Wanachofanya wengi, ni kusimamia vitu, kuvitumia kwa njia ambayo inafaa.

Angalia watu wanachofanya kwenye biashara zao, wanachofanya kwenye muda wao, wanachofanya kwenye fedha zao na kwenye mambo mengine wanayofanya. Wanasimamia, wanafanya kile ambacho kinafaa kufanywa, kwa namba ambayo wamezoea kufanya.

Lakini hivi sivyo watu wenye mafanikio makubwa wanavyofanya.

wp-image--1427239600

Wenye mafanikio makubwa hawasimamii vitu, bali wanadhibiti, wanavitawala. Wanafanya kile kinachopaswa kufanywa, iwe wanapenda kufanya au la, iwe kila mtu anafanya au la, na hawafanyi chochote kwa mazoea.

Unapodhibiti biashara yako, maana yake unajua kila kinachoendelea kwenye biashara yako, unajua kila eneo la biashara yako, na unachukua hatua sahihi pale mambo yanapoanza kubadilika, kabla hata matokeo ya mabadiliko hayajaanza kuonekana. Unapodhibiti biashara yako hutoi sababu za hovyo kwa nini imeshindwa au kwa nini hupati faida. Badala yake unamiliki kila kinachohusiana na biashara yako, na matokeo unayopata unayamiliki na kuyafanyia kazi.

SOMA; UKURASA WA 763; Hakikisha Watu Wanafanya Kile Wanachopaswa Kufanya….

Unapodhibiti muda wako, unafanya yale ambayo ni muhimu zaidi kwenye muda huo. Hupotezi muda kwenye chochote ambacho hakichangii kwenye mafanikio yako, hata kama kila mtu anafanya. Unapotawala muda wako, huanzi kupangilia kwamba unahitaji kuwa na mlinganyo, badala yake unafanya kile ambacho kinapaswa kufanywa, na hicho pekee ndiyo kinapaswa kuchukua muda wako.

Unapodhibiti fedha zako, unajua kila senti yako iko wapi, unajua kwa hakika kila njia unayoitumia kuingiza kipato, na hujaribu hata kidogo kuweka fedha zako kwenye mambo usiyoyajua kwa kina. Unalinda sana fedha zako na unahakikisha chochote unachofanya hupotezi fedha. Na fedha inakuwa kipaumbele muhimu kwenye maisha yako.

Chochote unachofanya, usisimamie tu, bali kidhibiti, tawala.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog