Unapoenda sehemu ambayo hujawahi kwenda, na kuna njia ambayo wengine wamepita wakafika huko, na wamekuonesha njia hiyo ni ipi, lakini wakati upo njiani, akatokea mtu na kukuambia njia hiyo unayopita ni ndefu, ipo njia ya mkato, pita hapa utafika kirahisi. Je utafuata njia ndefu ya uhakika au utafuata ya mkato?
Kwa hapa unaweza kujibu kirahisi kwamba utafuata njia ndefu na sahihi uliyoelekezwa. Lakini pale unapokuwa tayari upo kwenye njia ndefu, umeshachoka na matumaini ya kufika hayapo, anapotokea mtu na kukuambia ipo njia ya mkato, utamshukuru sana na kuchukua njia hiyo.

Ni mpaka pale utakapojaribu njia hiyo, ukapotea, halafu ikakuhitaji uje kuanza tena njia iliyo ndefu upya, ndiyo utagundua kwamba njia ndefu zaidi ni njia ya mkato.
Mafanikio kwenye maisha yanafuata njia ndefu, njia inayohitaji kazi sana na muda wa kutosha ili kupata chochote unachotaka kupata. Njia ambayo inachosha na kuumiza na wakati mwingine kukatisha tamaa.
Unapokuwa kwenye njia hii ndefu, watakuja watu wengi na habari zao za njia za mkato, njia zinazoshawishi kabisa kwamba mambo yatakuwa rahisi ukichukua hatua fulani.
Lakini unapoacha njia ndefu na sahihi na kuingia kwenye njia hizi za mkato, kwanza unapoteza fedha na muhimu zaidi unapoteza muda. Hivyo utakuja uanze tena njia ndefu, huku ukiwa huna muda wa kutosha na fedha umeshapoteza pia.
SOMA; UKURASA WA 1029; Huwezi Kuukimbia Ugumu, Unaweza Kuuhamisha Kwa Muda.
Mafanikio kwenye maisha ni rahisi sana, jua nini hasa unataka kupata au kuwa kwenye maisha yako, angalia wale ambao wamefika pale kwa uhakika, angalia aina ya njia sahihi walizopita, kisha pita njia hizo na wewe.
Hakuna muujiza kwenye hilo, mpaka pale utakapoanza kutafuta urahisi ndiyo utaingia kwenye mikono ya wale ambao kushindwa kwako ndiyo faida kwao, watakushauri njia za mkato ambazo siyo sahihi na mwishowe utapoteza muda na fedha zako.
Kila mtu anapokuja kwako na njia ya mkato ya kufanikiwa, mwambie hiyo ni njia ndefu kuliko ninayotumia mimi, na sihitaji kupoteza muda na fedha zangu. Watakuambia hii ni tofauti, siyo sawa na nyingine, watakuambia unakosa fursa hii nzuri ambayo haitajirudia tena. Ukisikia kauli kama hizo, jipe uhakika kwamba siyo njia sahihi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog