Maumivu ni sehemu ya maisha, na kama falsafa nyingi zinavyotufundisha, maumivu tunatembea na kukutana nayo kila siku. Kinachotufanya tukue na kufanikiwa ni maumivu tunayokutana nayo.

Watu wamekuwa wakitumia njia mbalimbali kutaka kuondokana na maumivu wanayokutana nayo. Lakini njia rahisi ambayo watu wamekuwa wanakazana nayo, imekuwa inazidisha maumivu badala ya kuyaondoa.

Tatizo kubwa

Njia mbaya ya kuondokana na maumivu ni kujilazimisha kuondokana na maumivu. Pale unapoilazimisha akili iondokane na maumivu, unazalisha maumivu zaidi. Akili haiwezi kutafuta suluhisho la maumivu kwa sababu yenyewe ni sehemu ya tatizo lililoleta maumivu.

Ni sawa na polisi ambaye ni mwizi, anatumwa afanye upelelezi wa kumkamata mwizi, ambaye ni yeye mwenyewe. Kitu ambacho hakiwezi kuzaa matunda, maana hatakuja na majibu ya upelelezi yakimtaja yeye kuwa mwizi.

SOMA; UKURASA WA 955; Zawadi Kubwa Unayoweza Kumpa Mtu Kwenye Zama Hizi…

Njia bora ya kuondokana na maumivu, ni kuweka akili yako pale ulipo sasa. Kwa sababu maumivu huwa yanaanza pale akili yako inapokuwa kwenye mambo yaliyopita au mambo yajayo. Lakini ukiiweka akili yako kwenye kile unachofanya sasa, na kutokukubali kuvutwa nyuma au mbele, maumivu hayatakuwa na sehemu ya kuwepo.

Mateso hayawezi kuhimili muda wa sasa, hivyo unapoupa muda umuhimu wake, na kutoruhusu akili yako irukeruke, hutaweza kukutana na maumivu.

Weka akili yako pale ulipo, kwenye kile unachofanya, na hutakuwa na nafasi kwa ajili ya maumivu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog