Rafiki yangu mpendwa, sijajua ni siku zinaenda kasi, mambo yanakuwa mengi au sisi ndiyo tunaenda taratibu, maana majuma yanaonekana kukatika kwa kasi ya ajabu.

Kama hivi tunamaliza juma la 22 la mwaka huu 2018, tuna majuma matatu mbele yetu kufika nusu ya mwaka huu 2018, hivyo chochote ulichokuwa umepanga kufanya mwaka huu 2018, unahitaji kuwa umeshafikia angalau nusu kama una matumaini ya kukikamilisha.

Lakini kama bado hujaanza, unaweza kuanza sasa, na ukaweka juhudi mara mbili na ndani ya mwaka huu 2018 ukafika ulikotaka kufika. Ninaposema juhudi mara mbili namaanisha hivyo kweli, kwamba kwa vyovyote unavyofanya sasa, basi unahitaji kufanya mara mbili na zaidi.

Nikukaribishe rafiki yangu kwenye TANO ZA JUMA, mkusanyiko wa mambo matano muhimu ninayokuandalia wewe rafiki yangu kila mwisho wa wiki, ili uweze kujifunza na kuchukua hatua kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi.

Ili kuzifaidi hizi tano za juma, hakikisha kwa kila unachojifunza, kuna hatua unayokwenda kuchukua mara moja bila hata ya kujiuliza mara mbilimbili kama kinakufaa au la, kwa lengo tu la kuona matokeo yake. Unaweza kujaribu kitu kwa siku 30, ukaona matokeo yake kisha ukaamua kuendelea au kuacha.

Kwenye juma hili la 22 nimekuandalia mambo haya matano muhimu sana, yapitie ukiwa umetulia, jifunze na chukua hatua kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi.

#1 KITABU NILICHOSOMA; UFALME ULIO MKUU (THE GREATEST EMPIRE.)

Juma hili nimesoma vitabu vitatu, na moja katika vitabu hicho ni kitabu kinachoelezea maisha ya mwanafalsafa wa ustoa, Seneca. Kitabu hichi kinachoitwa THE GREATEST EMPIRE, kimeyachambua maisha ya mwanafalsafa huyu, ambaye ni shujaa wangu kwa uzuri sana. Kitabu kimeangalia pande zote, kwa upande ulioonesha maisha yake kuwa ya unafiki, yaani maneno na matendo yake kutokuendana, na upande wa pili kimeonesha utetezi ambao Seneca alikuwa akitoa kuhusu maisha yake, kupitia maandiko yake.

Kitabu kinaanza na kauli ya Seneca inayosema; ufalme ulio mkuu ni kuwa mfalme wako mwenyewe (the greatest empire is to be emperor of oneself). Hii ni kauli yenye nguvu sana kwa sababu watu wanapenda kuwatawala wengine, kuwaongoza wengine, wakati wao wenyewe hawawezi kujitawala au kujiongoza. Ukiweza kujitawala mwenyewe, ukajiongoza mwenyewe, basi dunia nzima itakuwa chini yako, na siyo kwa ubaya, bali kwa wema.

Sasa tuingie kidogo kwenye maisha ya Seneca;

Seneca alikuwa mwanafalsafa, mwandishi, mwanasiasa na tajiri mkubwa sana kwa zama alizoishi. Na hili lilifanya wengi kumwona ni mnafiki, kwa sababu falsafa aliyoiishi, falsafa ya Ustoa ni falsafa inayotaka watu kuwa na kiasi. Na hata kwenye maandiko yake mengi, Seneca amekuwa akionesha kwamba kuwa na mali nyingi siyo uhakika wa kuwa na maisha ya furaha, na pengine akionesha kabisa kwamba mahitaji ya msingi ni machache na kila mtu anaweza kuyapata, lakini kinachowatesa wengi ni hamasa.

Kwa upande wa pili, maisha ya Seneca yalikuwa maisha ya mateso, kwanza alikuwa na ugonjwa sugu wa mapafu tangu akiwa mdogo, ambao unadhaniwa kuwa pumu au kifua kikuu, afya yake ilikuwa dhoofu sana na alifikia hatua ya kutaka kujiua. Kwa upande wa pili, ushiriki wake kwenye siasa za Roma ulimpelekea kuwekwa kizuizini kwa miaka 8, baadaye akarudishwa na kuwa mwalimu wa kijana aliyeandaliwa kuwa mfalme, ambaye baadaye alimtuhumu Seneca kutaka kumpindua na kuamuru auawe. Hivyo maisha ya Seneca yaliishia kwenye kifo ambacho nacho hakikuwa rahisi, kwa sababu mwili wake ulikuwa dhaifu, alijaribu njia tatu za kujiua ndiyo akafa kwa kunywa sumu.

Maisha haya ya Seneca yamewafanya wanahistoria na waandishi wengi kutaka kujifunza kwa kina na kujua namna alivyoishi na kuendesha maisha yake. Katika kitabu hichi mengi yameelezewa, kupitia maandiko yake na maandiko ya wengine walioishi zama zake, zaidi ya miaka 2000 iliyopita.

Kuhusu kuwa mwanafalsafa na kuwa tajiri, Seneca anasema kuna aina mbili za wanafalsafa matajiri;

Aina ya kwanza ni mkosaji ambaye hajakamilika, mwanafalsafa ambaye anajijua siyo mkamilifu na kila siku anakazana kuwa bora. Hapa Seneca anasema mtu anajiwekea viwango vya kuwa bora, lakini haimaanishi lazima kila wakati awe kwenye viwango hivyo. Kitendo cha kuwa na viwango na kukazana kila siku kuishi viwango hivyo, hata kama havifikii kwa asilimia 100 ni bora kuliko kutokuwa na viwango na kuishi tu kwa mazoea.

Aina ya pili ni aliye imara na mwenye kujiamini. Huyu ni mwanafalsafa ambaye anachagua kuwa tajiri kuliko kuwa ombaomba, anachagua kuvaa nguo zinazositiri mwili wake vizuri kuliko kuwa uchi. Huyu ni mwanafalsafa ambaye anajua utajiri ni kuchagua na hauna madhara yoyote kwake binafsi.

Somo kubwa nililoondoka nalo kwenye kitabu hichi ni hili; DUNIA INAPENDA KUTENGENEZA MABOKSI, KISHA KUWAWEKA WATU KWENYE MABOKSI HAYO, ukitaka kila mtu akubaliane na wewe, inabidi uingie kwenye boksi ulilotengenezewa, lakini hapo sasa hutakuwa wewe, bali utaigiza kuwa wewe.

Kwa mfano pale mtu anaposema wewe ukishakuwa mwanafalsafa basi hupaswi kujihusisha na siasa, au hupaswi kuwa tajiri, hizo sheria anakuwa ameweka nani? Hayo ndiyo maboksi ambayo dunia imeandaa ili kukufungia kwenye lolote utakalochagua.

Kama unataka kuwa na maisha yenye mafanikio makubwa, maisha bora kwako na kwa wengine, kataa kabisa kuingia kwenye boksi lolote unalolazimishwa kuingia. Ishi wewe, fanya kilicho sahihi na tumia uwezo mkubwa uliopo ndani yako. Kamwe usimsikilize yeyote anayekuambia WATU KAMA NINYI huwa hawafanyi hivi au wanafanya vile.

Na kama unakumbuka jina la kitabu hichi, UFALME ULIO MKUU, basi kuwa mfalme juu yako, tengeneza sheria za maisha yako na ishi hizo, ila tu uongozwe na falsafa sahihi kwako na wanaokuzunguka.

#2 MAKALA YA WIKI; MIAKA 30 YA MAISHA YANGU NA MAMBO 40 KUELEKEA MIAKA 40.

Mwanzoni mwa juma hili, tarehe 28/05/2018 ilikuwa siku yangu ya kuzaliwa, ambapo nimetimiza miaka 30 ya uhai wangu hapa duniani. Niliandika makala mbili muhimu sana kutokana na tukio hili, hasa la kubadili muongo wa maisha, kutoka muongo wa tatu kwenda muongo wa nne. Hizi ni makala ambazo wewe rafiki yangu unapaswa kuzisoma, na kuchagua kuziishi kama umechagua kufikia ukuu na unapenda twende pamoja.

Makala ya kwanza ni kuhusu MIMI KUJIWASHA MOTO, unaweza kuisoma hapa; Najiwasha Moto, Njoo Unione Nikiungua (Azimio La Miaka Kumi Ijayo Ya Maisha Yangu). (https://amkamtanzania.com/2018/05/29/najiwasha-moto-njoo-unione-nikiungua-azimio-la-miaka-kumi-ijayo-ya-maisha-yangu/)

Makala ya pili ni mambo 40 kuelekea miaka 40 ya maisha yangu, isome hapa; Mambo 40 Kuelekea Miaka 40 Ya Maisha Yangu (Na Vitabu Vitano Muhimu Unavyopaswa Kusoma Kwenye Maisha Yako). (https://amkamtanzania.com/2018/05/30/mambo-40-kuelekea-miaka-40-ya-maisha-yangu-na-vitabu-vitano-muhimu-unavyopaswa-kusoma-kwenye-maisha-yako/)

#3 TUONGEE PESA; MAHITAJI MATATU MUHIMU YA UTAJIRI WA MWANAFALSAFA.

Kwenye kitabu nilichokushirikisha hapo juu, kuhusu maisha ya Seneca, baada ya watu kumsema sana kwa utajiri wake, kwa kuwa pia alikuwa mwanafalsafa, Seneca alieleza mahitaji matatu muhimu ya utajiri wa mwanafalsafa.

MOJA; Utajiri usiwe tegemeo la mwanafalsafa kwenye maisha ya furaha. Hii ina maana kwamba, hata kama mwanafalsafa atapoteza utajiri wake wote alionao, maisha yake hayatabadilika kwa chochote.

MBILI; Utajiri huo upatikane kwa njia za uaminifu. Seneca anasema utajiri wa mwanafalsafa haupaswi kuwa na tone la damu ya mtu yeyote. Utajiri huo haupaswi kutokana na dhuluma au njia zisizo sahihi.

TATU; Utajiri huo uwe kwa ajili ya wengine. Kwamba utajiri ambao mwanafalsafa anaupata, siyo kwa ajili yake pekee, bali kwa ajili ya wengine pia, kuwasaidia wengine na hata kutoa huduma muhimu kwa jamii.

Hii ni misingi mitatu muhimu ambayo kila mtu anapaswa kuiishi kwenye kutafuta utajiri, hata kama siyo mwanafalsafa.

Na katika safari yangu ya kuelekea ubilionea (kama ulikuwa hujui kuhusu safari hii soma makala ya KUJIWASHA MOTO hapo juu), hii ni misingi ambayo nitakufa nayo;

Moja; Hata kama nitapoteza kila kitu, maisha yangu hayatatetereka kwa namna yoyote ile, ndiyo napigana usiku na mchana kuwa bilionea, lakini maisha yangu hayahesabiwi na fedha hizo. Nikipoteza kila kitu, lakini nipo hai, nitashukuru sana kwa uhai nilionao.

Mbili; Sitamdhulumu yeyote ili kujipatia fedha, na kama njia siyo sahihi ya kupata utajiri, sitajihusisha nayo, hata kama wengine wamenufaika nayo. Ndiyo maana nimekuwa nakataa fursa nyingi za kupata fedha haraka, lakini baadaye zina matatizo, kadhalika uwekezaji kwenye vitu vinavyoharibu afya za wengine kama pombe na sigara, nilishajiambia sitofanya, ndiyo kuna fedha, ndiyo ni halali, lakini kwa misingi yangu, kunufaika wakati wengine wanaumia siyo sahihi.

Tatu; utajiri ninaofanyia kazi, wote ni kwa ajili ya wengine. Kwa sababu sitafika peke yangu kwenye utajiri huo, nitaajiri wengine wengi, na hivyo maisha yao kuwa bora, na sehemu kubwa sana ya utajiri huo itarudi kutoa huduma muhimu kwa jamii, hasa elimu na afya, ambazo kwa upande wangu ndiyo huduma pekee zinazoweza kuiinua jamii kwa kiwango kikubwa sana.

Seneca anatuambia; popote penye binadamu, pana fursa ya kutoa.

Hivyo rafiki yangu, kuwa tajiri, lakini usiwe mtumwa wa utajiri huo, usiwe na tamaa ya kuwadhulumu wengine, na ukishapata utajiri huo, na hata kama bado hujaupata, urudishe kwenye jamii inayokuzunguka.

#4 HUDUMA NINAZOTOA; UTAJIRI HAUJAWAHI KUWA MBAYA, WATU NDIYO WABAYA.

Tano za juma hili zimekaa kitajiri tajiri sana, najua kama umejazwa zile sumu kwamba utajiri ni mbaya huenda hujasoma mpaka kufika hapa, lakini kama umefika hapa ukiwa na mashaka kwamba huyu bwana anajaribu kusema nini, maana anazungumzia sana utajiri, nina ujumbe mmoja muhimu kwako, UTAJIRI HAUJAWAHI KUWA MBAYA, WATU NDIYO WABAYA. Kuna matajiri wana roho nzuri na matajiri wenye roho mbaya, kuna masikini wenye roho nzuri na masikini wenye roho mbaya, hivyo fedha na utajiri ni kifaa tu, ubaya wanao watu.

Ukiwa bado hapa, na ukijiuliza unafikiaje utajiri wakati unakazana kila siku bila ya kuona matunda yake, niliandika kitabu kinachoitwa KWA NINI MPAKA SASA WEWE SIYO TAJIRI, Kitabu hichi kina sababu 25 zinazowazuia wengi kufikia utajiri na jinsi ya kuzivuka. Kama hujawahi kukisoma, basi kitu cha kwanza kufanya leo, unapaswa kukipata na kukisoma.

Kitabu hichi ni softcopy na kinatumwa kwa njia ya email, hivyo unaweza kukipokea popote pale ulipo. Kukipata unapaswa kulipia gharama ya shilingi elfu 5 kwa kutuma kwa namba 0755 953 887 au 0717 396 253 namba zina majina AMANI MAKIRITA, ukishatuma fedha, tuma ujumbe wenye email yako kwenda kwenye moja ya namba hizo na utatumiwa kitabu.

Chukua hatua sasa, weka juhudi ili maisha yako na wale wanaokuzunguka yawe bora, kuwa tajiri na kuwa kwa njia sahihi.

KWA NINI SIYO TAJIRI

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; KWA NINI 4 ZA KUJIULIZA ILI KUFANIKIWA.

“For true success ask yourself these four questions: Why? Why not? Why not

me? Why not now?” – James Allen

Unahitaji kujiuliza kwa nini hizi nne, kujipatia majibu na kisha kuyafanyia kazi ili uweze kufikia mafanikio makubwa sana kwenye maisha yako;

Moja; kwa nini? Hii ni kwa nini ya kwanza inayokusukuma, ni kwa nini inayohusisha uwepo wako hapa duniani. Unahitaji kujua kwa nini upo hai, na kwa nini upo hapa duniani, kisha kujipa jibu na kufanyia kazi.

Mbili; kwa nini isiwe. Hapa unajiuliza kwa nini mpaka sasa hujafika pale unapotaka kufika, hii itakusaidia kujua kile ambacho kinakuzuia na jinsi ya kukivuka.

Tatu; kwa nini isiwe mimi. Hii inakusaidia kuona kwamba unaweza kupiga hatua, maana wengine nao wameweza, kwa nini wewe usiweze.

Nne; kwa nini isiwe sasa. Kama umekuwa unapanga mambo na kuahirisha, kwa nini hii inakupa hamasa ya kuchukua hatua sasa na usisubiri tena.

Kila unapoianza siku yako, ziandike kwa nini hizo nne; kwa nini upo hai, kwa nini hujafika unakotaka, kwa nini usiwe wewe wakati wengine wameweza, na kwa nini usifanye sasa, kisha chukua hatua mara moja kupiga hatua zaidi.

Rafiki, ni imani yangu kwamba kwenye tano hizi za juma nimekupa vitu vikubwa vya kufanyia kazi, hivyo basi nichukue nafasi hii kukupa muda wa kuchukua hatua. Juma unalokwenda kuanza, juma la 23, lisiwe juma la kawaida kwako, liwe juma la kujiwasha moto na juma la kutengeneza utajiri ulio sahihi kwako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Rafiki, kama ungependa kujifunza zaidi kupitia mafunzo ninayotoa, karibu ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA. Hii ni blog maalumu inayoenda na kundi maalumu la wasap ambapo kila siku unajifunza na kuhamasika, kila wiki kuna madarasa ya mafanikio na kila mwaka kuna semina tatu nzuri sana kwa mafanikio yako.

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA tuma ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa wasap kwenda namba 0717396253 au fungua hapa;  www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog