Rafiki yangu mpendwa,
Hongera sana kwa nafasi nyingine nzuri ya siku hii ya leo, nafasi bora na ya kipekee kwa kila mmoja wetu kwenda kufanya makubwa sana kwenye maisha yake.
Rafiki, leo napenda kukukumbusha kwamba zama tunazoishi sasa ni zama zenye changamoto kubwa sana. Ni zama ambazo upekee wa mtu yeyote yule kwenye kazi au biashara anayofanya siyo mkubwa sana.
Hii ni kwa sababu taarifa na maarifa yamesambaa sana na mtu yeyote yule anaweza kupata maarifa na taarifa yoyote anayotaka ndani ya muda mfupi sana.
Siku za nyuma wapo watu walioweza kufanikiwa sana kwa sababu walijua kitu ambacho wengine hawakuwa wanajua. Na walikiweka siri na hivyo kunufaika wao wenyewe.
Lakini sasa hivi ni vigumu sana kuweza kufanya hivyo. Chochote unachojua, kila mtu anaweza kujua kama atataka kutafuta na kujua. Hivyo huwezi kutumia kile unachojua, yaani maarifa na taarifa kama kitu kinachokutofautisha na wengine.
Kitu kingine ambacho nimekuwa nawaambia watu ni kwamba kila mtu anaweza kubadilishwa, yaani nafasi yoyote mtu anashikilia sasa hivi, iwe ni kwenye kazi au biashara, inaweza kuchukuliwa na mtu mwingine.
Hivyo wale wanaofanya kazi wakiamini hakuna mtu mwingine anayeweza kushika nafasi waliyonayo, na hivyo kujiamini kwamba wakiondolewa basi mambo hayataenda, wanajidanganya sana. Kila mtu anaweza kuondolewa popote na wala dunia haitajua kama ameondolewa.
SOMA; Una Nini Cha Tofauti Mpaka Watu Wakufuate Na Kukusikiliza? Jua Hapa.
Kadhalika kwenye biashara, wapo watu wamekuwa wakifikiri kwamba iwapo wataondoka kwenye biashara zao leo, basi watu watapata shida kwa kutokuwepo kwao. Lakini utashangaa sana siku ukiondoka wala watu hawatachukua muda mwingi kuulizia na kusubiria, wataangalia nani mwingine anayetoa wanachotaka na kwenda kupata.
Yote hii ni kukuambia wewe rafiki yangu kwamba, vitu unavyofikiri vinakupa upekee na kukuzuia kuondolewa pale ulipo sasa havipo. Usijidanganye kwa namna yoyote ile kwamba pengo lako haliwezi kuzibika, linazibika tena haraka sana.
Chochote unachofanya sasa, wapo wengine wengi wanaoweza kufanya, na kama kina manufaa basi wengine wengi nao watafanya. Na wala haitahitaji sana ubunifu au uwezo wa tofauti. Mtu akichagua kujifunza, maarifa yanapatikana kwa urahisi na ataweza kufanya tu vizuri.
Pamoja na hayo yote, kwamba chochote unachofanya wengine wanaweza kufanya, na popote ulio pengo lako linaweza kuzibika iwapo utaondoka, kuna kitu kimoja tu ambacho kinaweza kukutofautisha na watu wengine.
Kitu hichi kama ukiweza kukitumia vizuri, kitakuweka mbele sana ya wengine na kitakuwezesha kufanikiwa sana. Kitu hicho siyo kwamba watu hawakijui, ila hawapo tayari kukifanya, na hivyo thamani yake inakuwa kubwa sana.
Kitu pekee ambacho kinaweza kukutofautisha na watu wengine wote hapa duniani ni kiasi cha kazi unachoweka, kwenye lolote lile ambalo unafanya.
Iko hivi rafiki, kila mtu anajua kwamba kazi inahitajika sana ili kufanikisha lolote lile. Lakini kazi ni ngumu, kazi inaumiza na kazi inachosha. Watu wengi hawapendi ugumu, hawapendi maumivu na hawapendi kuchoka, hivyo huwa wanatafuta kila namna ya kukwepa kufanya kazi.
Kwa namna hiyo wanatafuta njia za mkato za kupata wanachotaka, wanaweka juhudi ndogo sana kwenye kile wanachofanya na wanachoka na kukata tamaa haraka sana wanapokutana na vikwazo na changamoto.
Hapo ndipo panapobaki ombwe kubwa ambalo ukiwa tayari kuweka kazi kubwa, utaweza kulijaza na ukatengeneza utofauti wako na wale wengine wanaofanya kile unachofanya wewe, iwe ni kazi au biashara.
Penda sana kila unachofanya kiasi kwamba kinakuwa siyo kazi tena bali sehemu ya maisha yako. Kijali sana kiasi kwamba unakuwa tayari kuweka juhudi kubwa sana, na wala hujisikii kama unafanya kazi, bali unaona unatoa mchango wako kwenye kuiboresha zaidi dunia.
Penda kile unachofanya kiasi kwamba kila asubuhi inapofika unaamka kwa hamasa ukijua ni siku mpya ya kwenda kufanya makubwa, na kila siku ya kazi inapoisha unatamani sana kesho yake ifikie ili uendelee.
Penda sana kile unachofanya na kuwa tayari kuweka kazi bila ya kuangalia ni saa ngapi unaanza na saa ngapi unamaliza. Wakati wengine wanachelewa kuanza kazi zao na kuwahi kumaliza, wewe wahi kuanza na chelewa kumaliza. Kinachokusimamisha kwenye kazi kinakuwa siyo kwa sababu muda wa kumaliza umefika, bali muda wa siku umeisha.
Penda sana unachofanya na jitoke kukifanya kweli kiasi kwamba hujui hata ni siku gani ya wiki. Hujui kwamba siku fulani ni jumamosi au jumapili na hamna kazi, wewe unachokuwa unajua ni kwamba jua likichomoza ni siku ya kazi.
Penda sana unachofanya kiasi kwamba masaa 14, 16 na hata 18 ya kufanya kazi kwa siku siyo kitu unachofikiria mara mbili wala kukutisha. Wingi huo wa masaa ya kufanya kazi ni kitu cha kawaida kwako, na unatumia kweli kila saa ya kazi yako kwa uzalishaji wa hali ya juu.
Ni kazi ambayo upo tayari kuweka itakayokutofautisha na watu wengine wote, kadiri utakavyoweka kazi kubwa na bora zaidi, ndivyo utakavyojiweka mbele zaidi ya wengine.
Na hata hili haliwezi kujificha, fikiria mtu wa kawaida, ambaye anaanza kazi yake saa mbili asubuhi na kumaliza saa kumi, anafanya siku tano au sita za wiki, nyingine anapumzika, na siku ya kazi ana karibu masaa mawili ya kupumzika. Halafu fikiria wewe ambaye unaanza kazi saa kumi na mbili asubuhi na kumaliza saa mbili usiku, au hata saa nne, na muda wote wa siku unafanya kazi, na siku zote saba za wiki unafanya kazi.
Wewe unaweka muda mara mbili ya anaoweka mtu wa kawaida, hivyo hata kama utaweka juhudi sawa na wengine, bado utaweza kukamilisha kitu kwa nusu ya muda wanaotumia wengine kukamilisha.
Sasa wewe rafiki yangu, kama unaweza kukamilisha chochote kile kwa nusu ya muda ambao wengine wanatumia kukamilisha, na ukaweza kuweka ubora mara mbili ya ambao wengine wapo tayari kuweka, utaweza kufanikiwa kwa sehemu kubwa sana kuliko wengine wanavyoweza kufanikiwa.
Mchezo ni kazi rafiki, kazi unayoweka ndiyo kitu pekee kitakachotengeneza utofauti wako hapa duniani. Na kama kwa vyovyote vile utaanza kushangaa kwamba haiwezekani mtu ufanye kazi muda mrefu na kwa juhudi hivyo, kwamba una maisha mengine ya kufanya zaidi ya kazi, basi hakuna kikubwa kinaweza kufanywa kuhusu wewe.
Kama unaamini wewe ni bora kuliko kazi, na kama umenunua ule ukawaida wa wengine kwamba kuna maisha na kazi, basi jua umejitenga na mafanikio. Umejichanganya katikati ya kundi kubwa la watu na hakuna anayeweza kukuona wewe wala upekee wako.
Weka kazi, kusiwe na tofauti kati ya kazi yako na maisha yako, vyote viwe kitu kimoja na ndiyo maana unapaswa sana kupenda chochote unachotaka. Na siyo lazima uwe ulizaliwa unakipenda, bali kama ndiyo kitu inabidi ufanye, basi unachagua kukipenda na unakifanya kwa upekee kabisa.
Rafiki, kwa kusisitiza nikuambie tu, kama haupo tayari kuweka kazi kubwa kwenye chochote unachofanya, ni heri hata usifanye, maana unapoteza muda wa kila mtu. Unapoteza muda wako maana hakuna kikubwa utakachopata, na pia unapoteza muda wa yule unayemfanyia kazi maana unampa kitu cha kawaida ambacho anaweza kupata pengine.
Pia kama hakuna mtu anakuambia unafanya kazi sana, kama hakuna mtu anashangaa unawezaje kukamilisha uliyokamilisha, kama hakuna wanaokuambia punguza kazi kidogo maana unaenda sana, kama hakuna hata mmoja anakuambia hayo, nasikitika kukuambia kwamba hakuna kazi kubwa unayoweka.
Na watu wengi wanaweka kazi ndogo sana na za kawaida sana kiasi kwamba ukiwa tayari kuongeza juhudi kidogo mno kuliko kawaida, utaweza kujitenga kwa sehemu kubwa sana na wale wa kawaida.
SOMA; Hii Ndiyo Faida Kubwa Ya Kuwa Na Watu Wanaokupinga Na Hata Kukuchukia.
Weka kazi rafiki, weka kazi mara mbili ya wanavyoweka wengine wanaokuzunguka, na kwa hakika, utakuwa tofauti kabisa na wengine. Dunia inaona haraka sana wale wanaoweka kazi, wale wanaozalisha zaidi na inawalipa kulingana na wanavyoweka kazi na wanavyozalisha.
Chochote unachokitaka hapa duniani, unaweza kukipata, kama utakuwa tayari kuweka kazi kubwa na ya kipekee sana kadiri dunia inavyotaka. Kama haupo tayari kuweka kazi kubwa, dunia haina nafasi kubwa kwako na mafanikio siyo kitu utakachokutana nacho.
Kitu pekee kitakachokutofautisha na wengine, siyo kipaji ulichonacho, siyo maneno unayoweza kuongea na siyo bahati ulizonazo, bali kiwango cha kazi unachoweka na matokeo makubwa unayozalisha.
Fanya kazi kuwa nguzo kuu ya maisha yako, na weka juhudi kubwa, weka muda mwingi na dunia itakuwa tayari kukulipa kwa namna unavyojitoa.
Ipende kazi rafiki, usiyatofautishe maisha yako ya kawaida na kazi yako.
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha