Wahenga walituambia ni bora kuchelewa kuliko kutofika kabisa. Na hata kwenye jamii zetu, imekuwa ni kawaida kuchelewa sehemu fulani, kuliko kutokufika kabisa.
Hilo linaweza kuwa sahihi kwenye maisha ya kawaida, kwenye mahusiano na ahadi mbalimbali.
Lakini inapokuja kwenye swala la mafanikio, inapokuja kwenye hatua z akuchukua ili kufanikiwa, muda ndiyo kila kitu.
Ni muhimu sana kuchukua hatua sahihi, katika mazingira sahihi na muda sahihi. Na unapochelewa muda huo, ni bora hata usichukue hatua kabisa, badala yake ujiandae kwa nafasi nyingine au uchukue hatua nyingine.

Kwa mfano pale unapoona kitu fulani ni fursa nzuri kwako kupiga hatua, lakini ukawa unasubiri kwa sababu huna uhakika, au unaona hujajiandaa vya kutosha, mara baada ya muda mfupi unakuta wengine wameshachukua nafasi ile. Kwanza kabisa huna wa kumlaumu bali wewe mwenyewe, na pili, kuchukua tena hatua zile zile ni kujiingiza kwenye ushindani usio na msingi, na kutaka kuyafanya maisha kuwa magumu kwako.
SOMA; UKURASA WA 965; Kufanya Vitu Kwa Usahihi Na Kufanya Vitu Sahihi…
Unapoona hata sahihi kwako kuchukua, na unaamini itakusaidia sana kusonga mbele, unahitaji kuchukua hatua hiyo mara moja. Kwa sababu kile unachoona sasa jua huoni mwenyewe, kuna wengine nao wanaona. Hivyo kama utachelewa kuchukua hatua, utakuja kukuta wengine wameshachukua hatua na utajilaumu sana.
Miaka 10 ijayo utajilaumu sana kwa hatua ambazo hukuchukua leo kuliko hata utakavyojilaumu kwa hatua ulizochukua ukashindwa. Hivyo usichukulie kushindwa kama sababu ya kutokuchukua hatua. Bali kuwa mtu wa kuchukua hatua pale unapojua kweli kwamba kitu ni sahihi na kitakusaidia sana kusonga mbele.
Usiwe mtu wa kuchelewa na kushindwa kupata kile unachotaka. Chukua hatua sahihi kwa wakati sahihi, na ukichelewa, katafute pengine ambapo utaweza kuchukua hatua sahihi kwa wakati sahihi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,