Mtazamo ambao unao kwenye biashara unayofanya, ni moja ya vitu ambavyo vitaifanya biashara hiyo ifanikiwe sana au ishindwe kabisa. Hata kama utafanya kila kinachopaswa kufanya, kama mtazamo siyo sahihi, bado biashara haitapata matokeo makubwa.

Mtazamo ambao mfanyabiashara anao huwa unakuwa kikwazo au kichocheo kikubwa kwa mafanikio ya biashara hiyo. Kuna mitazamo ambayo inasukuma biashara kufanikiwa zaidi, na ipo mitazamo ambayo inaizuia biashara kufanikiwa.

Moja ya mitazamo ambayo ina madhara ya aina hii kwenye biashara ni kuhusu mteja na fedha zake.

Wafanyabiashara wengi, ambao wamekuwa hawafanikiwi sana, wamekuwa wakimwangalia mteja kama mtu wa kuwapa wao fedha. Hivyo wanaangalia kila namna ya kuchukua fedha ambayo mteja anayo. Na hapa ndipo wanapowalazimisha watu wanunue vitu ambavyo hawavitaki, ambavyo siyo bora kwao na haviwapi matokeo wanayotaka. Kinachotokea, watu wa aina hii wakishanunua, hawarudi tena, hivyo biashara inapoteza wateja.

Wafanyabiashara ambao wanafanikiwa sana, wamekuwa wakimwangalia mteja kama mtu anayetaka kupata fedha zaidi, na hivyo lengo la biashara zao ni kuwawezesha wateja kupata fedha zaidi. Kwa mtazamo huu, mfanyabiashara anampa mteja kitu ambacho kitampunguzia gharama ambazo kwa sasa anaingia, au kumwongezea kipato zaidi ya anachofanya sasa. Kwa njia hii, mteja akinunua anaridhika na atarudi tena pamoja na kuwaambia wengine.

SOMA; BIASHARA LEO; Mteja Hajui Anachotaka, Ila Anajua Kitu Hiki Muhimu Sana.

Kila mtu anataka kupata fedha zaidi, kila mtu. Njia pekee ya kuifanya biashara yako idumu, ni kuwapa watu kile wanachotaka zaidi, ambacho ni kupata fedha zaidi.

Lakini hii hamaanishi uwe kwenye biashara ili kuwagawia watu fedha. Hapana, zipo njia nyingi za biashara yako kuwawezesha watu kupata fedha zaidi. Baadhi ni kama;

  1. Kutoa bidhaa au huduma ambazo zinampunguzia mteja gharama za kuendesha maisha yake.
  2. Kutoa bidhaa au huduma ambazo zinamwezesha mteja kuongeza kipato chake zaidi.
  3. Kutoa bidhaa au huduma bora sana ambapo mteja hatahitaji kununua tena mara kwa mara au kufanya matengenezo.
  4. Kutoa bidhaa au huduma ambayo mteja ana uhakika kama haitafanya kazi basi fedha yake itarudi au atapata kinachomfaa.
  5. Kumpa mteja zawadi mbalimbali pale anapoleta mteja mwingine.

Upo kwenye biashara kuwafanya wateja wako wapate fedha zaidi, tumia nafasi hiyo vizuri na utafanikiwa sana kwenye biashara.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha