When we hate our enemies, we are giving them power over us: power over our sleep, our appetites, our blood pressure, our health, and our happiness. —DALE CARNEGIE
Siku mpya, siku nzuri na siku ya kipeke sana kwetu.
Tumepata nafasi nyingine nzuri sana kwetu ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari CHUKI NI UTUMWA…
Swali la haraka haraka; ni kitu gani unakichukia kweye maisha yako? Ni watu gani unawachukia kweye maisha yako?
Tafakari hilo, na ukishapata jibu, basi jua kile unachochuki, wale unaowachukia ndiyo wanaokutawala wewe.
Kwa sababu huwezi kuchukia kitu au watu na uache kukifikiria kila wakati.
Tena ili chuki ifanye kazi, lazima mara kwa mara ujikumbushe kwa nini unamchukia mtu au kitu hicho, jambo ambalo linakufanya uendelee kujiumiza zaidi.
Chuki ni utumwa, chuki ni kuchagua kuwa chini ya wengine, chuki ni kukabidhi hisia zako kwa wengine na kuwaacha wafanye vile wanavyotaka wao. Mpango ambao siyo mzuri kabisa.
Maisha bora kwako, maisha ya uhuru kwako ni kuondokana kabisa na kila aina ya chuki.
Haijalishi mtu amefanya nini, kamwe usiwe na chuki dhidi yake. Haijalishi kit hakiendani na wewe kiasi gani, usiwe na chuki dhidi ya chochote.
Hata kama mtu amefanya kitu kibaya sana kwako, labda alitaka hata kukuua kabisa, usiwe na chuki.
Na kutokuwa na chuki haimaanishi ujilazimishe kumpenda hata kama upendo hauji. Badala yake jifunze kupotezea.
Yaani endesha maisha yako kam vile hakuna lilichotokea, fanya kama vile yule unayemchukia hata hayupo kabisa kwenye maisha yako, kama vile ni mtu aliyekwishakufa siku nyingi zilizopita.
Mara zote kuwa huru, kuwa na hisia na fikra chanya juu ya mafanikio yako kimaisha. Usikubali kabisa chuki ya aina yoyote iingie ndani yako.
Hata kama mtu kakufanyia ubaya kiasi gani, mpotezee, fanya kama vile hayupo kabisa, kama vile hakuna kilichotokea, na maisha yako yawe ndiyo kipaumbele cha kwanza kwako.
Uwe na siku bora leo, siku ya kuondokana na kila aina ya chuki kwenye maisha yako.
#Fanya #ChukiNiUtumwa #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa #WhatEverItTakes
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha