Ni kawaida yetu sisi binadamu, pale mambo yanapokwenda vibaya, tunapopata matokeo tofauti na tuliyotegemea, huwa tunaanza kuangalia nani kasababisha, nani kapelekea mpaka tukapata matokeo hayo. Huwa hatuamini kwamba sisi wenyewe ndiyo tunaweza kuwa tunahusika, kwa sababu tunapenda kupeleka lawama kwa wengine.

Leo nataka kukukumbusha hili muhimu sana mwanamafanikio, siyo kosa la yeyote kwamba maisha yako yana changamoto au unakutana na matatizo. Ingekuwa ni wewe pekee dunia nzima unayekutana na changamoto au matatizo basi tungeweza kusema kuna namna.

Maisha

Lakini kwa kuwa kila mtu hapa duniani anapitia matatizo na changamoto mbalimbali, basi tunaweza kusema kwamba matatizo na changamoto ni sehemu ya maisha. Hivyo kukutana nayo ni nafasi ambayo kila mtu anayo kwenye maisha.

Katika kila unachofanya, kuna matokeo mengi mabaya unaweza kupata, wakati matokeo mazuri ya kupata ni machache sana. Katika kila hali, una nafasi kubwa ya kukosea na kukutana na matatizo kuliko kupatia na mambo yakawa rahisi.

Hivyo jikumbushe hili kila unapokutana na matatizo au changamoto usikimbilie kuangalia nani kahusika, nani kafanya nini, bali jua ni sehemu ya maisha. Na kikubwa unachopaswa kufanya ni kuangalia hali uliyokutana nayo imekufundisha nini?

UKURASA WA 1105; Acha Kukazana Kuibadili Dunia, Nenda Nyumbani Kaipende Familia Yako.

Kila matatizo au changamoto tunazokutana nazo ni somo kwetu, ni ukumbusho wa vitu ambavyo bado hatujavijua au kujifunza. Kila ugumu tunaokutana nao ni ukumbusho kwetu kwamba hatujui kama tunavyofikiri tunajua, hatujapiga hatua kubwa kama tunavyodhani tumepiga.

Hivyo usitafute nani mchawi nani anayekufanyia ubaya, jua ni sehemu ya maisha na jifunze ili kuwa bora zaidi ili wakati mwingine tatizo na changamoto kama hiyo isiwe kikwazo kwako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog