Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwa kila mmoja wetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari NO LIMIT…
Kama kuna kitu chochote umewahi kukitaka kwenye maisha yako, lakini hukukipata, ninamjua nani aliyesababisha usikipate.
Siyo serekali,
Siyo wazazi wako ambao hawakukujali,
Siyo wanasiasa au viongozi ambao hawakuwa na vipaumbele sahihi,
Siyo ndugu, marafiki au jamaa ambao hawakukuelewa,
Siyo hali mbaya ya kiuchumi,
Siyo mazingira ambayo hayakuendana na ulichotaka
Na siyo jamii inayokuzunguka ambayo haikukuelewa.
Yupo mtu mmoja tu ambaye alikuzuia wewe usipate unachotaka, na ataendelea kukuzuia zaidi usipaye mengine unayotaka, kama hutamjua na kumdhibiti.
Mtu huyo ni wewe mwenyewe, ndiyo, yaani wewe, kwa maneno mengine ukijiambia MIMI NDIYE MTU PEKEE AMBAYE NIMEKUWA NAJIZUIA NISIPATE NINACHOTAKA
Ndiyo, wewe umekuwa unajizuia kupata unachotaka, na unaweza usiamini hili kwa sababu huenda umeshajiambia umefanya kila kitu lakini hujapata unachotaka. Ni kweli unaweza kujiambia hivyo, lakini unajidanganya.
Wewe pekee umekuwa kikwazo kwako,
Wewe pekee umejiwekea ukomo, kwenye akili yako, fikra zako na maisha yako kwa ujumla.
Umejiambia vitu gani unaweza kufanya na vipi huwezi kufanya, huo ni ukomo.
Umejiambia wewe ni mtu wa aina gani hivyo unastahili kupata nini, huo ni ukomo.
Ndani ya akili yako kuna kiwango fulani cha uvumilivu umeshajiwekea, huo ni ukomo.
Kitu pekee kinachokufanya ushindwe kufanikiwa, ushindwe kupata unachotaka ni ukomo uliojiwekea.
Kama hutaondoa ukomo huo, ambao unaanzia kwenye fikra, hakuna kikubwa utaweza kufanya.
Asubuhi hiifikiria mambo makubwa matatu ambayo ulitaka sana kuyapata lakini hukuyapata, na jiulize ni ukomo gani ulikuwa umejiwekea mpaka ukakubali kirahisi kutokuendelea.
Ondoa ukomo huo na anza tena, kama mambo hayo ni muhimu sana kwako na unayaamini kweli kweli.
Maana imani ni moja ya ukomo unaokuzuia usipate unachotaka.
NO LIMIT, chochote unachotaka kufanya, ambacho ni muhimu sana kwako na kwa wengine na unakiamini kweli, ondoa kila aina ya ukomo uliojiwekea na fanya ka a huwezi kushindwa, kwa sababu ukweli ni huwezi kushindwa kama hujakata tamaa.
Jiweke huru kuweka juhudi kubwa ili kupata matokeo makubwa, bila ya ukomo wowote.
Ukawe na siku bora sana ya leo rafiki yangu, siku ya kuondoa kila aina ya ukomo uliojiwekea na kufanya kama vile hakuna kushindwa.
#NoLimit #Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa #WhatEverItTakes
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha