AMKA mwanamafanikio,
Amka kutoka kwenye ndoto za siku moja mambo yatakuwa mazuri na nenda kaweke juhudi kuyafanya mambo kuwa mazuri kweli.
Tayari siku mpya, siku bora na ya kipekee ipo kwenye mikono yetu.
Ni maamuzi yetu sisi wenyewe tuitumieje siku hii, kama tuitumie kwa kuzalisha na kusonga mbele zaidi. Au tuipoteze kwa kulalamika na kusema tutafanya kesho.

Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA na mwongozo wetu ni TATUA, AMUA NA ONGOZA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari USIFANYE MAMBO KUWA MAGUMU ZAIDI YA YALIVYO..
Mambo mengi kwenye maisha siyo magumu sana, ila sisi wenyewe huwa tunapenda kuyafanya kuwa magumu.
Na kinachowazuia wengi wasifikie malengo wanayotaka, ni kufanya mambo kuwa magumu zaidi ya yalivyo.

Kama kuna kitu muhimu unataka kufanya kwenye maisha yako, unapaswa kuanza kukifanya.
Huhitaji kuanza kujiuliza je utaweza au huwezim utashindwa au utafanikiwa. Kitu ni muhimu kifanye. Wala usianze kujiambia bado sijawa tayari, nitafanya kesho, au siku moja mambo yatakuwa mazuri.
Kama kitu ni muhimu zaidi, kifanye, kuna ugumu gani hapo?

Kama kuna kitu ambacho siyo muhimu kwako na hutaki kukifanya, acha mara moja kukifanya.
Huhitaji kuanza kujishauri unaachaje, au watu watakuchukuliaje, au maisha yako yatakuwaje baada ya kuacha kufanya.
Kitu siyo muhimu kwako, haijalishi umekifanya miaka 10 au 20, acha kukifanya, acha mara moja na fanya kile ambacho ni muhimu. Kuna ugumu gani hapo?

Kuna mtu anataka ufanye kitu, lakini wewe hutaki, kwa sababu unajua iitu hicho siyo muhimu na una mambo muhimu zaidi ya kufanya. Unaogopa kumwambiw hutafanya, hivyo unamwambia hutafanya halafu hufanyi, unaanza kupiga chenga. Huoni happ unayafanya maisha kuwa magumu kuliko yanavyostahilo?
Kitu hutaki kukifanya sema HAPANA, sitaweza kufanya, na mtu atajua hatua zipi za kuchukua yeye mwenyewe.

Maisha ni magumu, lakini tunaongeza zaidi ugumu kwa namna tunavyoyafanya mambo kuwa magumu zaidi ya yalivyo.
Pale tunapofanya mambo ambayo siyo muhimu, na kuacha kufanya yale muhimu.

Nikukumbushe rafiki, maana nimekuwa nakuambia hili mara kwa mara, jua hasa nini unataka kwenye maisha yako, jua nini unapaswa kufanya ili kupata kile unachotaka na anza kufanya, na usiache kifanya mpaka utakapopata unachotaka.
Kuna ugumu gani hapo? Ndiyo, utashindwa, ndiyo utakutana na changamoto, kwa hiyo? Ukiacha au kulalamika ndiyo utapata unachotaka?
Jibu ni hapana, njia pekee ya kupata unachotaka ni kufanya unachopaswa kufanya, hivyo fanya, mpaka utakapopata.

Ukawe na siku bora sana ya leo rafiki, siku ya kuacha kuyafanya mambo kuwa magumu zaidi.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYoueLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha