Rafiki yangu mpendwa,

Binadamu ni viumbe wa ajabu sana.

Ni viumbe ambao huwa hawapendi kuona wengine wakifanya kile ambacho wao hawawezi kufanya.

Na hivyo anapotokea mtu, akaanza kufanya kile ambacho wengine hawawezi kufanya, wanatafuta njia ya kumfanya asiweze kuendelea. Na hapo ndipo ukatishaji tamaa na kupinga kunapoanzia.

Na kama mtu huyo hatasikia kile anachoambiwa, kwamba haiwezekani au hawezi, basi wanamalizia na silaha ya mwisho waliyonayo, wanamchukia.

MIMI NI MSHINDI

Kama umeanza kuishi maisha ya mafanikio, kama umeanza kuchukua hatua kuyaboresha zaidi maisha yako utakuwa umeshakutana na hali hii.

Ulikuwa na rafiki zako na hata ndugu ambao mlikuwa mnapendana, mnakubaliana kwa kila jambo na wote mnalalamika maisha ni magumu. Lakini wewe unapoanza kuchukua hatua, unapokataa kwamba maisha siyo magumu bali wewe ndiyo laini, unapopunguza muda wa kulalamika nao na ukafanya kazi, wanaanza kusema una dharau, siku hizi unajisikia, unajiona ni bora kuliko wao. Wanasema unachofanya kitashindwa, au hutafika mbali, au utarudi tu. Na wakiona bado unaendelea licha ya maneno yao, basi wanakuchukia kabisa. Na wengine wataenda mbali zaidi kuhakikisha wanakuzuia usipige hatua, hapa ndipo watakuwekea vikwazo, ili ushindwe kufanya unachotaka kufanya.

SOMA; Hatua Tatu Za Kuchukua Pale Unapokatishwa Tamaa Na Watu Wa Karibu Kwako.

Rafiki yangu, leo nakuandikia hili muhimu sana kwa sababu nimeona baadhi ya watu wanakata tamaa na kurudi nyuma pale ambapo wale wanaowazunguka wanawageuka. Pale ambapo mzazi anamwambia kijana wake asijisumbue na mambo magumu. Pale mtu anapoanza biashara kwenye eneo lake la kazi na wafanyakazi wenzake wanamtengenezea majungu ili biashara hiyo ifungwe.

Rafiki, ikiwa kuna watu wanakupinga, wanakukatisha tamaa na hata kukuchukia kwa sababu ya hatua kubwa unazopiga kwenye maisha yako, unapaswa kufurahi sana, kwa sababu ni faida kubwa kwako. Usiumie na kuona ni hasara, au kuona unawapoteza watu muhimu, bali furahi sana kwa sababu;

Wale wanaokupinga na kukuchukia kwa sababu unachukua hatua ya kuyafanya maisha yako kuwa bora wanajieleza wazi kwamba hawapo upande wako, na hivyo utaacha kabisa kuwategemea. Huenda mwanzoni ulijua unaweza kuwategemea na wakakusaidia, lakini wanakuwa wamekueleza wazi kwamba siyo watu wa kutegemewa, hivyo unakuwa unajua wazi nani anafaa na nani hafai.

Kuwa na watu wanaokupinga na kukuchukia ni kiashiria kwamba unafanya makubwa kwenye maisha yako. Kama kila mtu anakubaliana na wewe, kama hakuna anayekupinga, kama hakuna anayekuchukia, hakuna unachofanya kwenye maisha yako, unafanya vitu vya kawaida sana, ambavyo kila mtu anafanya, hivyo hakuna anayestuka kwamba unaweza kuwa hatari kwao. Kama hakuna anayekuchukia, basi bado hujawa hatari kwa mtu yeyote. Kadiri wengi wanavyokupinga na kukuchukia, ndivyo unavyokuwa unafanya makubwa sana kwenye maisha yako. Na kusudi lako halipaswi kuwa kuwafanya wale wanaokuchukia wakupende, bali unahitaji kuwaumiza zaidi, kwa kufanikiwa zaidi.

Faida nyingine ya kuwa na wanaokupinga na kukuchukia ni kutumia chuki zao kama nishati ya wewe kusonga mbele zaidi. Kadiri wengi wanavyokupinga na kukuchukia, ndivyo unavyopaswa kuwa na hamasa ya kuendelea zaidi. Maana ukiacha, unawapa ushindi rahisi, na watafurahia maisha yao yote kwamba wamekuweza. Japokuwa hufanyi kwa ajili yao, lakini pale unapokutana na ugumu, na ukafikiria kuacha, fikiria ni jinsi gani wale waliokuambia huwezi watashangilia, na usikubali kuacha kabisa, endelea kuweka juhudi na mwisho wake utashinda, na wenye chuki watakuchukia zaidi.

SOMA; Kama Wewe Ni Mjasiriamali, Acha Kabisa Kuogopa Mambo Haya.

Na usifanye makosa, usifikiri kwamba ukifanikiwa kwenye kile wanachokuambia huwezi watakukubali na kuacha kukukosoa au kukuchukia, bali watazidi kukuchukia. Hivyo usijiambie nitawaonesha na wote watanikubali, hilo halitatokea, watatafuta kila njia ya kuonesha kwamba ulichofanya siyo kikubwa au hukuweza mwenyewe, bali umesaidiwa au umepata bahati.

Fanya kile unachopanga kufanya, na asiwepo yeyote wa kukuambia huwezi, au haiwezekani. Na wengi watakuchukia,  furahia hilo maana ni dalili nzuri kwamba unafanya makubwa na ni msukumo kwako kutokurudi nyuma.

Usitake kila mtu akubaliane na wewe, na kama hakuna wanaokupinga, kukukatisha tamaa au kukuchukia, fanya tathmini ya maisha yako upya, ulipo siyo sehemu sahihi kwako kuwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Rafiki, kama ungependa kujifunza zaidi kupitia mafunzo ninayotoa, karibu ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA. Hii ni blog maalumu inayoenda na kundi maalumu la wasap ambapo kila siku unajifunza na kuhamasika, kila wiki kuna madarasa ya mafanikio na kila mwaka kuna semina tatu nzuri sana kwa mafanikio yako.

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA tuma ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa wasap kwenda namba 0717396253 au fungua hapa;  www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Usomaji