“Man, like a bridge, was designed to carry the load for a moment, not the combined weight of a year all at once” – William A. Ward.

Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari BEBA UZITO KWA MUDA…
Sisi binadamu ni kama madaraja,
Daraja hata liwe imara kiasi gani, linaloweza kuvusha magari yenye uzito mkubwa kiasi gani, halitadumu muda mrefu iwapo magari yenye mizigo mizito yatasimama pale badala ya kupita.

Kazi ya daraja ni kupitisha magari, yenye mizigo mizito, na siyo kuyaacha magari yale juu ya daraja hilo kwa muda mrefu.

Kadhalika hivyo ndivyo tulivyo sisi binadamu.
Tunaweza kubeba uzito mkubwa kwa muda mfupi, lakini siyo kukaa nao kwa muda wote.
Tunaweza kukaa na msongo wa mawazo kwa muda mfupi, lakini tunapokaa nao kwa muda mrefu unatuumiza zaidi.
Tunaweza kupata maumivu kwa muda mfupi, tukavumilia na kusonga mbele, lakini maumivu yakiwa ya muda mrefu yanatuangusha.
Tunaweza kufanya kazi kubwa na ngumu sana kwa muda mfupi, lakini kwa muda mrefu inatuumiza.

Asubuhi ya leo, tafakari ni mizigo gani ambayo ilipaswa kupita kwa muda lakini wewe umeiacha ikae kwenye maisha yako kwa muda mrefu.
Ukishajua mizigo hiyo, itue ili uweze kusonga mbele.
Beba mzigo wowote utakao kwa muda mfupi, kisha utue na kusonga mbele.

Ukawe na siku bora sana ya leo rafiki yangu,
#SkinInTheGame, #AllIn, #WhateverItTakes, #10X, #DayOne.

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha