Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni siku bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari UNACHOSTAHILI NA UNACHOPATA…
Kila mtu kuna uongo ambao amekuwa anajiambia kwenye maisha yake.
Na ukubwa wa uongo ambao wengi wanajiambia, unaendana na udogo wa ndoto walizonazo.
Yaani mtu ukiwa na ndoto kubwa, uongo unaojiambia ni mdogo, lakini ukiwa na ndoto ndogo na maisha yako, uongo utakaojiambia ni mkubwa sana.

Mfano mtu mwenye ndoto ndogo kwenye maisha yake, atajidanganya sana kwamba hana haja ya kuwa na ndoto kubwa, kwamba maisha yake yana furaha, kwamba mafanikio makubwa siyo kila kitu. Yaani mtu anaweza akawa halalo usiku akifikiria kesho anakula nini, halafu atakuwa wa kwanza kukuambia fedha siyo kila kitu, wakati inawanyima usingizi.

Eneo kubwa ambalo watu wamekuwa wanajidanganya, ambao leo nataka tulitafakari kwa kina kwenye maisha yetu ni eneo la KUSTAHILI.
Chochote ambacho kwa sasa huna, halafu unajiambia kwamba unastahili kukipata, unajidanganya.
Unajidanganya kwa sababu hakuna anayepata kile anachostahili kwenye maisha yake,
Kila mtu anapata kile anachopigania, kile anachojitoa kweli na kile ambacho yupo tayari kukivumilia.
Hakuna anayepata chochote kwa sababu anastahili kupata.
Na wengi wamekuwa hawataki wanachotaka kwa sababu wanajiambia wanastahili kupata, badala ya kujitoa, kupigana na kupambana mpaka wapate wanachotaka.

Asubuhi hii hebu tafakari ni vitu vingapi umewahi kujiambia unastahili kupata kwenye maisha yako na vingapi hasa umepata. Utagundua, kama hukuchukua hatua kubwa, basi hukupata kile ulichostahili.
Sana sana utakuwa umeishia kuwalaumu wengine kwamba wamekuzuia kupata unachostahili.
Na wakulaumiwa hawajawahi kukosewa, wazazi ndiyo wanaongoza kwa kulaumiwa, inafuata serikali, halafu kuna waajiri na wengine huenda mbali mpaka kulaumu mazingira au hali ya hewa.
Kuna wale wasio na mshipa wa aibu, ambao wanaweza kuwalaumu watoto waliowazaa wenyewe kwamba ndiyo kikwazo kwao kupata walichotaka.

Rafiki, kumbuka tu, unapoanza kufikiria nani kafanya usipate unachostahili, jua kabisa hujachukua hatua, na utalaumu kila unayetaka kumlaumu, lakini mwisho wa siku ukweli utabaki kwamba hujapata ulichotaka. Na hutapata mpaka pale utakapoacha kusema unastahili kupewa na kuanza kuweka juhudi mpaka upate unachotaka.

Uwe na siku bora sana ya leo rafiki, siku ya kuchukua hatua kubwa kupata unachotaka na siyo kujiambia unastahili na kusubiri upewe unachotaka.
#Fanya #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha