Habari rafiki yangu?

Ni matumaini yangu kwamba uko poa kabisa na unaendelea kuweka juhudi kubwa kwenye maisha yako ili kuweza kufikia ndoto kubwa za maisha yako ambazo unazo. Endelea kuweka juhudi hizo rafiki na kamwe usidanganyike na njia yoyote ya mkato, kwa sababu njia zote za mkato ni njia ndefu. Kupata chochote unachotaka, lazima uweke kazi, lazima uweke muda.

Juma lililopita nilishirikisha makala inayoeleza hasara kubwa mbili za mitandao ya kijamii kwenye maisha ya wengi na jinsi ya kujikinga na hasara hizo. Pia nilieleza kwamba nimejiondoa kwenye mitandao yote ya kijamii niliyokuwa natumia baada ya kufanya tathmini na kuona muda na nguvu ninazoweka huko, hazizalishi matunda sana na kama nikihamishia nguvu hizo kwenye kutoa kazi bora kabisa za uandishi na mafunzo.

kujiondoa mitandao

Kama hukupata nafasi ya kusoma makala ile, unaweza kuisoma hapa; Hasara Mbili Kubwa Unazopata Kwenye Mitandao Ya Kijamii (Na Kwa Nini Sipo Tena Kwenye Mitandao Ya Kijamii)

Baada ya makala ile, nimepata maswali kutoka kwa baadhi ya wasomaji wakitaka kujua wanawezaje kujitoa kwenye mitandao hii. Nilipoona swali kwa mtu mmoja nikajiuliza hivi huyu anatania au ana shida gani? Yaani mtu aweze kujiunga na mtandao lakini asijue jinsi ya kujitoa?

Lakini ninaendelea kuona swali kutoka kwa wengine, wanawezaje kujitoa kwenye mitandao hii. Hapo ndipo nilipoacha kulichukulia hili swali kiurahisi na kujiuliza kwani kuna tatizo gani hapa? Nilipoangalia kwenye kila aina ya mtandao, nikagundua siri kubwa ya mitandao hii.

Kujiunga ni rahisi, wanakuletea kila kitu wazi kwenye kujiunga. Lakini kujitoa ni kugumu kweli, kujitoa kumefichwa mbali, inabidi utafute kweli mpaka upate sehemu ya kujitoa. Na hata ukifika sehemu hiyo, unaweza usijue kama ndiyo sehemu sahihi ya kujitoa, maana wanaweza kukuchanganya na lugha, wakakuambia usisimamishe akaunti yako kwa muda badala ya kuifuta.

Sasa nakwenda kukushirikisha njia rahisi ya kujitoa kwenye mitandao yote ya kijamii unayotumia, na kwa njia hiyo utajua mitandao mingine ambayo ulishajiunga huko nyuma bila hata ya wewe mwenyewe kujua.

Kwa kifupi, njia hii itakuonesha maeneo yote ambapo taarifa zako za mawasiliano zinapatikana kwenye mtandao wa intaneti, na wewe utachukua hatua ya kupunguza kule usikotaka taarifa zako ziwe.

Njia hiyo rahisi ya kujiondoa kwenye mitandao ni kuingia kwenye tovuti hii; www.deseat.me

Ukiingia kwenye tovuti hiyo, kuna sehemu imeandikwa sign up bonyeza hapo na jiunge kwa akaunti yako ya google, ambayo email yake ndiyo unatumia kujiunga na mitandao mbalimbali. Baada ya hapo utaorodheshewa mitandao yote uliyojiunga nayo na mbele yake panaandikwa DELETE.

Ukibonyeza hapo kwenye DELETE, itakupeleka moja kwa moja kwenye mtandao husika, kwenye eneo la kujitoa, na hapo unaendelea na mchakato wa kujitoa.

Hiyo rafiki yangu, ndiyo njia rahisi ya kujitoa kwenye mitandao yote ya kijamii unayotumia.

Kama nilivyoeleza kwenye makala ya kwanza, huhitaji kujitoa kwenye mitandao ya kijamii kwa sababu mimi au mwingine amefanya hivyo. Bali unahitaji kupima, unahitaji kufanya tathmini na kama utaona mitandao hii ina hasara kwako kuliko faida, basi jitoe bila ya kufikiria mara mbilimbili.

Lakini kama mitandao hii ina manufaa kwako, kwa maana kwamba inakuingizia fedha zinazoendana na muda unaotumia huko, au inakuwezesha kuwafikia watu wengi zaidi ambao baadaye wananufaika na wewe unanufaika, basi endelea kuitumia mitandao hiyo.

Fanya maamuzi kulingana na pale ulipo kwenye maisha yako. Na kama umekuwa rafiki mzuri, kwa maana kwamba unazingatia haya tunayojifunza kila siku, basi nina uhakika unaweza kufanya maamuzi haya kwa usahihi kabisa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Rafiki, kama ungependa kujifunza zaidi kupitia mafunzo ninayotoa, karibu ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA. Hii ni blog maalumu inayoenda na kundi maalumu la wasap ambapo kila siku unajifunza na kuhamasika, kila wiki kuna madarasa ya mafanikio na kila mwaka kuna semina tatu nzuri sana kwa mafanikio yako.

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA tuma ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa wasap kwenda namba 0717396253 au fungua hapa;  www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Usomaji