Rafiki yangu mpendwa,

Juma namba 23 linakwisha kama lilivyoanza, ila nina imani kubwa kwamba halijakuacha kama lilivyokukuta.

Kama umekuwa rafiki mwaminifu kwangu, na kama umechagua tu kufanyia kazi machache kati ya mengi ninayokushirikisha kila siku ya juma, basi najua ulipo leo siyo sawa na ulipokuwa wakati juma hili linaanza.

Hata kama hujaanza kuona matokeo mazuri, lakini nina imani mtazamo na fikra ulizonazo ni tofauti kabisa, na ni swala la muda tu kabla matokeo mazuri hayajaanza kuonekana.

Hiyo pia ni kukuambia, usitegemee matokeo ya papo kwa hapo, kwamba kwa kujifunza leo na kuchukua hatua leo basi matokeo ni leo leo, au hata kesho. Matokeo yanachukua muda, na si wote tunajua methali inayosema mambo mazuri hayataki haraka?

Karibu tena rafiki yangu kwenye TANO ZA JUMA, mkusanyiko wa sindano tano za moto sana, zinazokwenda kutibu eneo moja muhimu sana kwenye maisha yetu, ambalo ni fikra zetu. Eneo hili linahitaji matibabu ya mwendelezo na ya kila siku, la sivyo mtu anapata utapiamlo wa fikra na akili na kudumaa kimaendeleo pale alipo.

Juma hili nimekukusanyia haya matano muhimu, yasome, yatafakari, angalia maisha yako na unapokwenda, kisha panga kuchukua hatua na anza kuzichukua leo, maana ulipaswa kuwa unazichukua jana, hivyo ukizichukua leo utakuwa hujachelewa sana kama utakavyojidanganya utafanya kesho.

#1 KITABU NILICHOSOMA; SIRI ZA MATAJIRI.

Juma hili nimepata nafasi ya kusoma vitabu vingi kidogo, na haya yamekuwa matunda ya program nzuri ya kusoma vitabu niliyoanza kuitumia. Kama upo kwenye KISIMA CHA MAARIFA au kundi la KURASA KUMI ZA KITABU, nimeshirikisha program hiyo, unaweza kuitumia pia.

Moja ya vitabu nilivyosoma ni THE MILLIONAIRE’S SECRETS; LIFE LESSONS IN WISDOM AND WEALTH ambacho kimeandikwa na Mark Fisher. Kitabu hichi ni hadithi inayoelezea safari ya mafanikio ya kijana ambaye alianzia kwenye umasikini mpaka kwenye utajiri. Ni hadithi iliyojaa visa vya kufunza na kutahadharisha kwenye safari yoyote ya mafanikio ambayo mtu anachagua kuchukua.

siri za utajiri

Nikushirikishe hadithi hii kwa kifupi kisha mwisho nikupe hatua muhimu za kuchukua ili kufika kwenye utajiri mkubwa.

Alikuwepo kijana anaitwa John ambaye alikuwa ameajiriwa kwenye kampuni inayojihusisha na matangazo, yeye akiwa kama mwandaaji wa matangazo. Alikuwa na kipaji kikubwa cha ubunifu na matangazo mengi aliyobuni yaliweza kuuza sana. Lakini shida ilikuwa kwamba hakupenda kazi hiyo, alipenda zaidi kuwa mwandishi wa simulizi za tamthilia. Kazi yake haikuwa inamlipa vizuri, kipato kilikuwa kidogo, alikuwa na madeni na maisha yalikuwa magumu. Kila wakati alikuwa anasema ataacha kazi na akajiajiri kwenye uandishi wa simulizi lakini hakuweza kufanya hivyo, hakuwa na uwezo wa kuishi bila kazi.

Ilifika wakati mambo yakawa magumu zaidi, kazi nyingi na fedha haitoshi. Aliamua kwenda kwa mjomba wake kuomba ushauri na hata msaada wa kifedha ili aweze kufanya kile anachopenda. Alipofika kwa mjomba wake alimsikiliza kisha akamwambia sina kikubwa cha kukusaidia, na fedha siwezi kukupa, ila nitakupa mawasiliano ya milionea mmoja, mtafute na atakusaidia.

Kijana alichukua mawasiliano ya milionea na kuanza safari ya kwenda kumtafuta. Alipofika nyumbani kwa milionea yule, nyumba ya kifahari na iliyozungukwa na bustani nzuri, alikutana na msaidizi wake ambaye alimwambia amsubiri milionea huyo. Akiwa kwenye bustani, alitokea mzee wa makamo, ambaye alimwuliza kijana anahitaji nini, akajibu amekuja kuonana na milionea. Mzee yule ambaye hakuonekana kama ni milionea, alikuja kugundua ndiyo tajiri mwenyewe.

Basi alimweleza kwa kina hali yake ya maisha, milionea alimsikiliza, kisha akamwambia kama kwa umri wake (miaka 32) hajaweza kuwa na uhuru wa kifedha, ni kwa sababu hajajua sheria na siri za utajiri au kama anazijua basi anazipuuza. Basi alimuuliza kijana yule nini anataka kufanya na maisha yake. Akajibu anataka kuwa mwandishi wa simulizi, mwenye mafanikio makubwa. Akamwuliza kwa nini mpaka sasa hajawa, akajibu kwa sababu hana uhuru wa kufanya hivyo, hawezi kuishi bila kazi.

Waliongea na kupanga mengi, mwishowe milionea yule akampa kiasi cha fedha, kama cha kuanzia, akampa na siri muhimu za utajiri, ikiwepo kujua nini hasa anataka, na kutokukubali chochote kimzuie. Kijana aliondoka akiwa amejiamini, akaenda kazini kwake na kumwambia mwajiri anaacha kazi. Mwajiri akamwambia hakuna anayeacha kazi kwake asirudi kuomba tena kazi, lakini yeye hakusikiliza.

Mara moja alikwenda kuanzisha kampuni yake ya matangazo, akifikiria kufanya matangazo ili yamlipe fedha ya kuendesha maisha, wakati huo aendelee kuandika simulizi kitu ambacho ndiyo ndoto ya maisha yake. Kampuni ilianza, lakini miezi ilienda na hakuweza kupata kazi yoyote. Fedha alizopewa na milionea zilikuwa zinakaribia kuisha na hakukuwa na tumaini lolote la kupata kazi ya kuweza kumpa mapato ya kuendesha maisha yake. Wakati huo huo alikuwa ameanzisha mahusiano ya kimapenzi na binti ambaye alikutana naye kupitia kazi yake. Maisha yalikuwa magumu kiasi kwamba alifikiria kurudi kuomba kazi kwenye kampuni aliyoacha kazi. Alilaumu kwamba milionea alimpa siri ambazo hazifanyi kazi, na aliamua kuachana nazo.

Akiwa kwenye kukata tamaa, na akiwa hajui afanye nini na maisha yake, alikutana tena na milionea yule, ambapo alipata nafasi ya kuongea naye tena. Alimweleza kila alichofanya na kila kilichotokea, milionea alimsikiliza kwa makini, na kumwuliza swali moja, unataka kiasi gani cha fedha kwenye kazi yako ya simulizi? Kijana akawa hana uhakika. Akamfundisha jinsi ya kuweka malengo, ya kiasi cha fedha anachotaka na muda wa kukipata. Lengo aliloweka ni kupata milioni moja kwa kuuza kisa cha tamthilia.

Pia milionea alimuuliza kijana swali moja, kama yupo tayari kutoa kafara ili apate kile alichotaka, kijana alimwambia yupo tayari. Akamwambia kafara itakuwa kubwa, akajibu atakuwa tayari kuitoa.

Basi kijana aliondoka kwenye mkutano ule na milionea akiwa na hamasa kubwa sana ya kwenda kutekeleza yale aliyojifunza. Alikuwa na lengo lake ambalo aliliandika kila siku na kuanza kuandika simulizi yake ya kwanza, kwa muda ambao ni wa ziada, lakini muda mwingi akawa ameweka kwenye kampuni yake ya matangazo. Hata baada ya hamasa ile, bado mambo hayakubadilika, bado hakupata wateja wa matangazo, na kisa alichoandika, alipokipeleka kwa rafiki yake ambaye alikuwa mtu wa tamthilia, alimweleza ukweli kwamba kisa kile hakikuwa na mvuto.

Fedha kidogo alizokuwa amebaki nazo zilikuwa zinaisha na hana tegemeo la kupata fedha haraka, alianza kukata tena tamaa, na wakati huo huo akaanza kukosa nguvu ya miguu, alipopimwa hospitali, aligundulika kuwa na ugonjwa wa uti wa mgongo, na hivyo asingeweza kutembea tena, angetumia kiti cha kutembelea. Hilo lilimkatisha tamaa zaidi, kwamba licha ya maisha kuwa magumu, sasa atakuwa kilema anayetembea kwa kiti. Baada ya kugundulika kuwa na ugonjwa huo, na kujua kwamba hataweza kutembea, alifanya maamuzi magumu, kwanza aliachana na mpenzi wake, na pili alifunga kampuni yake ya matangazo.

Alibaki na kitu kimoja pekee, ambacho ndiyo kingemsimamisha au kumzamisha, aliweka nguvu zake na muda wake wote kwenye kuandika kisa cha tamthilia. Na aliweka lengo la kuuza kisa hicho kwa malipo ya dola robo milioni. Toleo la pili la kisa hicho bado halikuwa zuri, alirudi tena kuandika toleo la tatu, ambalo lilikuwa zuri. Katika kipindi hichi, hakukubali kabisa kushindwa au kukata tamaa. Baada ya kukamilisha toleo la tatu, ambalo rafiki yake alikubali ni toleo bora, alilituma kwenye makampuni yanayoandaa tamthilia, akijua watakigombania kisa kile na kumlipa fedha nyingi. Hakupokea simu hata moja au kutafutwa. Hili lilimfanya aanze kukata tamaa na kuona mafunzo ya milionea siyo ya kweli.

Aliendelea kutuma kisa kile kwa makampuni mengi zaidi, na kurudia kutuma kwenye makampuni ambayo alishatuma tena awali. Kampuni moja ilimwita kwa ajili ya kupata naye, na kwa kutumia mbinu alizojifunza kutoka kwa milionea, aliweza kuuza kisa kile siyo kwa robo milioni, bali kwa nusu milioni.

Baada ya kukamilisha mauzo yale, alirudi kwa milionea akiwa na furaha kwamba ameweza kupata kile alichotaka, milionea akampongeza na kumwambia hiyo ndiyo faida ya kutoa kafara. Kijana akastuka, ni kafara gani nimetoa, aliuliza. Milionea akamjibu, huo ugonjwa wa kushindwa kutembea uliopata, ni mimi nilikusababishia, kuna dawa nilikuwekea kwenye kinywaji ambayo ilisababisha usiweze kutembea. Kwa sababu nilijua bila ya kuwa na kitu kinachokuzuia, utaendelea kupoteza muda wako na vitu vingi ambavyo havitakulipa. Lakini unapouwa na kitu cha kukuzuia, unapojua huna namna nyingine basi unaweka nguvu zako zote kwenye kitu kimoja.

Kijana pamoja na furaha aliyokuwa nayo, alimkasirikia milionea na kumwambia kwa hiyo umeharibu maisha yangu kwa sababu ya umilionea? Milionea akamwambia ulijibu mwenyewe kwamba upo tayari kutoa kafara yoyote.

Mwishoni kijana aliweza kutembea tena kupitia siri za milionea yule na pia aliweza kurudiana na mchumba wake ambaye waliishi kwa furaha.

Ni kisa ambacho kinaendana na maisha halisi ya kila siku, maisha yaliyojaa kila aina ya changamoto, maisha ambayo wewe unapanga lakini yanayotokea ni tofauti.

Siri muhimu sana za kuondoka nazo kwenye kitabu hichi;

 1. Hofu ndiyo inawazuia wengi kuchukua hatua.
 2. Unahitaji kujua nini hasa unataka ili uweze kukipata.
 3. Ili upate kitu ambacho hujawahi kupata, unahitaji kufanya vitu ambavyo hujawahi kufanya.
 4. Kinachokuzuia kupata unachotaka, ni vile vitu ambavyo kwa sasa unavyo, unahitaji kupoteza baadhi ya vitu ili uweze kupata makubwa zaidi.
 5. Utashindwa kwenye mambo mengi utakayopanga kufanya, uvumilivu na ung’ang’anizi ni muhimu.
 6. Dunia inakupa kile unachotaka, na kile unachopata kwenye maisha yako, ni matokeo ya mawazo uliyonayo.
 7. Mara zote ishi kwa kanuni kuu; wafanyie wengine kile ambacho ungependa wakufanyie. Na ili ufanikiwe zaidi, piga hatua kwenye kanuni hiyo; usifanye chochote kwa ajili yako, fanya kila kitu kwa ajili ya wengine.
 8. Unaweza kutajirika kwa kufanya chochote, unachohitaji ni kujua wapi hasa unataka kufika, kujua watu gani unaoweza kuwasaidia na kufanya hivyo bila ya kuacha.
 9. Jamii inakujaza mawazo hasi na ya uongo, ili kufanikiwa unahitaji kutua mawazo yote yanayokuzuia kufanikiwa ambayo jamii imekupandikizia.
 10. Kushindwa ni darasa muhimu kwako, kila unaposhindwa unajifunza kipi ambacho siyo sahihi kufanya na kipi sahihi kufanya. Unaposhindwa mapema na kushindwa mara nyingi, inakupa nafasi kubwa ya kufanikiwa.

Pata kitabu hichi na ukisome, yapo mengi sana utakayojifunza kuhusu maisha na mafanikio.

095a5b996f7db11bfe3b1d93a17b444b.0

#2 MAKALA YA WIKI; NJIA TANO ZA KUKUZA BIASHARA YAKO.

Zama tunazoishi sasa, ni zama ambazo kila mtu anapaswa kwa na biashara. Lakini pia ni zama hatari kuingia kwenye biashara, kwa sababu ushindani ni mkali na kelele ni nyingi. Mpaka umfikie mteja wako, au mteja ajue ulipo, inakuchukua kazi kubwa.

Biashara nyingi zinakua, na nyingine zimedumaa. Ni biashara chache sana ambazo zinajiendesha kwa faida.

Kama sehemu ya KISIMA CHA MAARIFA, mwezi julai mwaka huu 2018 tutakuwa na semina ya biashara, ambapo tutajifunza njia 5 za kukuza biashara yako, ambapo utajifunza mbinu za kuongeza faida kwenye biashara yako kwa zaidi ya asilimia 50.

Soma hapa kujua zaidi kuhusu semina hii; SEMINA; NJIA TANO ZA KUKUZA BIASHARA YAKO, Ongeza Faida Kwa Zaidi Ya Asilimia 50 Ndani Ya Mwaka Mmoja. (https://amkamtanzania.com/2018/06/04/semina-njia-tano-za-kukuza-biashara-yako-ongeza-faida-kwa-zaidi-ya-asilimia-50-ndani-ya-mwaka-mmoja/)

NYONGEZA; Kwa wale ambao wapo njia panda kuhusu kuajiriwa au kufanya biashara, nina kisa kifupi hapa ambacho kitakuwezesha kufanya maamuzi muhimu ya maisha yako; Huo mnyororo shingoni kazi yake nini? (gharama ya uhuru unayopaswa kulipa ili kufanikiwa). (https://amkamtanzania.com/2018/06/07/huo-mnyororo-shingoni-kazi-yake-nini-gharama-ya-uhuru-unayopaswa-kulipa-ili-kufanikiwa/)

#3 TUONGEE PESA; UPO TAYARI KUTOA NINI KAFARA?

Rafiki, kama tulivyoona kwenye kitabu nilichokushirikisha, ili upate fedha na utajiri, kuna kafara unahitaji kutoa. Na ninaposema kafara usipate picha zile za wajinga wanaofikiria unahitaji kuua mtu au kuchinja wanyama kama kafara ya mafanikio. Hayo yanafanywa na wajinga wasioijua misingi sahihi ya mafanikio.

Kwa msingi wa mafanikio iko hivi rafiki yangu, kila mtu pale alipo, kuna kitu anakipenda sana, ambacho ndiyo kinamzuia kufanikiwa. Kama hatakuwa tayari kuachana na kitu hicho, hataweza kufanikiwa, hata angefanya nini.

Inawezekana mtu ana kazi ambayo anaiona ndiyo njia pekee ya kuendesha maisha yake.

Huenda mtu ana marafiki ambao kila wakikutana ni kunywa pombe au kubishana mambo fulani.

Inawezekana una ushabiki mkubwa wa michezo au siasa au dini au vitu vingine, kiasi kwamba muda wako mwingi unautumia kwenye mambo hayo kuliko kwenye kufanya kazi zinazozalisha.

Inawezekana mtu unapenda sana usingizi, unapenda kulala unavyotaka, mpaka usingizi uishe wenyewe.

Huenda mtu una mahusiano ambayo yamekubeba mzima mzima, huwezi kufikiria kitu kingine nje ya mahusiano hayo.

Hii ni mifano ya vitu ambavyo vinakuzuia kufanikiwa, lakini wewe unaweza kuwa navyo vingi zaidi.

Zoezi la kutoa kafara kwako.

Kaa chini na yatafakari maisha yako, angalia ni vitu gani huwa unapenda kuvifanya kila siku, viorodheshe vitu hivyo vyote bila ya kuacha hata kimoja. Pia orodhesha vile vitu ambavyo unaamini huwezi kuishi bila ya kuwa navyo.

Kwenye orodha ya vile vitu ambavyo unapenda kufanya, anza na kimoja kimoja, jiulize je kinakuingizia fedha nyingi inayoweza kukupeleka kwenye utajiri? kama jibu ni hapana, mbele yake andika ONDOA. Fanya hivyo kwenye orodha nzima, kisha baki na vile ambavyo unapenda kuvifanya kweli na vinakuingizia kipato kikubwa.

Kwenye orodha ya pili, kwenye vitu ambavyo umejiambia huwezi kuishi bila ya kuwa navyo, jiulize tena kwa mara nyingine, je maisha yako yalikuwaje kabla ya kuwa na vitu hivyo. Kisha fanya zoezi la kuacha kwa muda kila ulichojiambia huwezi kuishi bila ya kuwa nacho. Kama ni kazi, jaribu kuishi kama huna kazi, hata kwa mwezi mmoja, fanya kazi yako, lakini usitumie kipato chochote kutoka kwenye kazi yako na uone je maisha yanaweza kwenda bila ya kuwa na kipato cha kazi?

Na ninachoweza kukuhakikishia ni hichi, ukiondoa pumzi unayovuta kila siku, hakuna kingine chochote ambacho huwezi kuishi bila kuwa nacho. Kila kitu unaweza kukiacha na maisha yako yakaendelea vizuri tu.

Hivyo chagua vitu utakavyovitoa kafara kwenye maisha yako, ili akili zako na nguvu zako uzielekeze kwenye maeneo machache muhimu. Na kumbuka kufanya hivyo hakumaanishi mafanikio yatakuwa rahisi, bado utakutana na vikwazo, lakini kama umejitoa kweli, kumbuka kile ninachokuambiaga, kama wewe hutakimbia, ugumu unaokutana nao utakimbia.

Unatoa kafara nini kwenye maisha yako? Unaweza kunishirikisha ili nikufuatilie kwa karibu kama kweli utafanya. Nitumie kwenye email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Baadhi ya vitu ambavyo kama unafanya nakushauri uache mara moja, kama kweli umejitoa kufanikiwa;

 1. Kama unatumia kilevi cha aina yoyote ile, kiache mara moja, mara moja, wala hata usianze kujiuliza nitaachaje wakati nimeshazoea. ACHA. Ni hivyo tu.
 2. Kama unatumia muda wa siku yako kufuatilia habari au mambo ya wengine, ACHA.
 3. Kama unatumia muda wako kwenye mitandao ya kijamii, lakini hakuna fedha unayoingiza, ACHA.
 4. Kama upo kwenye mahusiano ambayo kila siku ni changamoto, yanakuvuruga, huwezi kutulia na ukaweka akili na nguvu zako kwenye kile unachotaka, ONDOKA.
 5. Kama upo kwenye ajira ambayo umekuwepo kwa muda mrefu, lakini hakuna unachoweza kuhesabu, kipato hakikutoshelezi, una madeni na hufurahii unachofanya, anza sasa kuishi kimaandalizi bila ya kazi hiyo.

Rafiki, chukua hatua kwenye baadhi ya vitu unavyopenda, ili ubaki na uhuru wa kufanya yale ambayo ni muhimu zaidi kwako.

#4 HUDUMA; SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA.

Moja ya manufaa ya kuwa kwenye KUNDI PEKEE la mafunzo ninaloendesha kwenye mtandao wa wasap, KISIMA CHA MAARIFA, ni kushiriki semina tatu kwa mwaka. Semina mbili zinakuwa kwa njia ya mtandao, na semina moja inakuwa kukutana kwa pamoja.

Tunaelekea kwenye semina yetu ya pili kwa mwaka huu 2018 ambayo itakuwa semina ya kujifunza njia za kukuza biashara. Moja ya mahitaji ya kuwa mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA ni kuwa na biashara. Hivyo kama umekuwa unafikiria kuingia kwenye biashara lakini huchukui hatua, au unaingia na kushindwa na hujawa kwenye KISIMA CHA MAARIFA, hayo yote unayokutana nayo umejitakia mwenyewe.

Nakukaribisha leo rafiki yangu, ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA, upate maarifa sahihi ambayo kwa kuyafanyia kazi maisha yako yatakuwa bora. Ninayaamini sana maarifa haya, na ninaamini sana nguvu ya wapenda maarifa wanaokutana pamoja kiasi kwamba nipo tayari upate hayo yote bure.

Hivyo ninachokuambia ni hichi, jiunge na KISIMA CHA MAARIFA, kwa kutafuta ada uwezavyo, iwe hata kwa kuuza kile unachopenda kweli. Halafu kaa mwaka mmoja, jifunze yale yote yanayoshirikishwa, yafanyie kazi, halafu unapomaliza mwaka mmoja, jifanyie tathmini, je mwaka mmoja wa kukaa kwenye KISIMA CHA MAARIFA umekuwa na manufaa kwako. Kama jibu ni hapana niandikie, kwamba umekaa kwenye KISIMA CHA MAARIFA na hujapata manufaa, sitakuuliza swali lolote lile, bali nitakachofanya ni kukurejeshea ada uliyolipa.

Karibu rafiki tujifunze, kama upo nje ya KISIMA CHA MAARIFA, ni sawa na umejiweka mwituni, ambapo ni hatari sana kwako, wakati ipo sehemu salama ya wewe kuwepo.

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA, niandikie ujumbe kwa njia ya wasap wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA na utume kwa namba 0717 396 253, tuma ujumbe kwa wasap tu.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; NENO LINALOPATIKANA KWENYE KAMUSI YA WAPUMBAVU PEKEE.

“Impossible is a word to be found only in the dictionary of fools.” – Napoleon Bonaparte

HAIWEZEKANI ni neno ambalo linapatikana kwenye kamusi ya wapumbavu pekee.

Wakati Thomas Edson anatengeneza taa ya umeme, wapumbavu walimwambia HAIWEZEKANI, akashindwa zaidi ya mara elfu kumi, lakini hakukata tamaa na sasa tunaweza kufanya kazi usiku na mchana, kwa sababu hakuwasikiliza wapumbavu.

Wakati Hendry Ford anataka silinda nane zikae kwenye pistoni moja ili kupata gari yenye nguvu kubwa, wapumbavu walimwambia HAIWEZEKANI, hakuwasikiliza wapumbavu na leo tuna ma-V8 ambavyo ni magari bora kabisa.

Wakati Steve Jobs anasema atatengeneza simu isiyo na kitufe, yenye kioo kizuri ambacho mtu atatamani kukilamba, wapumbavu walimwambia HAIWEZEKANI, lakini alifanya hivyo na leo simu karibu zote tunazotumia hazina vitufe, ni kupapasa tu vioo.

Wakati Wright Brothers wanasema watarusha chombo cha usafiri angani wapumbavu waliwaambia HAIWEZEKANI, lakini waliendelea kujaribu na leo hii tuna ndege za kusafiri, kutoka bara moja kwenda jingine ndani ya masaa na siyo miezi kama ilivyokuwa wakati wa kutegemea meli.

Utakapowaambia watu kuhusu ndoto yako, utakapoanza kuchukua hatua kubwa ili kufanikiwa, wapumbavu watakuambia HAIWEZEKANI. Sasa hapo kazi ni kwako, kama utajisikiliza wewe unayetaka, au utawasikiliza wapumbavu.

Imani yangu ni kwamba utajisikiliza wewe na utaachana na wapumbavu. Hivyo basi rafiki yangu mpendwa, yeyote anayekuambia HAIWEZEKANI, jiambie kimoyomoyo, mpumbavu mwingine huyu hapa, ngoja nimwache na upumbavu wake na nifanye yangu.

Kumbuka, usibishane na mpumbavu, labda kama na wewe unataka kuwa mpumbavu. Mtu anakuambia haiwezekani, mpuuze na wewe fanya. Ukikutana na ugumu jifunze, na chukua hatua. Watakucheka kwa muda wakati unapitia magumu na kushindwa, lakini mwisho wa siku wewe utacheka zaidi na utacheka milele, huku wapumbavu wakiteseka na mzigo wao wa upumbavu.

Juma namba 24 likawe juma bora sana kwako rafiki, na nenda kampambane, wapumbavu wasikubabaishe kwa lolote.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Rafiki, kama ungependa kujifunza zaidi kupitia mafunzo ninayotoa, karibu ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA. Hii ni blog maalumu inayoenda na kundi maalumu la wasap ambapo kila siku unajifunza na kuhamasika, kila wiki kuna madarasa ya mafanikio na kila mwaka kuna semina tatu nzuri sana kwa mafanikio yako.

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA tuma ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa wasap kwenda namba 0717396253 au fungua hapa;  www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Usomaji