Kuna makundi makuu mawili ya watu, ambapo watu wote wanaingia kwenye kundi moja au jingine.

Kundi la kwanza ni watu jasiri, watu ambao wapo tayari kuchukua hatua na kupata kile ambacho wanakitaka.

Hawa ni watu ambao kwa nje wanaonekana kama hakuna wanachohofia, wapo tayari kuchukua hatua na wanapata kila wanachokitaka. Wakati mwingine watu hawa wanaonekana kama wana bahati, maana kila wanachotaka wanakipata.

Kundi hii la watu lina watu wachache, lakini ambao wamefanya makubwa sana ukilinganisha na kundi jingine la watu.

Kundi la pili ni watu waoga, watu waliojawa na hofu, ambao wanapenda sana kuchukua hatua, lakini hawawezi. Hofu imewajaa kiasi cha kushindwa kabla hata hawajaanza. Kundi hili, wanaonekana kama hawajui wanachotaka, na kama hawana bahati. Maana kila wanapoonekana kutaka kitu, kuna jambo haliendi sawa na hivyo kushindwa kuchukua hatua.

Sasa wengi hufikiri kwamba kinachowatofautisha watu kwenye makundi haya mawili ni hofu, kwamba wale jasiri hawana hofu na wale waoga wana hofu. Ukweli ni kwamba watu wote wana hofu, ila watu jasiri wanachagua kuchukua hatua licha ya kuwa na hofu. Huku watu waoga wakikubali hofu ziwazuie kuchukua hatua.

SOMA; UKURASA WA 1084; Tiba Kamili Ya Hofu Ya Kukataliwa…

Hii ina maana kwamba, kila mtu anaweza kuchagua kuwa jasiri, kila mtu anaweza kuchagua kuchukua hatua, licha ya kuwa na hofu. Maana hofu hazitakoma kabisa kwenye maisha yetu, ila tunapochukua hatua, tukijua kwamba hofu haitaondoka, tunaifanya hofu isiwe kikwazo kwenye mafanikio yetu.

Majasiri wanakuwa washindi, wanaangusha kila aina ya kikwazo na kupata chochote kile wanachotaka.

Waoga wanateseka na kufa, siyo tu kifo cha mwili, bali kifo cha kiroho, kifo cha matumaini na maisha yanakuwa kama gereza kubwa ambalo hawawezi kutoka.

Ni swala la wewe kuchagua, unataka kuwa shujaa kwa kuanza kuchukua hatua sasa, au unataka kuwa mwoga kwa kukubali hofu ikuzuie kuchukua hatua. Tafadhali chagua wewe mwenyewe na usije kupeleka lawama zako kwa mtu mwingine yeyote, hata kama amefanya nini.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog