“If you hate Mondays, it’s probably because you aren’t making enough money. People who are making BIG money like Mondays because they are winning.” – Grant Cardone.
Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari JUA LA JUMATATU…
Kuna watu ambao wanachukua muda wao na kulaumu baadhi ya siku,
Unakuta watu wanalaumu jumatatu, kwamba ni siku mbaya na inapewa kila aina ya majina.
Napenda kukuuliza swali hili muhimu kama unaichukia au umewahi kuichukia jumatatu; je jua la jumatatu huwa linachomozea upande upi wa dunia?
Unafikiri ipo tofauti yoyote kwenye kuchomoza na hata kutua kwa jua kati ya jumatatu na ijumaa?
Kwa hakika hakuna tofauti, lakini sisi wenyewe tunaongeza tofauti, kwa kuchagua kuichukia jumatatu na kuipenda ijumaa.
Kama unaichukia jumatatu, Grant Cardone anatuambia ni kwa sababu huna fedha za kutosha.
Ukiwa unatengeneza fedha za kutosha, ukiwa unashinda kila siku, basi kila siku kwako itakuwa siku nzuri, siku ya furaha, siku ya mafanikio.
Lakini kama hushindi, kama hutengenezi fedha nyingi, kama umeyakabidhi maisha yako kwa mwingine aamue ni kiasi gani cha fedha unatengeneza, jumatatu zote zitakuwa sumu kwako.
Kwa sababu uliyemkabidhi maisha yako atataka kuyatumia vizuri kila jumatatu na mapema, kufidia muda uliopumzika mwisho wa wiki.
Kama unaichukia jumatatu, au siku yoyote ya wiki, suluhisho ni kupata fedha rafiki, hakuna zaidi ya hicho.
Weka kazi kubwa na yenye thamani kwa wengine ili pia ulipwe kwa kiasi kikubwa.
Lakini pia usisubiri mpaka uwe na fedha ndiyo uchague kuzipenda siku fulani, wewe ukishaona jua limechomoza, sema “LEO NI SIKU YA KAZI” na amka uende ukafanye kazi.
Wala usitake kujua kama ni jumatatu, ijumaa au jumapili, wewe weka kazi, maana kazi ndiyo ukombozi wako.
Nakutakia siku bora sana ya leo rafiki, nenda kaipende siku hii, nenda kaweke juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora. Usisumbuke na siku, sumbuka na wewe mwenyewe.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha