Wealth is the product of man’s capacity to think. —Ayn Rand

Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari CHANZO KIKUU CHA UTAJIRI…
Watu wanapenda vitu, lakini huwa hawajui chanzo cha vitu hivyo.
Wanafikiri kwa kupenda na kutamani vitu basi watavipata tu, kwa sababu wengine wanavyo.

Unapoona mti umeota mahali, ni kwa sababu ilitangulia mbegu, ambayo ilikuwa mbegu ndogo sana.
Hata unavyouona mbuyu mkubwa, kabla haujawa mbuyu, ulikuwa mbegu ya ubuyu, ambayo ni ndogo sana.

Kadhalika vile viti tunavyoviona kwenye maisha ya watu, havikuanza kama vitu, vilianza kama wazo, vilianza kama maono, vilianza kama ndoto.
Baadaye watu hao wakafanyia kazi mawazo hayo na kuweza kuleta matokeo yanayoonekana.

Kadhalika kwenye fedha na utajiri, utajiri hauanzi na hela,
Kama ingekuwa hivyo, wale wanaoshinda bahati nasibu ma wanaorithi mali wangeendelea kuwa nanutajiri mkubwa.
Lakini wengi hupoteza mali hizo ndani ya muda mfupi na kurudi kwenye maisha waliyozoea.

Utajiri unaanzia kwenye fikra,
Utajiri ni zao la uwezo wa mtu kufikiri kwa usahihi.
Kama huwezi kufikiri vizuri, kama huna ndoto kubwa unayofanyia kazi, ni sawa na mbegu isiyo na uwezo wa kutoa mmea hai ndani yake.

Hivyo eneo kubwa la kufanyia kazi ni fikra zetu, maana hizi ndiyo zinazalisha matokeo yetu.
Unahitaji kuwa na maono na ndoto kubwa unayofanyia kazi, na muda wako mwingi uutumie kufikiria ndoto yako hiyo.
Kwa njia hii utajifunza njia sahihi za kuifikia, na pia kuiambia dunia ikuweke kwenye mazingira ya kuifikia ndoto yako hiyo.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kutengeneza na kuishi ndoto yako kubwa.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha