Popote ulipo na chochote unachofanya, zipo nafasi nyingi sana za kufanya kuliko ambavyo unaweza kuzitumia. Nafasi za kufanya kwa ubora zaidi ni nyingi, lakini wengi wamekuwa wanatuma nafasi na njia chache, zile walizozoea, zile ambazo wamekuwa wanaona wengine wakitumia.
Ndiyo maana mtu anaponiambia ameshafanya kila kitu lakini hapati anachotaka huwa nakataa. Kwa sababu najua hakuna anayeweza kufanya kila kitu.

Kwa mfano kama kuna kitu unauza, halafu unasema umekazana sana kuuza lakini hupati wateja wa kununua. Unafikiri hilo linaweza kuwa kweli? Halina ukweli hata chembe moja. Kuna watu zaidi ya bilioni saba duniani, na huwezi kupata hata watu 10 au 100 wa kununua unachouza? Halafu unasema umefanya kila kitu! Yaani unataka kuwaaminisha kwamba umeongea na watu wote bilioni saba na hujapata wa kununua?
Wengi wamekuwa wanakata tamaa haraka kabla hata hawajatumia nafasi zaidi ya moja au mbili walizozoea kutumia.
Kabla hujajiambia huwezi tena kufanya, kabla hujajiambia kitu hakiwezekani, kabla hujafikia hitimisho kwamba hutaendelea tena kufanya, naomba ujiulize na ujipe jibu la swali hili, je nimetumia njia zote na nafasi zote zinazopatikana za kufanya?
SOMA; UKURASA WA 839; Haijalishi Hali Ya Uchumi Ikoje, Fursa Za Kutengeneza Fedha Bado Ni Nyingi…
Na usije ukajipa jibu la ndiyo ili ujihalalishie kuacha, maana hakuna awezaye kutumia kila nafasi na kila njia. Hivyo kama utaacha, acha kwa sababu umeamua kuacha, kwa sababu siyo muhimu sana kwako au kwa sababu una uzembe mkubwa sana kiasi kwamba huwezi kujitoa zaidi.
Lakini usiache ukisema huwezi, haiwezekani au umekazana sana na imeshindikana. Njia zipo nyingi sana, kama kitu ni muhimu sana kwako, kama una kiamini kweli basi utafanya kila linalopaswa kufanya na kuweza kukamilisha. Kama kitu siyo muhimu na kama hukiamini kweli kweli utakuwa na kila sababu ya kuacha.
Njia moja ikishindikana, nafasi moja ikiisha jua zipo njia na nafasi nyingine nyingi, usibadili kile unachotaka kupata, bali badili njia na nafasi ya kukifikia.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,