Kama unajua kile unachotaka, na unaweka juhudi kubwa ili kuweza kukipata, lakini matokeo unayopata ni tofauti kabisa na matarajio, basi jua bila ya shaka yoyote kwamba kuna maarifa unakosa.
Kuna kitu ambacho hukijui, ndiyo maana hupati kile ambacho unataka. Na wakati mwingine, kile unachojua kinaweza kuwa ndiyo kikwazo kwako kupata kila unachotaka.

Hivyo unahitaji kukaa chini na kufanya tathmini, kujiuliza kipi ambacho hujui, kinachokuzuia kupata unachotaka? Pia unahitaji kujiuliza kwa yale unayojua kuhusu hicho unachotaka, je yote ni sahihi? Hakuna ambacho unakijua na kimekuwa kinakurudisha nyuma badala ya kukusogeza mbele?
Juhudi watu wanaweka sana, lakini matokeo wanayopata ni madogo sana. wapo watu wanaofanya kazi ngumu na kwa kujituma sana, lakini miaka yote wako pale pale walipo. Huu ni ushahidi tosha kwamba kile ambacho hawakijui, au wanachokijua lakini siyo sahihi, kinawakwamisha.
Hivyo rafiki, usikate tamaa pale unapokosa kile unachotaka, badala yake jua kile usichojua na tenga muda kujifunza kitu hicho kwa kina. Ndiyo maana ni muhimu sana kuendelea kujifunza kila siku, bila ya kujali umepiga hatua kiasi gani. Kwa sababu kila hatua zaidi unayohitaji kupiga, unahitaji kujua kitu ambacho kwa sasa hujui.
SOMA; UKURASA WA 1106; Wale Unaowavumilia, Ndiyo Wanaokutengeneza…
Matokeo unayopata sasa, ni kutokana na maarifa uliyonayo sasa. Hata ukiongeza juhudi kiasi gani, hata ukiwa na hamasa kubwa kiasi gani, matokeo utakayoendelea kupata hayatatofautiana sana na unayopata sasa. Ili kupata matokeo ya tofauti, unahitaji kuwa na maarifa tofauti, maarifa bora zaidi ya uliyonayo sasa.
Jifunze kile ambacho hujui, na kama kipo ambacho unajua lakini kinakuwa kikwazo kwako, kiondoe kwa kujifunza kile ambacho ni sahihi. Ukijifunza maarifa sahihi, ukayaelewa na kuyafanyia kazi, hakuna kitakachoweza kukuzuia kufanikiwa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog