Faida ndiyo kitu kinachofanya biashara iendelee kuwepo. Kama biashara haitengenezi faida, haitachukua muda mrefu, itakupa.
Pamoja na kuweka juhudi kubwa kwenye kuongeza mauzo na mapato, sehemu kubwa inayopunguza faida ya biashara ni gharama za kuendesha biashara hiyo.
Gharama za kuendesha biashara zinapokuwa kubwa, faida inakuwa ndogo au hakuna kabisa.
Hivyo eneo muhimu kwenye kuongeza faida kwenye biashara yako, ni kudhibiti gharama zako. Na kama gharama zipo juu basi unazipunguza, kwa kuondoa zile ambazo siyo muhimu.
Sasa, karibu kila biashara ina gharama ambazo siyo muhimu sana na zinaweza kupunguzwa. Ila wafanyabiashara wengi wamekuwa wanakosea, wamekuwa wanachelewa kupunguza gharama zao za biashara na hilo linapelekea biashara nyingi kufa.
Wafanyabiashara wengi, huwa wanaanza kufikiria na hata kupunguza gharama pale ambapo biashara haipati faida, pale wanapoanza kuona biashara inayumba. Lakini kwa muda huo wanakuwa wameshachelewa sana kiasi kwamba matokeo wanayopata kwenye kupunguza gharama siyo makubwa, na yanakuwa hayana msaada.
Wakati sahihi wa kupunguza gharama kwenye biashara ni wakati biashara inatengeneza faida kubwa sana. Wakati ambapo biashara ipo kwenye kilele cha mafanikio na wewe mfanyabiashara unajiona kama umeshajua kila kitu kwenye biashara.
Huu ni wakati sahihi kupunguza gharama kwenye biashara yako kwa sababu ndiyo wakati ambao ni rahisi sana kujisahau kwenye biashara. Pale biashara inapotengeneza faida kubwa, ndipo wengi wanapojisahau sana na kukuta gharama zinapanda zaidi. Gharama zinapokuwa kubwa, faida inakuwa ndogo na wanaacha kukazana na kile kilicholeta faida na kuanza kukazana na kupunguza gharama, kitu kinachopelekea biashara kufa.
Kila siku kwenye biashara yako lazima ujiulize swali hili, ni gharama gani naweza kupunguza kwenye biashara yangu leo? Angalia kila unachofanya na jiulize kama kinaweza kufanyika kwa gharama ya chini zaidi kuliko unavyofanya sasa.
Kama unataka kufanikiwa kwenye biashara, kama unataka kupata faida kubwa na kuimarisha biashara yako, unahitaji kudhibiti sana gharama zako wakati unatengeneza faida kubwa kama vile biashara ipo kwenye hali mbaya. Usijisahau na kuona faida unayopata ni kubwa na hivyo inaweza kumudu gharama zozote. Tabia ya gharama ni kukua kama zisipoangaliwa. Angalia gharama zako kila wakati na dhibiti.
Na wakati sahihi wa kudhibiti na kupunguza gharama zako za biashara ni kila siku yako ya kibiashara.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,