Maisha yetu ni mkusanyiko wa matukio mbalimbali yanayotokea kwenye kila siku ya maisha yetu.

Japokuwa tunaweza kuwa na lengo moja kubwa tunalofanyia kazi, lakini hatutaamka siku moja na kujikuta lengo limetimia. Badala yake kila siku tunapiga hatua kuelekea kwenye lengo lile kubwa.

Sasa watu wengi huwa wanasahau maisha ya kila siku pale wanapofanyia kazi lengo moja kubwa. Wanaona wakishafikia lengo lile basi maisha yao ndiyo yatakuwa na maana. Wanaona wakishafika wanakotaka kufika ndiyo watakuwa na furaha na maisha yatakuwa mazuri kwao.

Na hapo ndipo wengi sana wanapokosea na maisha yanakuwa hovyo sana kwao. Hapa ndipo wanapozaliwa wale watu ambao wanaonekana wamefanikiwa sana ila hawana furaha ndani yao na wala maisha siyo mazuri kwao.

Maisha ya uhai ni maisha ambayo kila siku mtu unaweza kuona na kuishi vitu hivi viwili; furaha na uzuri.

Unapaswa kuwa na furaha wakati wote wa maisha yako, licha ya kujali upo wapi au una nini. Kila siku ni siku unayopaswa kuwa na furaha, kwa sababu kuna mengi mazuri yanaendelea kwenye maisha yako mpaka kufika pale ulipofika sasa. Haihitaji usubiri uwe na chochote au mpaka upate kitu fulani ndiyo uwe na furaha, furaha ni sehemu ya maisha ya kila siku.

SOMA; UKURASA WA 990; Raha Na Furaha Ipo Kwenye Mchakato Na Siyo Matokeo…

Unapaswa kuona uzuri wa maisha wakati wote wa maisha yako, hata kama unaona mambo ni magumu kiasi gani kwako. Maisha ni mazuri na kila unachokutana nacho kwenye maisha ni kwa ajili ya kukufanya wewe uwe bora sana. Ukiona maisha ni mabaya, maisha hayafai, kwanza utajizuia kufika kule unakotaka kufika, na hata kama utafika, basi maisha yatazidi kuwa mabaya kwako.

Ndiyo maana nakuambia asubuhi hii rafiki yangu, kama huoni vitu hivi viwili, furaha na uzuri wa maisha kila siku ya maisha yako, basi ni sawa na mtu ambaye hayupo hai. Kwa sababu kuwa hai na huku huna furaha na maisha unayaona ni mabaya hakuna maana yoyote.

Vitu hivyo viwili, haviletwi na yeyote au chochote kwenye maisha yako. Bali vinaanza na wewe mwenyewe, vinaanzia ndani yako, kwa wewe kuchagua kuishi maisha yako kwa namna ambayo utakuwa na furaha na utayaona maisha ni mazuri kila wakati, hata kama unapitia magumu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog