Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo. Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari JINSI YA KUITENGENEZA BAHATI…
Kwenye maisha, kuna watu ambao huwa tunawaona wana bahati kweli kweli.
Kila jambo zuri linalotokea, linatokea kwao.
Huwa tunatamani na sisi bahati hizo zitufike, lakini wengi huona kama hawakuzaliwa na bahati.
Ipo hivi rafiki, bahati siyo kitu cha kizaliwa nacho, bali ni kitu kinachotengenezwa.
Bahati ni pale maandalizi yanapokutana na fursa, hivyo bila ya maandalizi, hakuna bahati.
Hivyo, ili kujitengenezea bahati, zingatia yafuatayo;
👉🏼Jua nini unataka kweny maisha yako, jua kwa uhakika, usiyaendee maisha kama bahati nasibu, kwamba chochote kinachotokea ni sawa, jua unataka nini hasa.
👉🏼Jua kila unachoweza kujua kuhusiana na kile unachotaka, jua historia yake, jua nje ndai kuhusiana na kitu hicho, jua waliofanikiwa kwenye kitu hicho, na jua kanuni za mafanikio kwenye kitu hicho.
👉🏼Ishi kanuni za mafanikio ulizojifunza, fanya kile ambacho waliofanikiwa wanafanya. Mafaikio yanaacha alama, hivyo ikifuata alama, utafika walipofika wengine.
👉🏼Endelea kujifunza kila siku, isifike hatua ukajiambia tayari unajua kila kitu, ukifika hatua hiyo umekwisha.
👉🏼Jaribu mambo mapya kila wakati, jaribu mambo hatari, ambayo unaweza kushindwa, kuwa mbunifu.
👉🏼Ukishindwa kaa chini na jiulize wapi ulipokosea na wapi unaweza kuboresha zaidi.
👉🏼Kuwa mbele ya mabadiliko, badilka kabla mabadiliko hayajatokea, na ukichelewa kuwa mbele ya mafanikio basi nenda na mfanikio. Usijaribu kuyapinga mafanikio.
👉🏼Angalia mwenendo wa mambo, na jiandae vyema kwa yale yanayokuja.
👉🏼Jifunze kupitia kila anayefanya unachofanya, na wasiofanya pia.
Bahati inatengenezwa, na utaweza kuitengeneza ukishajua nini unataka na kujitoa kweli kukipata. Utakutana na fursa nzuri ukiwa umejiandaa, na watu wataona una bahati, kumbe unajituma kuliko kawaida.
MUHIMU; Hatuzungumzii bahati ya kushinda tatu mzuka!
Uwe na siki bora leo, siku ya kutengeneza bahati, ili kuweza kutumia vizuri fursa zinazokuzunguka.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha