Without constant activity, the threats of life will soon overwhelm the values.” —Jim Rohn
Mwanamafanikio,
Leo tena tumeipata siku mpya, siku bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora kabisa.
Nafasi tuliyoipata leo, haitajirudia tena kwenye maisha yetu, hivyo tunapaswa kuitumia vizuri ili kuweza kupata matokeo bora kabisa.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari USIKOSE CHA KUFANYA KILA WAKATI…
Rafiki, kila wakati unapaswa kuwa na kitu cha kufanya, unapaswa kuwa na kitu kinachoyabeba mawazo yako na kutumia nguvu zako.
Ukiruhusu muda wowote uwe huna cha kufanya, hapo ndipo unapokaribisha hofu kwenye maisha yako.
Hapo ndipo unapoanza kufikiria kwamba mambo ni magumu na hayawezekani.
Hapo ndipo unapoanza kusikiliza maneno ya wakatishaji tamaa na ukakosa nguvu ya kuendelea.
Lakini kama utaijaza siku yako, kila dakika ukawa na cha kufanyia kazi, hutapata kabisa nafasi ya kufikiria hofu, kushindwa au kuwasikia wanaokukatisha tamaa.
Akili yako inakuwa bize na yale muhimu unayofanya na nguvu zako zinatumika kisawasawa, ukimaliza siku yako unakuwa umechoka kiasi kwamba unataka tu kupumzika na siyo kufikiria kuhusu hofu au wengine.
Kama pia unafikiria wengine wanakuchukuliaje, au wanasemaje juu ya unachofanya, ni dalili kwamba hutumii muda wako vizuri.
Kama unaweza kuwasikia wengine wanaokukatisha tamaa, umeweka mwanya makubwa kwenye muda wako kiasi cha kukaribisha mambo ya hovyo.
Wanasema akili tupu ni karakana ya maovu,
Hivyo basi, muda mtupu ambao huna cha kufanya ni karakana ya kutengeneza kushindwa.
Jaza kalenda yako ya siku, kila dakika kuwa na kitu unachofanya, na akili zako zote ziwe kwenye kile unachofanya.
Hata kama ni kula, akili yako yote iwe pale kwenye kula.
Dhibiti akili yako na muda wako kwa kiasi hicho, na utaona jinsi ulivyo na nguvu na uwezo mkubwa ndani yako wa kufanya chochote unachotaka kufanya.
Uwe na siku bora sana leo, siku yenye kitu cha kufanya kwenye kila dakika.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha