Rafiki yangu mpendwa,

Changamoto kwenye maisha ni mrejesho kwetu kwamba kuna kitu hatukifanyi vizuri au kuna kitu hatujajua bado. Hivyo badala ya kuogopa na kukimbia changamoto, tunapaswa kuzipanda na kuzikaribisha.

Kila unapokutana kwenye changamoto kwenye maisha yako jiulize maswali haya mawili. Swali la kwanza ni kipi ambacho sijui kuhusu hili. Na swali la pili ni hatua zipi ambazo sichukui kuhusu hili.

Kwa sababu changamoto yoyote unayokutana nayo, chanzo chake na hata utatuzi wake ni maarifa sahihi na kuchukua hatua kubwa. Ambavyo hivyo viwili vitakupeleka kwenye mafanikio makubwa.

BIASHARA NDANI YA AJIRA SOFT

Karibu kwenye juma jingine ambapo unapata makala ya ushauri wa changamoto mbalimbali zinazotuzuia kufikia mafanikio makubwa.

Leo tunakwenda kuangalia njia tatu za kukuza biashara yako pale unapokutana na changamoto ya kukosa bidhaa bora kwa bei nafuu.

Kabla ya kuingia kwenye njia hizo mbili, tusome maoni ya msomaji mwenzetu aliyeomba ushauri kwenye hili;

“Nashindwa kuendeleza biashara yangu Ya Viatu vya mtumba wateja ninao ila sehemu Ya kupata hivyo viatu kwa bei rahisi na pia vyenye ubora. Naomba msaada yenu niweze kufikia malengo yangu makubwa asante”. – Natalia J. N.

Rafiki na msomaji wetu tayari ana kitu kikubwa sana, anayo biashara ambayo anaielewa na pia tayari anao wateja wa biashara yake. Lakini anakwama eneo moja, kupata bidhaa bora kwa bei nafuu ili akiuza kwa wateja wake apate faida na kuweza kukuza biashara yake.

Zifuatazo ni njia tatu ambazo mwenzetu anaweza kutumia ili kuvuka changamoto hiyo na kukuza biashara yake.

Njia ya kwanza; pata taarifa zaidi, usifanye kwa mazoea.

Rafiki yetu anatuambia hajui wapi pa kupata bidhaa bora na kwa bei nafuu. Lakini kama tutachukua muda na kumuuliza atuelezee ni masoko mangapi ameyatembelea kutafuta bidhaa yake atatupa masoko machache sana.

Unahitaji kupata taarifa zaidi na kuzunguka maeneo mengi zaidi ili kuweza kupata taarifa sahihi. Usiendeshe biashara kwa mazoea kwa kwenda pale ulipozoea kwenda kila wakati.

Angalia wengine nao wanapata wapi bidhaa zao, tafuta muda wa kutembelea masoko yote makubwa yanayouza bidhaa hiyo. Tafuta watu wanaofanya biashara hiyo na tengeneza nao mahusiano mazuri na hao watakuwa watu wazuri kukupa taarifa sahihi.

Kila siku hakikisha kuna kitu kipya unajifunza kuhusu biashara yako, ikiwa upatikanaji wake na hata wateja wako. Kama hujaweza kufikia uwezo wa kununua jumla ili kupata kwa bei nafuu, unaweza kujiunga na wengine na mkanunua mzigo wa jumla kwa pamoja na hapo mkapata kwa bei nafuu.

Pata taarifa sahihi, zipo nyingi sana kama utaanza kuzitafuta.

SOMA; USHAURI; Kwa Nini Kila Ukianzisha Biashara Inakufa, Na Hatua Za Kuchukua Ili Kufanikiwa Kwenye Biashara.

Njia ya pili; uza kwa bei uliyozoea kuuza, ila kwa wateja wengi zaidi.

Kama kwa namna unavyopata mzigo wako sasa hutengenezi faida kubwa ukiuza, basi hakikisha unauza kwa wateja wengi zaidi. Ukipata faida hiyo ndogo ndogo kwa wateja wengi, utaweza kukuza biashara yako zaidi.

Unahitaji kuwafikia wateja wengi na kuwapa bidhaa hiyo bora, ambayo siyo rahisi kwao kuipata kwa wengine.

Kadiri wateja wanavyokuwa wengi, ndivyo faida ndogo unayopata inakusanyika na kuwa nyingi, na hiyo itakuwezesha kukuza biashara yako.

Njia ya tatu; ongeza bei na lenga wateja wachache wanaomudu bei yako.

Njia ya tatu, kama hupati sehemu ya kununua kwa bei nafuu ni kuongeza bei unayouzia na kulenga wateja wachache ambao wanaweza kumudu bei hiyo.

Kwa kuwa bidhaa yako ni bora kabisa, basi unaweza kuwapata wenye uhitaji wa bidhaa bora kama hiyo na wakawa tayari kulipia bei unayouza.

Kwa njia hii utaweza kuwahudumia wateja wachache vizuri na ukatengeneza faida ya kuiwezesha biashara yako kukua zaidi.

Rafiki, tumia njia hizo tatu kuhakikisha unapiga hatua zaidi kwenye biashara yako. Na wakati wowote unapoona umekwama, chukua hatua fulani kuhakikisha una bidhaa bora na unauza kwa wateja wako.

Changamoto zitakuwa ngumu kwako kama hakuna hatua unazochukua, lakini ukipata maarifa sahihi na kuchukua hatua kubwa, kila changamoto itakukimbia.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog