Kosa kubwa ambalo watu wengi wamekuwa wanafanya, ambalo linawazuia kufanikiwa kwenye chochote wanachofanya, ni kujumuisha mambo au watu.

Kwa sababu mtu mmoja amesumbua au amekuangusha basi unachukulia watu wote waliopo kundi moja na mtu huyo hawafai.

Kwa sababu umejaribu kitu kimoja ukashindwa, basi unachukulia vitu vingine vyote navyo vitashindikana tu.

Tatizo kubwa

Hii siyo sahihi, na inakuzuia kuziona na kuzitumia fursa nyingi zinazokuzunguka.

Haijalishi watu wanafanana kiasi gani, ni kosa kuwa kuwajumuisha watu wote kwa makosa ya mtu mmoja.

Haijalishi hali zinafanana kiasi gani, ni kosa kujumuisha hali zote kwa sababu ya hali moja uliyokutana nayo.

Watu wanatofautiana na hali zinatofautiana.

SOMA; DARASA LA JUMAPILI; JINSI YA KUFIKIRI KWA KINA NA KUFANYA MAAMUZI SAHIHI.

Hivyo haijalishi mtu mmoja amefanya nini, usipeleke makosa yake kwa mwingine ambaye hata hujampa nafasi.

Kadhalika kwenye wateja wa biashara au chochote unachofanya. Kwa sababu mmoja kanunua haimaanishi wengine kama yeye watanunua. Na kwa sababu mmoja amekataa kununua, usiache kuwaambia wengine kama yeye na wao pia wanunue.

Usije kutumia kauli ya wote ni wale wale labda kama umeshasafiri dunia nzima na kumjaribu kila mtu na kila kitu.

Dunia ina watu zaidi ya bilioni saba, huwezi kusema watu wote ni wale wale. Watu wanatofautiana, inapowezekana, mpe kila mtu nafasi na akishindwa, mhukumu yeye kama mtu, na usijumuishe kundi lote la watu ambalo linafanana na yeye.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog