Rafiki yangu mpendwa,

Karibu tena kwenye makala za ushauri wa changamoto mbalimbali tunazokutana nazo kwenye maisha yetu, ambazo zinatuzuia kufika pale tunakotaka kufika na maisha yetu.

Changamoto siyo kitu kibaya, bali ni kiashiria kwamba tumejaribu mambo makubwa, mambo ambayo hatujayazoea huko nyuma. Hivyo kama tukitumia changamoto tunazokutana nazo kama darasa, tutaweza kupiga hatua zaidi.

Kinachowaponza wengi ni pale wanapochukulia changamoto kama ukomo, wanaona hawawezi kufanya tena na hivyo wanakata tamaa. Kumbuka kwenye safari ya mafanikio kukata tamaa ni mwiko. Hivyo kwenye makala hizi za ushauri, mimi rafiki yako nahakikisha hukati tamaa kabisa, kwa kukupa maarifa sahihi ya kuvuka kila aina ya changamoto unayokutana nayo.

Kwenye makala ya leo tunakwenda kuangalia changamoto ya kufa kwa biashara. Pamoja na kwamba kuingia kwenye biashara ndiyo njia bora ya kuongeza kipato chako, biashara siyo rahisi. Kuingia kwenye biashara ni moja ya mambo hatari sana unayoweza kufanya kwenye maisha yako.

Na siyo mimi tu nakuambia, bali ndivyo tafiti zinavyoonesha. Kwamba asilimia 80 ya biashara mpya zinazoanzishwa huwa zinakufa muda mfupi baada ya kuanzishwa. Nyingi zinakufa ndani ya mwaka mmoja, na mpaka miaka mitano inaisha, asilimia 90 zinakuwa zimekufa. Hii ina maana kwamba kama zikianza biashara kumi leo, miaka mitano ijayo itakuwa imebaki biashara moja pekee.

Hivyo kufa kwa biashara siyo kitu cha kushangaza, kwa hakika ndiyo njia ya biashara nyingi. Lakini wewe unataka mafanikio, hutaki biashara yako ife, na zipo njia za kuiwezesha biashara yako ifanikiwe zaidi na isife. Hizi ndiyo tutakwenda kujifunza kwenye makala ya leo.

BIASHARA NDANI YA AJIRA SOFT

Kabla hatujaangalia jinsi gani unaweza kuzuia biashara yako isife na iweze kukua zaidi, tupate maoni ya msomaji mwenzetu aliyetuandikia kwenye hili;

Kila nikianzisha biashara inakufa. – Prisca F. M.

Kama alivyotuandikia Prisca, na kama inavyotokea kwa wengi, biashara nyingi zinakufa. Wakati mwingine mwenye biashara anaona anafanya kila kilicho sahihi, lakini biashara bado inakufa.

Hizi hapa ni sababu kwa nini kila biashara unayoanzisha inakufa, na hatua za kuchukua ili kufanikiwa kwenye biashara.

Sababu ya kwanza; huna wateja wa kutosha kwenye biashara yako.

Biashara ni wateja, kama huna wateja wa kutosha kwenye biashara yako, hutaweza kuendesha biashara yako kwa muda mrefu, hata kama utaweka juhudi kiasi gani.

Lazima biashara iwe na wateja wanaoiamini na kuitegemea biashara hiyo. Wateja ambao wapo tayari kununua na wana mudu kununua bidhaa na huduma unazotoa.

Biashara nyingi zinakufa kwa sababu hazina wateja wa kutosha wanaonunua kwenye biashara hizo. Watu wengi wanaweza kuwa wanaijua biashara, ila waliopo tayari kununua ni wachache sana.

Hatua za kuchukua kuondokana na tatizo hili;

Yapo mambo mawili makubwa ya kufanya kuondokana na tatizo la biashara kutokuwa na wateja wa kutosha wanaonunua.

Hatua ya kwanza kuchukua ni kuhakikisha biashara yako inawafikia watu wengi zaidi. Unahitaji kuwa unawafikia wengi ambao wana sifa za kuwa wateja wako, wajue uwepo wako kibiashara na waje kwenye biashara yako. Hapa unahitaji kuwafikia wateja wapya kila wakati na kuwapa sababu kwa nini waje kwenye biashara yako.

Hatua ya pili ni kuwageuza wale wanaoijua biashara yako kuwa wateja wanaonunua. Hata kama kila mtu anajua kuhusu biashara yako, kama hawachukui hatua kununua, bado hao siyo wateja na hutadumu kwenye biashara kwa muda mrefu. Unahitaji kuwashawishi wale wote ambao wanajua kuhusu biashara yako wanunue, na siyo wanunue baadaye wakiwa tayari, bali wanunue sasa, kwa sababu kuna vitu watanufaika navyo wakinunua sasa kuliko wakisubiri wanunue baadaye. Kuwa na njia za ushawishi za kuwafanya wateja wanunue.

SOMA; Njia Tatu Za Kumuuzia Mteja Ambaye Amekataa Kununua. Jifunze Hapa Ili Usishindwe Kuuza Tena.

Sababu ya pili; mauzo yako kwenye biashara ni madogo.

Kuwa na wateja wengi pekee haitoshi, unaweza kuwa na wateja wengi lakini wakawa wananunua mara chache na wananunua vitu vichache kiasi kwamba biashara haipati mapato ya kutosha. Kama biashara yako haina mapato ya kutosha, itakufa.

Mzunguko wa fedha kwenye biashara ndiyo damu ya biashara husika. Kama mzunguko wa fedha haujakaa sawa, biashara lazima itakufa.

Hivyo angalia biashara yako inayokufa na utaona kwamba mzunguko wa fedha haujakaa sawa, mapato ni madogo na hakuna wateja wanaonunua kwa kujirudia au wanaonunua ka wingi.

Zipo hatua mbili za kuchukua ili kuongeza mapato kwenye biashara yako;

Hatua ya kwanza ni kuongeza idadi ambazo mteja anunua kwako kwa kipindi fulani. Kama mteja ananunua kwako mara moja pekee, biashara yako inapata hasara. Kwa sababu umetumia gharama nyingi sana kumfikisha mteja kwenye biashara yako. Ili unufaike na mteja, lazima anunue mara kwa mara. Hivyo ni jukumu lako kumshawishi mteja kununua mara kwa mara kwenye biashara yako. Hakikisha mteja akiondoka anarudi tena na tena kwenye biashara yako.

Hatua ya pili ni kuongeza kiasi cha manunuzi ambayo mteja anafanya anapokuja kwenye biashara yako. Usikubali mteja aje kwenye biashara yako anunue kile tu alichopanga kununua, bali muuzie vitu vingine vinavyoendana na kile alichonunua. Kama utamsikiliza mteja wako vizuri, na ukawa unaijua biashara yako vizuri, utaona vitu vingi sana vya kumuuzia mteja wako kila anapokuja kwenye biashara yako. Na hufanyi hivyo kwa manufaa yako tu, bali kwa manufaa ya mteja pia, kwa sababu unampa vitu ambavyo vitamsaidia sana.

Sababu ya tatu; biashara haitengenezi faida.

Biashara inaweza kuwa na wateja wengi ambao wananunua, na wananunua mara nyingi na kwa wingi, biashara ikawa na mapato makubwa, lakini bado ikafa. Hapa ndipo wale wasiojua biashara wala fedha hushangaa fedha za biashara zao zinaenda wapi, maana wanaona anauza sana, lakini biashara inakufa.

Kama biashara haitengenezi faida, haitegemei mapato ni makubwa kiasi gani, itakufa. Hivyo ni jukumu lako kubwa kuhakikisha biashara yako inatengeneza faida. Na faida halisi ya biashara ni kuchukua mauzo kisha unatoa mtaji wa mali ulizouza na gharama zote za biashara kwenye kipindi hicho cha mauzo.

Zipo hatua mbili za kuchukua ili kuongeza faida kwenye biashara yako;

Hatua ya kwanza ni kuongeza kiasi cha faida kwenye bidhaa au huduma unazouza. Kama unauza vitu vya bei rahisi, ni vigumu sana kupata faida hata kama una mauzo makubwa. Hivyo unaweza kuuza vitu vya bei ya juu kidogo lakini ambavyo ni bora. Vinapaswa kuwa bora sana kiasi kwamba mteja hatafikiria kuhusu bei.

Hatua ya pili ni kupunguza gharama za kibiashara. Kama kuna gharama unaingia kwenye biashara yako, ambazo hata usipoingia gharama za aina hiyo, biashara yako haitakufa, basi unapaswa kuachana nazo mara moja. Kila fedha unayotumia kwenye biashara yako, hakikisha ina umuhimu mkubwa, la sivyo ni bora usitumie. Kuwa sana mwangalifu na matumizi yako ya kibiashara, haya ndiyo yanatafuna faida ya biashara yako.

Rafiki, kama ulikuwa unafuatilia vizuri, utakuwa umeona hapo juu kuna sababu 3 za kwa nini biashara zinakufa, na hizo ndiyo sababu tatu pekee. Kila biashara inayokufa, sababu ni kati ya hizo tatu. Nyingine zote ni za ziada tu, ila sababu za msingi ni hizo tatu. Hivyo kama utazielewa vizuri, na kuziepuka, biashara yako itakuwa salama.

Pia kama umefuatilia vizuri makala hii, utakuwa umejifunza hatua sita za kuizuia biashara yako isife. Hatua hizi sita ni muhimu sana na hakuna biashara inayoweza kufa kama mambo hayo sita yatafanyiwa kazi.

HUDUMA KWAKO; Rafiki, nina masomo ya kuiwezesha biashara yako kukua na kuongeza faida kwa zaidi ya asilimia 50, ambapo ndani yake kuna njia 50 za kufanyia kazi ili kukuza biashara yako. Kama ungependa kupata masomo haya, jiunge na KISIMA CHA MAARIFA. Masomo yapo ndani ya KISIMA CHA MAARIFA. Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa wasap namba 0717396253.

Nakutakia kila la kheri katika kuendesha biashara yenye mafanikio makubwa, biashara isiyoshindwa wala kupata hasara. Hilo linawezekana kabisa kama utaelewa sababu tatu za biashara kufa, hatua sita za kuchukua na njia 50 za kukuza biashara yako zaidi.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Usomaji