Aah kocha usiniambie kuna sheria nyingine tena ambazo bado sijazijua…
Ni kweli kuna sheria nyingine za mafanikio, lakini si kweli kwamba hujazijua, ni sheria zile zile ambacho tumekuwa tunashirikishana mara kwa mara, ila zimeelezewa kwa namna tofauti.
Najua wengi hatupendi sheria, lakini bila ya sheria, za kujiwekea sisi wenyewe au za kuwekewa na wengine, maisha yatakuwa magumu sana.

Hivyo basi, bila ya kupoteza muda, twende kwenye sheria hizi nyingine tatu;
Moja; fanya mambo magumu mapema kwenye maisha yako.
Kuna mambo magumu ambayo kila mtu lazima ayafanye kwenye maisha yake. Sasa wengi huwa wanajaribu kuyakwepa wakiwa bado vijana, wakiamini wameweza kuachana nayo, wanakuja kukutana nayo wakiwa wameshazeeka au umri umekwenda na hawawezi kufanya makubwa.
Jua yale magumu unayopaswa kufanya kwenye maisha yako, na yafanye mapema, wakati bado una nguvu.
Mbili; maisha siyo tamthilia, hakuna anayekuja kukuokoa.
Tamthilia huwa ni nzuri sana, kwanza mwigizaji mkuu huwa hafi. Atateseka sana, lakini mwishoni kuna kitu kitakuja kumwokoa. Sasa ondoka kwenye tamthilia na njoo kwenye maisha yako. Wewe ndiye mwigizaji mkuu wa maisha yako, lakini hakuna anayekuja kukuokoa. Utakutana na mambo magumu sana, na kama hutapambana, utakufa.
SOMA; KURASA YA 01; Maisha Unayoishi Ni Yako.
Tatu; omba msaada, usijaribu kufanya kila kitu mwenyewe.
Huwezi kufanya kila kitu mwenyewe, na hata ungeweza, huna muda na nguvu za kukutosha kufanya kila kitu. Lakini unahitaji vitu vingi vifanyike kwenye maisha yako ili kufika pale unapotaka kufika. Hapa ndipo unapohitaji mchango na msaada wa wengine.
Usijaribu kufanya kila kitu mwenyewe, kuwa tayari kuomba msaada, na watu watakuwa tayari kukusaidia.
Sheria za ziada ni hizo tatu rafiki yangu, siyo mpya, bali zimeelezewa kwa mtazamo wa tofauti. Anza na mambo magumu, jua hakuna anayekuja kukuokoa na omba msaada.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog