Rafiki yangu mpendwa,

Karibu kwenye makala za ushauri wa changamoto zinazotuzuia kufikia mafanikio makubwa ambayo tunataka kufikia kwenye maisha yetu.

Jambo moja kuhusu changamoto ni kwamba, huwa hazikomi, hakuna chochote kinachoweza kwenda kama tulivyopanga kwa asilimia 100. Tunapanga yetu na mengine tofauti kabisa yanatokea. Hivyo lazima tujiandae kwa chochote tunachofanya, tukijua mambo yatakwenda tofauti na tulivyopanga.

Kwenye makala ya leo tunakwenda kushauriana kuhusu mambo ya kuzingatia pale unapoanzisha biashara lakini wateja hawanunui. Kabla ya kuangalia mambo hayo kwa kina, tupate ujumbe kutoka kwa msomaji mwenzetu aliyeomba ushauri kwenye hili.

Nina siku ya tatu tangu nifungue duka la nguo za kudarizi lakini sijapata mteja hata mmoja ila watu wanakuja kuuzia bei na kusifia kuwa nguo zangu ni nzuri Sana! Kutonunua kwao kunanikatisha Tamaa. – R. Robert

Kwanza kabisa hongera kwa kuanzisha biashara yako ya duka la nguo, ni hatua kubwa sana umepiga kwa kuanza tu, maana wengi huwa wanasema wataanza biashara, wanapanga kuanza biashara lakini huwa hawaanzi. Kitendo cha wewe kuanza biashara yoyote ile ni kitendo kikubwa na cha kishujaa, inaonesha una uthubutu mkubwa na una kitu ndani yako ambacho kitakuwezesha kufanikiwa zaidi.

Japokuwa kuanza biashara ni kugumu, na wachache ndiyo wanaoanza, sehemu nyingine ngumu kwenye biashara ni kuiendesha biashara hiyo kwa mafanikio. Asilimia 80 ya biashara zote zinazoanzishwa hufa ndani ya mwaka mmoja baada ya kuanzishwa. Yaani biashara nane kati ya kumi zinazoanzishwa, hazimalizi mwaka mmoja. Hizi ni takwimu za kusikitisha sana, lakini tunahitaji kuzijua ili kufanikiwa kwenye biashara.

BIASHARA NDANI YA AJIRA SOFT

Ili kufanikiwa kwenye biashara yoyote unayoanzisha, unahitaji kuzingatia mambo haya muhimu sana.

Moja; jua miezi sita ya kwanza ya biashara ni miezi migumu sana.

Mwanzoni mwa kitu chochote huwa ni pagumu, na kwenye biashara, miezi sita ya mwanzo huwa ni kipindi kigumu sana. Ni kipindi ambacho biashara inaweza kuwa inajiendesha kwa hasara na usipate faida yoyote. Wakati mwingine ugumu huu unaweza kwenda mpaka miaka miwili.

Hivyo unapoanza biashara, hakikisha umejipanga kuwa na njia nyingine ya kuendesha maisha yako na siyo kutegemea biashara hiyo pekee, hasa kwa mwanzoni. Hivyo kuwa na kitu kingine kinachokuingizia kipato, au kuwa na akiba inayoyawezesha maisha yako kwenda itakusaidia kukuza biashara yako hapo mwanzoni ambapo ni pagumu.

Mbili; siyo kila anayekuja kwenye biashara yako atanunua.

Wafanyabiashara wengi wageni huwa hawaelewi tofauti ya wateja tarajiwa na wateja halisi wa biashara. Wanaweza kupita watu wengi kwenye biashara yako, wengine wakaulizia na wengine wasiseme chochote. Siyo kila mtu anayepita kwenye biashara yako atanunua. Kuna wateja tarajiwa na wateja halisi. Unahitaji kuwa na wateja tarajiwa wengi, ili kuweza kupata wateja halisi. Kwa kila watu kumi wanaopita kwenye biashara yako, ni wawili mpaka watatu wanaoweza kuwa wateja halisi.

Hilo halimaanishi kwamba uwadharau wengine na kuona ni wasumbufu, bali ina maanisha kuwahudumia wote vizuri kama vile ni wateja ili kuweza kuwashawishi wengi zaidi kununua.

SOMA; USHAURI; Njia Tano Za Kupata Mtaji Wa Biashara Bila Ya Kuchukua Mkopo.

Tatu; jua biashara yako inawalenga watu gani hasa na wafuate kule wanakopatikana.

Kila biashara huwa kuna aina ya watu ambao inawalenga, wale ambao ndiyo wateja halisi wa biashara hiyo. Kwa zama tunazoishi sasa, kuanzisha biashara na kutegemea wateja waje kwa sababu umeanzisha ni mpango hatari sana. Unahitaji kuwafanya wateja wako wajue kuhusu uwepo wako, maana wengi hawajui hata kama upo.

Kuwa na njia z akutangaza biashara yako na kuwafikia wale wateja unaowalenga ili wajue uwepo wako, kile unachotoa na jinsi kinavyowasaidia kuwa na maisha bora kabisa.

Nne; jifunze kwa kila unachopitia na chukua hatua.

Unapoanzisha biashara, huwa unakuwa na mipango yako na matarajio yako. kadiri biashara inavyokwenda, kuna mambo utakayojifunza kwenye kufanya ambayo hukuyajua wakati unapanga na kutarajia vitu fulani. Hivyo unapoanza biashara, jua umejiandikisha kwenye darasa la kujifunza kila siku.

Angalia jinsi biashara inavyokwenda, angalia tabia za wateja, angalia vitu ambavyo wengi wanaulizia, na angalia ambavyo wengi wananunua. Kwa njia hiyo utajifunza ni vitu gani muhimu kwa wateja wako, kisha wape vitu hivyo ambavyo ni muhimu.

Usikazane tu na kile ulichopanga wewe, angalia soko linaendaje kisha nenda nalo. Kwa maana kwamba utahitaji kubadilika na kubadili baadhi ya mipango yako ya kibiashara ili kuweza kwenda vizuri na wateja wako.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; SELLING YOU (Mbinu Bora Za Mauzo Zitakazokuwezesha Kufanikiwa Kwenye Maisha Yako)

Tano; kamwe usikate tamaa, hata kama watu hawanunui.

Kosa kubwa sana ambalo wafanyabiashara wanaoanza huwa wanafanya, ni kuanza biashara kwa siku chache, wanaona watu hawanunui, wanakata tamaa a kufunga biashara. Kitu ambacho hawajui ni kwamba, wapo watu wanaona biashara hiyo ila hawanunui kwa sababu labda kwa sasa hawana uhitaji. Siku wakiwa na uhitaji wanajua wapi pa kupata wanachotaka, wanakuja kwenye biashara yako na kukuta ulishaacha kabisa.

Hatua ya kwanza kabisa ya kufanikiwa kwenye biashara ni kuwepo kwenye biashara, kuonekana kwenye biashara. Hiyo ni hatua muhimu ambayo hupaswi kuiacha kwa namna yoyote ile. Jua kila anayeulizia kitu kwako leo, anajua kuhusu uwepo wako na namna unavyoweza kumsaidia. Hata kama hanunui, lakini ataondoka akijua unafanya nini. Na ipo siku atakuwa na uhitaji na atauja kununua.

Kuwa mvumilivu na kamwe usikate tamaa. Kama umejitoa kuingia kwenye biashara, basi jitoe kupitia magumu utakayokutana nayo mwanzoni mwa biashara. Magumu hayo yatakufanya kuwa imara na kukuandaa kwa mafanikio makubwa ya baadaye.

Hakuna biashara ambayo haina changamoto, na mwanzoni mwa biashara ni kipindi ambacho changamoto ni nyingi na kubwa. Unahitaji kuwa na msingi sahihi mwanzoni mwa biashara ili uweze kuendelea na biashara yako. Mambo haya matano muhimu tuliyoshirikishana hapa, ni muhimu sana kwa ukuaji wa biashara yako.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Usomaji