kutumia picha ni lugha ya picha. Siyo kila wakati utaweza kuwa na picha, lakini hilo halikuzuii kutumia nguvu ya picha. Unaweza kutumia lugha ya picha, ambapo mtu kwenye akili yake, anaona taswira ya kile unachoelezea. Lugha ya picha inakuwa na nguvu kama picha yenyewe kwa sababu mtu ndiye anayetengeneza picha yake mwenyewe.
Picha inaeleza mengi, picha inateka hisia, picha inamfanya mtu ajione ni sehemu ya kile anachosikia au kujifunza.
Unapotaka watu wakuelewe vizuri, tumia picha na lugha ya picha. Mifano na hadithi zinajenga picha nzuri pia.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog