Yapo magonjwa ya kuambukizwa, ambayo ni hatari sana, ambayo yanasambaa kwa kasi na kuua wengi. Njia pekee ya kukabiliana na magonjwa ya aina hii huwa ni kuweka karantini wagonjwa au wasio wagonjwa. Unaondoka kila namna ya ugonjwa kuweza kusambaa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine.

Yapo maeneo ya maisha yako ambayo ni hatari sana kwa maambukizi. Mafanikio kwenye maisha yetu ni maambukizi, na kushindwa pia kunasambaa kwa kuambukizwa. Kadhalika hofu huwa inasambaa kwa kuambukizwa. Umewahi kukaa na mtu na baada ya dakika chache ukajisikia una hamasa kubwa na unaweza kufanya chochote unachotaka? Je umewahi kukaa na mtu na baada ya muda mfupi unajisikia kukata tamaa na kama huwezi chochote? Hayo ndiyo maambukizi ninayokuambia hapa.

Walioshindwa

Sasa ili kujikinga na maambukizi mabaya, maambukizi ya hofu na kushindwa, na kujiweka kwenye maambukizi mazuri, maambukizi ya hamasa na mafanikio, unahitaji kujiwekea karantini.

Unahitaji kuweka viwango kwenye kila unachofanya na kujihusisha nacho. Unahitaji kuweka viwango kwa watu, na kujihusisha na watu wa viwango vya juu, huku ukiepuka wale wa viwango vya chini. Watu wa viwango vya juu ni wale wanaopiga hatua na wana matumaini ya kufanikiwa zaidi. Watu wa viwango vya chini ni wale walioshindwa, wamekata tamaa na wanajisifia kwa hili.

SOMA; UKURASA WA 1005; Usishushe Viwango Vyako…

Weka viwango pia kwenye maarifa na taarifa unazoruhusu ziingie kwenye akili yako. Maarifa au taarifa yoyote iliyobeba uhasi ndani yake ni ya viwango vya chini, achana nayo mara moja. Maarifa na taarifa zenye uchanya, zenye matumaini na hamasa ni za viwango vya juu, jihusishe nazo.

Jiwekee viwango kwenye kila unachofanya na kujihusisha nacho, na kamwe usikubali kujihusisha na vile vilivyo chini ya kiwango. Utaambukizwa viwango vya chini na utashindwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog